Na Francis Godwin, IRINGA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Iringa leo inatarajia kusoma hukumu ya kesi ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo.
Nondo anakabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, mwaka huu akiwa eneo la Ubungo, Dar es Salaam na kuzisambaza kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp kwamba yupo hatarini.
Katika shtaka la pili, anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga alipokuwa anatoa taarifa kwa askari kwenye Kituo cha Polisi Mafinga kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto Mafinga.
Katika kesi hiyo Nondo anatetewa na mawakili wawili wakiongozwa na Jebra Kambole chini ya mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini (THRDC).
Julai 23, mwaka huu kesi hiyo iliendelea mbele ya Hakimu Liadi Chamshama ambapo shahidi wa sita, Fred Kapala alitoa ushahidi wake.
Katika ushahidi wake shahidi huyo ambaye ni mwanasheria kutoka Kampuni ya Mawasiliano ya Mtandao wa Tigo, alisema Machi 9, mwaka huu alipokea barua kutoka kwa mkuu wa upelelezi ikimtaka kuchapisha kumbukumbu za namba ya usajili na mawasiliano ya mshitakiwa.
Akijibu maswali ya wanasheria, shahidi huyo alisema katika upekuzi alioufanya kwenye kompyuta alibaini mawasiliano ya sauti kati ya namba ya mshtakiwa akiwa maeneo ya Ubungo jijini Dar es salaam huku mawasiliano ya mwisho yakifanyika saa kumi alfajiri ya Machi 8, mwaka huu.
Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake, upande wa Jamhuri uliiomba mahakama kupokea kielelezo cha kopi ya upekuzi kuwa sehemu ya ushahidi jambo ambalo liliwekewa pingamizi na upande wa utetezi huku wakitoa hoja tatu za kupinga kielelezo hicho na mwanasheria wa Nondo, Jebra Kambole, alipinga kupokewa kwa ushahaidi huo.