HUDUMA ya usafiri wa Reli ya Kati iliyokuwa imesimama kwa takribani miezi miwili sasa imerejea baada ya kukamilika kwa ukarabati wa reli hiyo katika eneo la Kidete wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, baada ya kukagua na kuridhika na ukarabati uliofanywa katika maeneo ya Magulu, Munisagara, Mzaganza na Kidete wilayani Kilosa.
“Hakikisheni mnailinda reli hii kwa manufaa yenu na ya Taifa, leo (jana) reli iko vizuri na treni ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda bara itapita na kumaliza changamoto ya usafiri iliyokuwa inawakabili wananchi wanaotumia reli hii,” alisema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa, aliwataka wananchi wa maeneo ya Kilosa, Magulu, Munisagara, Mzaganza, Kidete, Godegodena Gulwe ambao maeneo yao yanakabiliwa na mafuriko ya Mto Mkondoa kuacha kilimo cha kuelekeza maji kwenye reli bali washirikiane na Serikali kudhibiti maji hayo kwenda kwenye hifadhi ya reli.
Alisema Shirika la Reli Tanzania (TRL), linaendelea kuhakikisha kuwa treni inayopita kwenye Reli ya Kati inapata mzigo mwingi wa kusafirisha kutoka bandari za Tanga na Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Mwanza, Kigoma na Mpanda na wafanyabiashara watumie fursa hiyo ili kupunguza mzigo unaosafirishwa kwa njia ya barabara.