27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

HUKUMU VIGOGO TPA YAAHIRISHWA TENA

vigogo-tpa

Na TUNU NASSOR- DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kwa mara ya tatu kusoma hukumu ya kesi inayowakabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma, hadi Februari 10, mwaka huu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Willbroad Mashauri, alisema mahakamani hapo kuwa hakuachiwa hukumu na hakimu anayeendesha kesi hiyo.

“Hakimu anayehusika na kesi hii, Cyprian Mkeha, hakuniachia hukumu bali ameomba niiahirishe hivyo naiahirisha hadi Februari 10, mwaka huu,” alisema Mashauri.

Hukumu ya kesi hiyo inaahirishwa kwa mara ya tatu, mara ya kwanza ilitakiwa kutolewa Oktoba 13, mwaka jana na mara ya pili ilitakiwa kutolewa Novemba 25, mwaka jana.

Novemba 25, mwaka jana hakimu Mkeha aliahirisha kusoma hukumu hiyo kutokana na kuwa na kesi nyingine za kuendesha.

Katika kesi hiyo, Mgawe na mwenzake inadaiwa Desemba 5, 2011, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC) bila kutangaza zabuni.

Katika hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kuweka saini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo bila zabuni shindanishi, ambapo ni kinyume cha sheria ya ununuzi wa umma namba 21 ya 2004 na walitumia dola milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.3 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwaita mahakamani jumla ya mashahidi watano kujenga kesi yao, akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa TPA, Kokutulage Kazaura.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imeahirisha kesi ya kutakatisha fedha inayowakabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake wawili kutokana na kutokukamilika kwa ushahidi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon, waliokuwa wafanyakazi waandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania.

Washtakiwa hao watatu wanadaiwa kutakatisha fedha Dola milioni sita za Marekani (sawa na Sh bilioni 1.2) wakati Serikali ilipokopa Dola milioni 550 (takribani Sh trilioni 1.2) kati ya mwaka 2012 na 2013 kutoka katika Benki ya Standard ya Uingereza ambayo ni kampuni mama ya Stanbic.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles