32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Mwananyamala yajivunia huduma za kibingwa

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM 

HOSPITALI ya Rufaa ya Mwananyamala inajivunia kuanzisha huduma za kibingwa sita katika kipindi cha miaka minne ambazo zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Kutokana na kuanzishwa huduma hizo, sasa hospitali hiyo inatoa huduma 10 za kibingwa zinazotolewa na madaktari bingwa 24.

Akizungumza wakati wa ziara ya kampeni ya ‘Tunaboresha Sekta ya Afya’ jana Dar es Salaam, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Musa Wamburi, alisema kutokana na huduma hizo kuimarika, wamekuwa wakiona wagonjwa 1,700 hadi 2,500 kwa siku.

“Mwaka 2015 tulikuwa na huduma nne za kibingwa, lakini sasa zimeongezeka, kadiri huduma inavyoongezeka pia idadi ya madaktari bingwa kama wa mifupa, upasuaji, mionzi, meno na uchunguzi wa wagonjwa inaongezeka, mwanzoni tulikuwa tunapokea wagonjwa 1,200 hadi 1,400 sasa idadi imeongezeka.

“Sasa hivi tuna vyumba vya upasuaji vinne, kina mama sasa wanapata huduma za haraka na rahisi, tulikuwa tunafanya upasuaji mara nane kwa siku, lakini sasa hivi tunafanya upasuaji mara 16 kwa siku moja,” alisema Dk. Wamburi.

Alieleza vifaa vya matibabu vya kisasa vimeongezeka kama Ultrasound tano na wagonjwa 60 wanapata huduma hiyo kwa siku.

Dk. Wamburi alisema pia kiwango cha upatikanaji dawa kwa sasa kimefikia asilimia 97, huku asilimia 93 ya dawa hizo zikipatikana kutoka Bohari ya Dawa (MSD).

“Tuna dawa muhimu zote tofauti na zamani, kutokana na hatua hiyo huduma zimeimarika, tunahakikisha kila mgonjwa anayetibiwa anapata dawa kwa urahisi na kwa wakati,” alieleza Dk. Wamburi.

Akizungumza huduma za uzazi, alisema jumla ya wanawake 12,000 walihudumiwa kwa mwaka jana huku kina mama wanaojifungua kwa siku ni 40 hadi 60.

“Vifo vya uzazi pia vimepungua, tulipata 12 kwa mwaka jana, miaka ya nyuma vifo vilikuwa vinaenda mpaka 17 hadi 20.

“Mwezi wenye kina mama wengi wanaojifungua ni wa tatu hadi wa tano, kipindi hicho kwa siku moja tunaweza kuzalisha wajawazito hadi 120 na kwa mwezi wanaweza kufika zaidi ya 900,” alisema Dk. Wamburi.

Alisema huduma zingine zinazopatikana ni uzalishaji gesi kwa kutumia kondo la nyuma (Placenta) ambayo imesaidia kina mama kupata maji ya moto.

“Pia tuna huduma za kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya. Hapa tunawapa dawa, na mpaka sasa waathirika 1,200 hadi 1,900 wamepona na uhalifu umepungua,” alisema Dk. Wamburi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles