29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 11, 2024

Contact us: [email protected]

Hotuba ya Kikwete iliyoitikisa Malawi-2

Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akiwa na Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda.
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akiwa na Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda.

Na MICHAEL MAURUS,

AGOSTI 31, 2012 aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Jakaya Kikwete, alitoa hotuba ya aina yake ambayo iliitikisa Malawi na nchi nyinginezo majirani wa Taifa hilo na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Jambo lililowagusa wengi katika hotuba hiyo, ni pale alipozungumzia juu ya mpaka kati ya Tanzania na Malawi, ambao kwa miaka mingi kumekuwa na mgogoro wa chini kwa chini baina ya nchi hizo mbili juu ya wapi zinatengana katika Ziwa Nyasa.

Ni kutokana na kufahamu hilo, hasa baada ya Malawi kuanza kurusha ndege zao katika eneo la Ziwa Nyasa ambalo Watanzania tunaamini ni eneo letu, Kikwete aliona ni vema kuliweka sawa hilo.

Wiki iliyopita, tuliona jinsi Kikwete, alivyozungumzia juu ya suala zima la sensa na kudokezea juu ya mgogoro huo wa mpaka na Malawi. Hebu pamoja na mambo mengine, tuone chimbuko la mzozo huo. Endelea…

Chimbuko la mzozo

Ndugu Wananchi; Chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina ya nchi zetu mbili jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, ni makubaliano baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetu yaliyofanywa Julai Mosi, 1890.

Makubaliano hayo yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland Treaty) yalitiwa saini kule Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na Wajerumani.  Wakoloni hao walikubaliana kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wengine waliopakana nao.

Kwetu sisi hayo ndiyo makubaliano yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake.  Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu.  Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya Malawi.  Kwa upande wa Mto Songwe mpaka ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa Tanzania.

Ndugu Wananchi; Katika kipengele cha sita (Article VI) cha mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali popote kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi ya mahali hapo.

Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa.  Ilianzia kazi katika Mto Songwe kuhakiki mpaka baina ya nchi yetu na Malawi. Tume ilikubaliana kuhamisha mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati ya mto.  Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.

Tume iliendelea na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa mwaka 1910.  Tume iliendelea katika ziwa Jipe ambapo mpaka ulihamishwa pia hadi katikati ya ziwa.

Ndugu Wananchi; Bahati mbaya tume hiyo haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 – 1918.  Kama tunavyokumbuka, Waingereza na Wajerumani waligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini.  Baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa (The League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika. Hivyo, Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.

Ndugu Wananchi; Wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na kazi.  Matokeo yake, mwaka 1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka wa Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji, na kuuhamishia katikati ya ziwa.

Ndugu Wananchi; Jambo la kustaajabisha ni kuwa, Waingereza walioona umuhimu na busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi na Msumbiji, hawakuona umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi.  Inashangaza, kwa sababu wakati huo Uingereza ilikuwa mtawala wa nchi zetu mbili hivyo kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi, lakini hawakufanya hivyo.

Baya zaidi ni kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotaka kupatiwa ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa.  Watu walitaka ufafanuzi kwa sababu inasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa ziliweka mpaka katikati ya ziwa.  Lakini, kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.

Ndugu Wananchi; Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala la mpaka wa Malawi lilijitokeza tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati ule lilijulikana kuwa Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO).

Hoja ya Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpaka kuwekwa kwenye ufukwe wetu kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kando kando ya ziwa haki yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samaki na kupata manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya Serikali ya Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana wakati ule.

Hoja iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya Tanganyika ijadiliane na Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa Uingereza ili ufumbuzi upatikane.  Wakoloni hawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuru wake Desemba 9, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.

Usikose nakala yako ya Mtanzania Jumatano ijayo kupata jitihada zilizokuwa zimefanywa na Serikali tangu tulipopata uhuru kutatua utata wowote ambao ungejitokeza kuhusiana na mpaka huo.  +255 713 556 022

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles