25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Hongera RC Gabriel kwa utekelezaji agizo la Rais

KWA muda mrefu Rais Dk. John Magufuli ameonesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Wizara ya Madini, jambo ambalo limekuwa likimsukuma kufanya mabadiliko ya mara kwa mara.

Mara ya mwisho Rais Magufuli kufanya mabadiliko katika wizara hii, ilikuwa Januari 9, mwaka huu, alipomwondoa Angella Kairuki na nafasi yake kuchukuliwa na Doto Biteko.

Siku anamwapisha Biteko Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli alimpa maagizo mazito akimtaka kwenda kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wasiokuwa waaminifu ndani ya wizara hiyo.

Pia alimwagiza kuanzisha mara moja vituo vya kuuzia madini ili kusaidia au kupunguza utoroshaji madini na tatizo la upotevu wa fedha nyingi kutokana na wafanyabiashara wengi kukwepa kodi. Pia kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.

Alisema kwa kipindi kirefu Serikali imeruhusu wawekezaji na wachimbaji wadogo wachimbe dhahabu, lakini Wizara ya Madini haijawahi kujiuliza madini hayo yanauzwa wapi.

Lakini pia kama wanachimba na wanauza, Serikali inapata asilimia ngapi.

Katika sheria ya madini kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini ili kudhibiti upotevu unaojitokeza.

Leo si nia yetu kueleza mambo mengi, lakini tumeguswa na uongozi wa Mkoa wa Geita ambao umeutangazia umma kuwa keshokutwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atazindua rasmi soko la mnada wa dhahabu mkoani humo.

Kama tunavyotambua Mkoa wa Geita ndio unaozalisha  asilimia 40 ya dhahabu yote Tanzania, hivyo tunaamini ujio huu wa soko hili utakuwa mkombozi mkubwa  kwa wachimbaji na Serikali kwa ujumla.

Mkuu wa Mkuu wa Geita, Robert Gabriel anasema tayari ujenzi wa soko hilo umekamilika kwa asilimia 100 na kwamba vyumba vyote 15 kwa ajili ya wanunuzi vimeshapangishwa. Kwa hakika hii ni habari njema.

Anasema soko hilo litakuwa ni mojawapo ya masoko makubwa ya dhahabu barani Afrika, ukiachia mbali  lililopo Afrika Kusini na Botswana.

Katika hili tunasema RC Gabriel ameonesha anaweza, ametekeleza agizo la Rais Magufuli ndani ya wakati.

Sisi wa MTANZANIA tunaamini kuanza kwa soko hili kutasaidia kuinua mkoa huu kiuchumi, kwani unatarajia kupokea wawekezaji wengi katika sekta mbalimbali.

Ni matarajio yetu kwamba sasa wachimbaji wadogo wadogo wataondokana na changamoto ya masoko kwa sababu mengi yatakuwapo katika maeneo kama Rwamgasa, Nyarugusu, Katoro, Bwanga, Ushirombo, Msalala na Chato mjini.

Ni wazi ujio wa soko hili, utaongeza uzalishaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo.

Sisi MTANZANIA, tunachukua fursa hii kumpongeza RC Gabriel na timu yake ya mkoa kwa kazi ya ujenzi wa soko hili, huku tukiwahimiza wafanyabiashara ya madini sasa kulitumia, badala ya kuuzia vichochoroni.

Tunasisitiza hili kwa sababu fedha nyingi zilizokuwa zikipotea, sasa zitakuwa kwenye mikono salama na Serikali itapata kodi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,763FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles