Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Baada ya ukimya wa muda mrefu, mwongozaji na mwigizaji mahiri wa filamu kutoka Houston, Texas, Marekani, Alenga Elize maarufu kama Alenga The Great, amezindua filamu yake mpya ya Kiswahili inayokwenda kwa jina la Lost Love (Wolf in a Sheep’s Clothes).
Alenga, ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kupitia filamu zenye mvuto wa aina yake, ameendelea kuiwakilisha vyema tasnia ya filamu ya Kiswahili nje ya mipaka ya Afrika, akiwa miongoni mwa vinara wa Bondowood Movie Industry.
Akizungumza na mtanzania.co.tz, Alenga amesema filamu hiyo mpya imepokelewa kwa kishindo, na ndani ya muda mfupi imefanikiwa kufikia watazamaji maelfu kupitia chaneli yake ya YouTube.
“Lost Love ni filamu yenye maudhui halisi ya Kiafrika. Visa vya kusisimua, mapenzi ya dhati, na usaliti vimetawala. Ni kazi usiyopaswa kuikosa. Natoa shukrani za dhati kwa timu yangu ya Izack Productions na waigizaji wote waliovaa uhusika vilivyo kuhakikisha filamu hii inakuwa bora,” alisema Alenga.
Filamu hiyo inaonyesha uwezo mkubwa wa Alenga na timu yake katika kuleta simulizi zinazogusa maisha ya kila siku, huku wakichanganya utamaduni wa Kiafrika na hadithi zenye kuvutia kimataifa.
Alenga ameongeza kuwa mafanikio ya kazi zake yanampa motisha ya kuendelea kukuza na kuipambania tasnia ya filamu ya Kiswahili akiwa ughaibuni.
Mashabiki wa filamu za Kiswahili wanaweza kutazama Lost Love kupitia chaneli yake ya YouTube na kufurahia kazi hii iliyosheheni burudani na mafunzo kwa wote.