Derick Milton, Maswa
NOVEMBA 29, mwaka huu, Wilaya ya Maswa chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya hiyo Dk. Seif Shekalaghe, ilitangaza rasmi kuanzisha mfuko wa walimu, uliolenga kuwapatia mikopo midogo kwa ajili ya kujikimu.
Wakati akitangaza kuanzishwa kwa mfuko huo, Dk. Shekalaghe alisema sababu kubwa iliyowafanya kuja na jambo hilo ni inatokana na walimu wengi kukosa sehemu sahihi na rafiki za kuwapatia mikopo midogo.
Alisema walimu wengi hasa wilayani humo wamekuwa wakihangaika kupata mikopo na kulazimika kwenda kwa watu au kampuni binafsi zinazokopesha fedha mitaani.
Wengi wamepata matatizo, kwani asilimia kubwa ya walimu hawana kadi zao za benki (ATM), wakilazimika kuziweka reheni kama sharti la kupata mkopo.
Zimekuwa zikiwanyonya, mwalimu akihitaji mkopo lazima kadi yake ya benki (ATM) awaachie, siku mshahara ukitoka wanaenda pamoja benki kutoa fedha kisha unampatia ya kwake na riba hapo hapo tena kubwa.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo halmahuari hiyo iliamua kubuni njia sahihi ya kupamba na jambo hilo, ambapo iliamua kuanzisha Mfuko wa walimu ambao utachangiwa na walimu wenyewe kisha kukopa.
Mfuko ulioanzishwa utakuwa chini ya walimu wenyewe na unachangiwa na wao, utatumika kuwapatia mikopo midogo ambayo wamekuwa wakiipata kwenye kampuni binafsi, tofauti ni kwamba riba yake ni ndogo na hakuna sharti la kuacha kadi ya ATM.
Katika kuanza utekelezaji, mfuko huo ulizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, kwenye hafla ya kuwapongeza walimu wa wilaya hiyo kutokana na matokeo mazuri ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu.
Mfuko unaonekana utafanya kazi iliyokusudiwa na kuweza kuwasaidia walimu kukopa mikopo midogo ya kukidhi mahitaji yao, unyanyasaji hautakuwapo tena na badala bali kuwasaidia walimu wetu.
Tunawaomba walimu waache mazoea, waache kuweka rehani kadi zao, wao ni wasomi wasidhalilishe taaluma yao, utumie mfuko huo kufuta aibu hii iliyozagaa mitaani hadi wanafunzi wenu wanajua.
Naungana na Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka, ambaye mara baada ya kuzinduliwa kwa mfuko huo, alipiga marufuku walimu kwenda mitaani kukopa na atakayebainika hatua kali itachukuliwa dhidi yake.