27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Huduma saba za ubingwa wa juu zitakavyoibeba Tanzania SADC

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAENDELEO yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya yamepunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata matibabu ambayo yalikuwa hayatolewi hapa nchini aidha kutokana na kukosa wataalam wa kutoa huduma hizo au vifaa vya uchunguzi.

Huduma mbalimbali za ubingwa wa juu zimeanzishwa sambamba na kuimarishwa kwa uwezo wa wataalamu na vifaa tiba na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua katika sekta ya afya.

Baadhi ya huduma hizo za ubingwa wa juu ni zile zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Miongoni mwa huduma hizo bado nyingi hazipatikani katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ndiyo maana Tanzania inautumia mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaoendelea hapa nchini kuzinadi.

Mathalani huduma ya upandikizaji figo (kidney transplant) inayotolewa Muhimbili inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo katika Ukanda wa SADC ikitanguliwa na Afrika Kusini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema kupitia mkutano huo Tanzania itafaidika katika maeneo matatu ambayo ni kutoa huduma muhimu zikiwamo za dharura, kuwaonyesha wajumbe namna walivyopiga hatua kutoa huduma za kibingwa na suala la ununuzi na usambazaji dawa baada ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuteuliwa na jumuiya hiyo kuwa mnunuzi mkuu.

“Tutatumia mkutano huu kuwaeleza na kuwaonyesha wenzetu kwamba, Tanzania tumepiga hatua katika kutoa huduma za kibingwa hivyo, hawana haja ya kupeleka wagonjwa India au nje ya nchi za SADC wanaweza kuwaleta kwetu,” anasema Ummy.

Anasema maboresho yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya yamesaidia kupata wateja kutoka baadhi ya nchi za jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa Ummy, kwa mwaka MNH hupata wagonjwa 284 kutoka nchi mbalimbali za SADC na kila mwezi wanapata wagonjwa 24 kutoka nchi za Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Malawi.

“Tunaamini uwapo wa mkutano huu utaongeza pia idadi ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma nchini. Tumetumia Wiki ya Viwanda kuonyesha uwezo, ubunifu na utashi wetu wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya utalii wa kimatibabu.

Mfano wa kikombe cha mfupa wa nyonga ambacho kinahitaji utaalamu katika kufanyiwa matibabu.

“Kupitia Muhimbili tumeanza kupandikiza figo, vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto na huduma za radiolojia, huduma hizi na zingine zilikuwa hazipatikani hapa nchini na hata nchi mbalimbali za SADC,” anasema.

Kuhusu mfumo wa ununuzi wa pamoja wa dawa, alisema utasaidia kupunguza bei kwa zaidi ya asilimia 40 na kwamba Botswana, Lesotho, Shelisheli na Mauritius wako tayari kununua dawa kupitia utaratibu huo.

Huduma inazonadi

Katika mkutano huo, Tanzania imeendelea kunadi huduma mbalimbali za ubingwa wa juu zinazotolewa Muhimbili, MOI na JKCI.

Kwa upande wa Muhimbili mbali ya upandikizaji figo, huduma nyingine za ubingwa wa juu ni upandikizaji watoto vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant) na tiba kwa njia ya radiolojia (interventional radiology). 

Kwa upande wa MOI, huduma wanazonadi ni upasuaji wa mivunjiko ya kikombe cha mfupa wa nyonga, upasuaji wa kuweka nyonga na magoti bandia na upasuaji wa magoti, ubongo na mgongo kupitia matundu madogo.

Kwa upande wa JKCI, ni huduma za tiba ya umeme wa moyo, kuzibua mishipa ya damu na upasuaji wa kufungua kifua kwa ajili ya kurekebisha valvu au matundu katika moyo.

Maendeleo upandikizaji figo

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, zinaonyesha tangu huduma hiyo ilipoanzishwa nchini Novemba 2017, hospitali hiyo imeokoa Sh bilioni 3.5.

Anasema tangu walipoanza kutoa huduma hiyo, wagonjwa 47 wamepandikizwa figo na kugharimu Sh bilioni 1.1 na iwapo huduma hiyo ingefanyika nje ya nchi ingegharimu Sh bilioni 4.7.

“Kama wagonjwa wote hao wangepelekwa nje ya nchi kwa mgonjwa mmoja ingegharimu Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 wakati kwa hapa nchini unagharimu kati ya Sh milioni 25 hadi milioni 32,” anasema Aligaesha.

Kabla ya kuanza upandikizaji wa figo hapa nchini, Serikali ilipeleka wagonjwa takribani 230 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Mivinjiko ya kikombe cha nyonga

Huduma ya upasuaji wa mivunjiko ya mfupa wa nyonga na kiuno inapatikana katika nchi sita za Afrika yaani Tanzania, Kenya, Misri, Morocco, Afrika Kusini na Botswana.

Dk. William Mgisha kutoka MOI, anasema huduma hiyo imekuwa ikitolewa na taasisi hiyo kwa miaka 10 lakini uwezo umepanuka kwa maana ya vifaa na madaktari ambao wameongezeka kutoka wawili hadi wanne.

Dk. Mgisha anasema kwa wiki wana uwezo wa kufanya upasuaji kwa wagonjwa wanne hadi sita ambapo mmoja hufanywa kati ya saa sita hadi nane.

Kwa mujibu wa Dk. Mgisha, wengi wanakumbwa na tatizo hilo ni wale waliojeruhiwa kutokana na ajali za barabarani ama kuanguka.

“Tumetumia Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC kunadi huduma hii na nyingine ili kuwavutia nchi wanachama kuja kutibiwa katika taasisi yetu kwani tuna uwezo mkubwa na vifaa vya kisasa, huduma hizi zina gharama kubwa zaidi kama ukienda nje ya Afrika,” anasema Dk. Mgisha.

Anazitaja huduma nyingine kuwa ni upasuaji wa kuweka nyonga na magoti bandia, upasuaji wa magoti kwa matundu madogo, upasuaji wa mgongo na upasuaji wa ubongo wa aina mbili yaani bila kufungua fuvu na upasuaji wa kuziba mishipa ya damu inayovilia.

Kwa mujibu wa Dk. Mgisha, huduma hizo ambazo zimefanyika kwa zaidi ya miaka 15 katika taasisi hiyo ni zile zinazohitaji utaalamu wa hali ya juu na madaktari wabobezi na nyingi uwezo wake umepanuka.

Kuhusu huduma ya upasuaji mgongo, anasema wanafanya upasuaji wa vibiongo na mivinjiko ya mgongo kutokana na ajali na kwamba huduma hizo zinahitaji teknolojia ya hali ya juu kwa sababu zisipofanyika kwa umakini badala ya kumponya mgonjwa anaweza kupata ulemavu.

Kwa upande wa upasuaji ubongo, anasema hufanywa bila kufungua fuvu kwa baadhi ya vivimbe vilivyoko sehemu ya mbele ya ubongo karibu na pua.

“Upasuaji wa magoti hivi sasa hatufungui goti kama zamani, tunafanya kwa kutoboa matundu matatu. Tunaweka kamera ambayo daktari na mgonjwa wataona kwenye ‘screen’, unapitisha maji na kifaa cha kurekebisha sehemu ya goti iliyoathirika.

“Unaweza kufanyiwa operesheni hii na kurudi nyumbani badala ya kukaa wodini kwa wiki tatu kama ilivyokuwa hapo awali tulipokuwa tukifungua goti,” anasema Dk. Mgisha.

Hata hivyo, anasema huwa wanapata wateja kutoka baadhi ya nchi za SADC kama Malawi, Kenya na Shelisheli lakini hakuna machapisho ya kisayansi yanayoonyesha kama nchi nyingine zinatoa huduma hizo.

“Wengi wamekuwa wakipeleka wagonjwa India ndiyo maana tumeamua kuwaonyesha ili waje watibiwe kwetu kwa gharama nafuu,” anasema.

Uwezo wa wataalamu waimarishwa

Waziri Ummy anasema awali walikuwa na tatizo la miundombinu, vifaa na watalaamu lakini wameanzisha utaratibu wa kupeleka madaktari bingwa katika nchi mbalimbali kama vile Israel, Marekani, Saudi Arabia, Ujerumani na India kwa ajili ya kuwajengea uwezo zaidi.

“Wataalamu wetu wa ndani hususani madaktari bingwa wa upasuaji wamepata ujuzi wa kufanya upandikizaji wenyewe, na mwaka huu tumepata ufadhili wa kuwasomesha wataalamu kati ya 25 hadi 50 katika ubingwa wa hali ya juu,” anasema Ummy.

Anatoa mfano kwa JKCI ambayo awali wataalamu wa ndani walikuwa wanaweza kufanya upasuaji kwa asilimia 45 huku kazi nyingi zikifanywa na wataalamu wa nje lakini hivi sasa wana uwezo wa kufanya upasuaji mgumu wa moyo kwa asilimia 95.

Maeneo mengine tayari wamefikia asilimia 100 hususani wauguzi wa vyumba vya upasuaji, madaktari bingwa wa tiba ya magonjwa ya figo, wataalam wa vipimo vya maabara na radiolojia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles