30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Rufaa Musoma kukamilika mwakani

Na MWANDISHI WETU-MUSOMA

UJENZI wa Hospitali ya Rufaa ya Kwanga iliyopo Musoma mkoani Mara unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 15, unatarajiwa kukamilika Agosti 2020.

Hayo yalisemwa jana mjini Musoma na Kaimu Mkurugenzi wa Ubunifu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Margret Ezekiel wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula aliyefika kukagua maendeleo ya ujenzi.

Margret alisema jengo lenye mita za mraba 24,482 na majengo mengine ya pembeni yenye mita za mraba 1,039 lina sehemu kuu tatu zinazojumisha sehemu zenye ghorofa tano, nne na sehemu ya tatu ghorofa mbili.

Alisema kuwa ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ulianza Septemba mwaka huu na kuchelewa kuanza kwa mradi huo kulitokana na changamoto ya upatikanaji wa michoro ya kujengea pamoja na kutokamilika kwa mchakato wa kumpata mshauri mwelekezi.

“Jengo hili ambalo limepitia wakandarasi wawili kabla ya shirika letu kukabidhiwa, limefanyiwa maboresho ili kuwa na huduma zote kadiri ya hospitali ya rufaa inavyotakiwa,’’ alisema Margret.

Alisema kazi za ujenzi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na kupiga lipu maeneo yote ambayo hayatakuwa na marekebisho, kuvunja baadhi ya kuta na kuzijenga kwa mujibu wa marekebisho sambamba na kuandaa sehemu ya nyongeza.

Kwa upande wake, Dk. Mabula alisema kukamilika kwa jengo la Hospitali ya Rufaa la Kangwa itakuwa mkombozi kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambao watakuwa wakipata huduma za hospitali ya rufaa katika mkoa huo tofauti na sasa wanalazika kwenda hadi Bugando mkoani Mwanza.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa kufanikisha kutoa kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 15 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ambao ulisimama kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2011,’’ alisema Dk. Mabula.

Aliitaka NHC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kuchelewa kwa mshauri mwelekezi wa ujenzi wa jengo hilo hakucheleweshi ujenzi.

Katika hatua nyingine, Dk. Mabula ameitaka Kampuni ya Kiure Engineering inayojenga jengo la kitega uchumi la Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha inakamilisha ujenzi ifikapo Desemba 30.

Alisema ikiwa watashindwa kufanya hivyo mkataba wa ujenzi wa jengo hilo la Mkendo Plaza lenye ghorofa tano utavunjwa bila kujali kama kampuni hiyo imefikia asilimia ngapi na itatakiwa kurejesha gharama za ujenzi.

Hatua ya Dk. Mabula inafuatia kampuni hiyo kushindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo tangu kuingia kwa mkataba wa ujenzi mwaka 2015. 

Kwa mujibu wa mhandsi wa ujenzi wa jengo hilo, kampuni ya Kiure iliingia mkataba mwaka 2015 na ujenzi kuanza rasmi 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles