Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana imeanza kampeni ya kutafuta Sh bilioni 3 kwa lengo la kuboresha miundombinu na kununua vifaa tiba kuwaokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).
Hospitali hiyo inahudumia watoto wengi wanaozaliwa kabla ya wakati ambapo ina vitanda vidogo 80 na vitano tu vinavyomuwezesha mama kulala na mtoto wake.
Akizungumza Agosti 17,2024 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk. Bryceson Kiwelu, amesema walibuni kampeni ijulikanayo kama ‘Rafiki wa Amana’ ili kuboresha miundombinu ya hospitali kwa kujenga wodi ya mama na mtoto pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo vitanda vya kisasa vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Dk. Kiwelu alikuwa akizungumza baada ya matembezi ya hisani yaliyoanzia Coco Beach hadi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ili kuhamasisha umma kuchangia fedha kufanikisha kampeni hiyo.
“Tulifanya utafiti na kubaini endapo mama atalala na mtoto wake (aliyezaliwa kabla ya wakati) ataweza kupata joto, kumnyoyesha mara nyingi na wanaweza kupona zaidi kulinganisha na watoto wanaolala peke yao, ndiyo maana tuliamua kuja na kampeni hii,” amesema Dk. Kiwelu.
Kwa mujibu wa Dk. Kiwelu, hospitali hiyo inahudumia wakazi zaidi ya milioni 1.5 kutoka Ilala na maeneo mengine ya jirani na inapokea rufaa kutoka vituo 226 vikiwemo vya serikali, binafsi na mashirika ya dini.
Naibu Waziri wa Afya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Dk. Godwin Mollel, ameipongeza Hospitali ya Amana kwa kubuni wazo hilo na kwamba Serikali tayari imetenga Sh bilioni 31 kuboresha hospitali hiyo na nyingine za Mwananyamala, Temeke, Mbagala na Chanika.
“Kabla ya uchaguzi tunaenda kuiona Amana mpya, wakuu wa mikoa maeneo mengine wajiongeze na kuunga mkono kampeni hii,” amesema Dk. Mollel.
Amesema maboresho mbalimbali yanayoendelea katika sekta ya afya yameleta matokeo chanya kama vile kupunguza vifo vya akinamama wakati wa kujifungua kutoka 556 hadi 104 na kuvuka malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kupunguza vifo 225 kufikia mwaka 2025.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila, amesema kuboreshwa kwa miundombinu ya hospitali hiyo kutasaidia kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili ili ibaki na mabingwa bobezi tu.
“Hili ni wazo la Dk. Kiwelu tunampongeza kwa kuwa ameona mbali, tusipoiboresha Amana tunapelekea mizingi mingi isiyo ya lazima kwenda Muhimbili…tunapookoa maisha ya mama na mtoto ndiyo tunajenga kizazi salama cha baadaye,” amesema Chalamila.