Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
HOSPITALI ya Wilaya ya Ilala Kivule imeanza kutoa huduma ya upasuaji na huduma ya mama na mtoto baada ya Serikali kufunga vifaa vyote vinavyohitajika.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule, Amos Hangaya alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata hiyo kuhusu maendeleo yaliyofanyika ndani ya kata yao.
“Tunampongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayofanya, sasa hivi wakazi wa Kivule na maeneo mengine hawatapata shida ya kwenda mbali kutafuta huduma za afya huduma zote za matibabu zinapatikana katika Hospitali ya Wilaya.
Hide quoted text
“Vifaa vyote vya upasuaji vimeshafungwa, upasuaji umeanza wiki hii, huduma ya mama na mtoto inapatikana,”alisema Hangaya.
Alisema tayari kuna wodi ya wanaume na wanaume pale kunapokuwa na uhitaji wa kulazwa kwa ajili ya matibabu.
Hangaya alisema kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti , jengo la kuchomea takataka na mejengo mengine.
“Zilililetwa zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo, tunashukuru kazi inaendelea vizuri chini ya usimamizi wa bodi na mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo,”alisema.
Katika hatua nyingine alihamasisha wananchi kutunza mazingira , kutoa ushirikiano kwa wazoa takataka wanapofika kukusanya taka.
Aliomba wenye nyumba zenye mageti watoe ushirikiano kwa kutoa taka nje na kulipia huduma hiyo kwa wakati kila inapofika mwisho wa mwezi.
“Tulikuwa na mkandarasi wa kuzoa takataka Magereza lakini mkataba wao umeisha tumeweka Kampuni nyingine, tunaomba muwape ushirikiano,”alisema Hangaya.