Na MANENO SELANYIKA –DAR ES SALAAM
HUKUMU ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Ephraim Mgawe na Naibu wake, Hamad Koshuma, imeahirishwa tena hadi Januari 6, mwakani.
Hili itakuwa ni mara ya pili kwa hukumu hiyo kuahirishwa, mara ya kwanza hukumu hiyo ilitakiwa kutolewa Oktoba 13, mwaka huu.
Kesi hiyo ilitajwa jana katika mahakama hiyo kwa ajili ya hukumu, lakini hakimu anayehusika, Syprian Mkeha, alitaja tarehe nyingine kwa kuwa alikuwa anasikiliza kesi nyingine.
“Leo ilikuwa ni siku ya kusoma hukumu ya kesi hii, lakini kuna kesi nyingine naendesha, hivyo nitapanga tarehe nyingine kwa ajili ya hukumu ya kesi hii,” alisema Mkeha.
Katika kesi hiyo, Mgawe na mwenzake inadaiwa Desemba 5, 2011, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC), bila kutangaza zabuni.
Aidha, katika hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kuweka saini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo ya Kichina bila zabuni shindanishi, ambapo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma namba 21 ya 2004, ambapo walitumia dola milioni 600.
Mbali na kesi hiyo, Mgawe na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi nyingine ambapo hivi karibuni walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusomewa shtaka la kuomba rushwa zaidi ya Sh milioni 8.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkurugenzi wa uhandisi TPA, Bakari Kilo, meneja wa manunuzi TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya DB Shapriya Ltd, Kishor Shapriya.