MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora inayosikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila inatarajia kutoa hukumu Mei 17, mwaka huu.
Jaji wa mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo mjini Kigoma, Ferdinand Wambali, alisema kuwa amepanga kutoa hukumu tarehe hiyo baada ya pande zote mbili kuwasilisha ushahidi na maelezo yao.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi huo, Jaji Wambari aliomba kupatiwa muda wa kutosha kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo ili aweze kutoa hukumu ya haki.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza, Ruben Mfune ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2015, Kafulila anaishawishi mahakama itengue matokeo yaliyompa ushindi aliyekuwa mgombea wa CCM, Hasna Mwilima badala yake imtangaze yeye kama mshindi halali wa jimbo hilo.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mbunge wa jimbo hilo Hasna, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza, Ruben Mfune ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria wa Serikali ambaye anaiwakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Katika kesi hiyo, Wakili Kenedy Fungamtama anamtetea Husna huku Kafulila akitetewa na mawakili watatu, Profesa Abdallah Safari, Tundu Lissu na Daniel Rumenyela.