24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Huduma ya uchunguzi wa kifua kikuu yafika vijijini Simiyu

Na Samwel Mwanga, Simiyu

KAMATI ya usimamizi wa huduma za Afya ya mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Afya imeanza kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wanaoishi kwenye mazingira duni na hatarishi.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Simiyu, Dk. Emanuel John wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bariadi.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoa wa Simiyu, Dk. Emanuel John akizungumza na Waandishi wa Habari hawako pichani juu ya ugonjwa wa Kifua kikuu.

Alisema kuwa mkoa huo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la MDH wameanza kampeni hiyo katika maeneo mbalimbali katika wilaya za Bariadi na Busega.

Alisema kuwa maeneo ya wilaya hizo yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu kutokana na hali duni za maisha pamoja na shughuli za kiuchumi kama vile uchimbaji madini na uvuvi.

Alisema kuwa kwa mkoa huo idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu imekuwa ikiongezeka kutokana na idadi kubwa ya wananchi kuishi kwenye mazingira hayo huku takwimu zikionyesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na idadi ya wagonjwa 2,700 na kufikia mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 3,600.

“Katika mkoa wetu maeneo ya wilaya ya Bariadi kuna machimbo ya madini na kuna wachinbaji wadogowadogo wengi na wilaya ya Busega kuna wale wavuvi wadogo wadogo wanaoishi kwenye makambi wanaishi kwenye maeneo hatarishi ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu.

“Hivyo tumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu ambao unaambukizwa kwa njia ya hewa na wakazi wake wengi kwenye maeneo hayo wanaishi kwenye makazi duni ambayo ni hatarishi na rahisi kupata ugonjwa huo,” alisema.

Alisema kuwa moja ya makundi hatarishi yaliyoko katika hatari ya kupata maambukizi ya kifua kikuu ni umaskini katika jamii ikiwamo kuishi chumba kimoja watu wengi, nyumba zisizokuwa na mwanga na hewa ya kutosha.

Alisema ndiyo maana Serikali ya mkoa kupitia wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na wadau wa maendeleo Shirika la MDH kwa pamoja imedhamiria kutokomeza kabisa ugonjwa huo kwa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao na kuwapima kwa kutumia gari maalum(Mobile van).

“Kwa kushirikiana na wadau wetu tunawafuata wananchi huko huko kwenye maeneo yao vijijini kwa kutumia gari maalum ambalo ndani yake lina Wataalam na vifaa vya kupimia na majibu yanatoka siku hiyo hiyo tukimgundua mtu mwenye maambukizi tunamwanzishia dawa mara moja,”alisema.

Aidha Dk John alisema kuwa katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa wameanza kwenda kila wilaya kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo ili jamii iweze kufahamu na kuchukua hatua ya haraka ikiwamo kuwahi hospitali kupata matibabu.

Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dk. Richard Marwa alisema kuwa kampeni hiyo itafanyika katika wilaya zote za mkoa huo na matumaini kuwa italeta tija kubwa na itasaidia kuokoa maisha ya watu ambao wameambukizwa ugonjwa huo lakini wameshindwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali.

Dk. Marwa alieleza kuwa ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na muhimu kwa mtu aliyepata ugonjwa huo kuwahi haraka ili kuepuka vifo na kuambukiza wengine.

Pia aliwaomba waandishi wa habari kuhakikisha wanatoa elimu juu ya ugonjwa huo kupitia vyombo vyao vya habari kwa lengo la kuelimisha jamii njia ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Nao baadhi ya wakazi wa wilaya hizo wameipongeza serikali kupeleka huduma ya uchunguzi katika maeneo yao kwani itasaidia sana kuokoa maisha ya watu wengi hasa wazee ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma.

“Kuna watu wanasumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu lakini wameshindwa kwenda kupata matibabu kwenye vituo vya Afya na Hospitali kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo nauli ya kutoka nyumbani kwenye maeneo ya kutolea huduma za afya na wengine kupoteza maisha,” alisema James.

Walisema huduma hiyo ni nzuri kwani inatoa majawabu ya shida za wananchi wenye maradhi ambao wana tabia ya kumeza dawa bila kupata ushauri wa madaktari.

Pia wametoa pongezi kwa watoa huduma kwa kazi wanaofanya ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi na kuwataka kuendelea kuwasaidia watu ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha ikiwamo maradhi ya mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles