24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Hotuba ya Profesa Kabudi yawateka Wakenya

Mwandishi Wetu -Nairobi, KENYA

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, aliwateka Wakenya na hotuba yake akisisitiza waepuke ukabila.

Kabudi alisema hayo jana katika Ukumbi wa Bomas jijini Nairiobi, Kenya wakati wa uziduzi wa ripoti ya jopo la usuluhisho la Building Bridges Initiative (BBI).

Jopo hilo liliundwa kwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kufuatia tukio lao la Machi 9 mwaka jana walipojitokeza hadharani wakashikana mikono na kuzika tofauti zao za kisiasa.

BBI ilizunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi na makundi mbalimbali na baada ya takribani miezi 18, wamekabidhi ripoti ambayo Rais Uhuru anawataka Wakenya kusoma na kuwepo na mjadala wa kitaifa ili yatakayopitishwa yawe kwa manufaa ya nchi hiyo.

Akihutubia umati mkubwa wa viongozi mbalimbali, Kabudi aliwahimiza Wakenya kuachana na siasa za ukabila ili kufanikiwa kupata maendeleo na ukuwaji wa uchumi.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikiri Kenya imepiga hatua katika suala la maendeleo na ujasiriamali lakini ukabila bado ni changamoto ambayo inahitajika kushughulikiwa.

“Hakuna ubishi Kenya ni nchi nzuri sana, Kenya imebarikiwa na watu wenye nguvu, wabunifu, watu waliojawa na talanta na wafanyabiashara.  Kwanini watu wazuri kama hao wanawezaje kuruhusu kutawaliwa na ukabila?” alihoji Kabudi.

Aliwataka Wakenya kuiga Watanzania katika kanuni zao za umoja ili waweze kukuza uchumi na kufanikisha usawa katika usambazaji wa rasilimali.

“Hatutaingilia mambo yenu ya ndani lakini ikiwa tunaona kile mnachofanya ni hatari kwa maendeleo ya Afrika Mashariki, tutasema kwa sauti kubwa – wachani,” ameongeza Kabudi.

Umati mkubwa uliokuwa umetulia katika hotuba hiyo ya takribani dakika 25 ukilinganisha na waongeaji wengine, walisisimka na kumshangilia Waziri Kabudi ambaye pia aliwakonga Wakenya na jinsi alivyokuwa anaongea kwa Kiswahili.

Kabudi aliwakumbushia Wakenya undugu kati ya Tanzania na Kenya akisema baadhi ya makabila yaliyopo Kenya pia yapo Tanzania lakini tofauti baina ya nchi hizo mbili ni Tanzania hawaongei kuhusu ukabila.

 Alikumbusha kuhusu marehemu Waziri Joseph Mungai ambaye nchini kwake Kenya hakufahamika zaidi lakini alipanda katika vyeo vya uongozi nchini Tanzania hata kabla hajafikisha miaka 30.

Prof. Kabudi alisema Mungai alizaliwa katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya na kupanda hadi kuwa Waziri akiwa na umri mdogo.

“Kuna watu walizaliwa Kiambu na wakaja Iringa kufanya kazi kwenye mashamba ya chai na wazazi wa Mungai walikua miongoni mwao. Mungai alikuwa kijana mwenye nguvu ambaye alipata umaarufu katika umri mdogo.

“Mwaka 1972, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alimteua Mungai kama Waziri wa Kilimo akiwa na miaka 30. Uteuzi huo ulifanywa bila ya yeye kuwepo kwa sababu alikuwa masomoni Canada,” alisema Prof Kabudi

Alisema muda wote Mungai alikuwa na mawasiliano na familia yake Kijiji cha Gichungo, Kaunti ya Kiambu ambapo baadhi ya ndugu zake akiwemo Njoroge Mungai alikuwa daktari wa Hayati Jomo Kenyatta na mwingine ni Meja Jenerali Paul Mungai.

“Akiwa njiani kurudi Tanzania akitokea Canada, alipitia Kiambu ambapo alikaribishwa na ndugu zake Njoroge Mungai na Paul Mungai kabla ya kuja Tanzania,” alisema Kabudi akimkumbuka Waziri Mungai na kusisitiza uhusiano uliyopo kati ya Kenya na Tanznaia.

Mungai aliyezaliwa Oktoba 24, 1943 alifariki Novemba 8, 2016 na mazishi yake yalikuwa ya kitaifa ambapo miongoni mwa viongozi waliyohudhuria ni Rais Dk. John Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles