29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

HUKUMU YA SHILOLE ITUKUMBUSHE MAJUKUMU YETU

NA MWANDISHI WETU

MAHAKAMA ya Mwanzo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, juzi ilimhukumu msanii wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, kulipa faini ya shilingi milioni 14 baada ya kupatikana na hatia ya kutapeli na kusababisha hasara kwa kushindwa kufika kwenye onyesho lililoandaliwa na Mary Musa.

Shilole alilipwa kiasi cha shilingi milioni 3 ili atumbuize kwenye onyesho la mkesha wa Pasaka mwaka jana katika Ukumbi wa Mbagala Kijichi lakini hakufanya hivyo.

Tukio la Shilole kutotumbuiza katika onyesho hilo, liliibua hasira miongoni mwa mashabiki waliofika ukumbini hapo kiasi cha kufanya fujo na kuharibu mali huku wakisababisha hasara ya shilingi milioni 14 ambazo Mahakama hiyo imemtaka Shishi azilipe ndani ya siku 7 kuanzia Machi 1 mwaka huu.

Kupitia mkasa wa Shilole, tunaweza kujifunza kitu sisi kama mashabiki lakini pia wao kama wasanii na waandaaji wa maonyesho maana matukio kama haya yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwenye tasnia ya burudani.

Upande wa shabiki ambaye hulipa fedha yake ili kwenda kumtazama msanii anayempenda inakera sana linapoibuka suala la mwanamuziki huyo kutotokea ukumbini.

Japo ni ngumu ila tunapaswa kuzuia hasira na kudai haki zetu kwa waandaaji wa onyesho bila kufanya fujo au kuvunja sheria.

Wasanii nao wanapaswa kujifunza kuwa muziki umekuwa biashara, hakuna mtu anayekubali kula hasara kizembe, hivyo ukimsababishia hasara promota lazima akuburuze mahakamani ili apate haki yake.

Ni vyema kama unaona huwezi kutumbuiza, acha kupokea fedha. Au toa taarifa mapema kwa mwaandaaji wa onyesho ili promota afanye michakato ya kuepusha hasara.

Lakini pia waandaaji wa maonyesho wanapaswa kujifunza kutoka kwa promota huyu (Mary Musa) ni kutotaka kumalizana na Shilole kienyeji, amefanyiwa kosa, amekwenda mahakamani kutafuta haki yake.

Ni vyema tukumbuke kuwa muziki umekuwa biashara na kila kitu kilichopo ndani yake kinaendeshwa kihesabu. Wasanii wanapaswa kuelewa kuwa jukumu lao ni kuburudisha hivyo wasichezee kazi zao.

Mashabiki nao wana haki ya kupata burudani inayolingana na fedha waliyoitoa, lakini pia waandaaji wa maonyesho nao wanahitaji kupata faida kutokana na shoo za wasanii hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,220FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles