25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hongera Rais Magufuli, tumaini la Watanzania

Na DONALD NDAGULA

Nianze kwa kukupongeza wewe binafsi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kwa ushindi wa kishindo ulioupata wa asilimia 84.4 kwenye uchaguzi uliopita wa Oktoba 28, mwaka huu bila kumsahau, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye naye alishinda kwa  kwa ushindi mnono.  

Pia nichukue fursa hii kuipongeza, Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Taasisi zote zilizohusika kusimamia uchaguzi huu  kwa ufanisi, uadilifu na weledi wa hali ya juu na kufanikisha mchakato mzima bila uvunjivu wa amani licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza.

Kwa namna yoyote ile ufanisi wa Taasisi zetu za Serikali umeonekana wazi kwa wananchi na duniani kote, katika makala yangu ya Oktoba 28, kwenye gazeti hili kwa dhati kabisa niliwasihi Watanzania wote wamchague, Dk. Magufuli na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kazi nzuri iliyofanywa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ya uongozi wake kwenye maeneo mbalimbali ya uchumi na ustawi wa jamii, hivyo kupelekea Tanzania kuingia kwenye Uchumi wa Kati.

Binafsi na Watanzania wenzagu wenye mapenzi mema  na nchi yetu tumetiwa moyo na matokeo ya ushindi wa kihistoria wa Dk. Magufuli na chama chake, waswahili husema “Chanda chema huvikwa pete”, na  ndivyo walivyofanya Watanzania kwa kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na historia ya  mafanikio yao na kwamba wana uwezo wa  kutuletea maendeleo ya kweli.

Ushindi huu ni ushahidi na ishara tosha ya rais kukubalika na kuaminika na Watanzania na hivyo atabaki kuwa ni tegemeo lao.

Kimsingi, Watanzania wamepima na kuridhika na utendaji wa rais na chama chake na kuamua kumpa tena miaka mitano ili aweze kuongoza na kukamilisha miradi aliyoianzisha mwenyewe.

Muhula wa pili wa awamu hii ya tano ya uongozi ulioanza Jana Novemba 5, 2020 baada ya rais kuapishwa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, unatarajiwa kufanya maendeleo makubwa zaidi  ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na kwamba Tanzania imekwishaingia kwenye Uchumi wa kati kabla ya muda wake.

Aidha, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Bashiru Ali katika hafla ya rais kukabidhiwa Cheti cha Ushindi wa UchaguziNovemba 1,  kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Tume aliwaasa wanachama CCM, “Kuchukulia ushindi huo kama deni”na hivyo kujipanga juu ya  utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya (CCM) 2020-2025.

Hata hivyo Watanzania wanatambua kuwa uongozi wa muhula wa kwanza wa awamu ya tano unaanza wakati nchi imekwisha piga hatua kubwa ya kiuchumi, pamoja na uwepo wa janga la ugonjwa wa corona duniani.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyotolewa Julai, mwaka huu, Uchumi wetu utaweza kukua kwa kasi ya asilimia 5.5 chini ya malengo ya awali ya asilimia 6.9 kutokana na hali ya mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na janga la corona. Aidha, mfumuko wa bei kwa sasa ni asilimia 3.4 huku deni la taifa bado likiwa ni himilivu na akiba ya fedha za kigeni ikivuka kiwango kilichowekwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa kiwango cha SADC.

Hivyo changamoto kubwa ni kuendeleza jitihada za kujiletea maendeleo kwa kukamilisha miradi iliyopo na kwa kasi iliyo endelelevu, hapa nitoe wito kwa wananchi wenzagu kuwa tuendelee kumuunga mkono kwa dhati rais wetu na serikali yake.

Rais aliishasema “Ushindi huu ni wa Watanzania wote” na hivyo  kutoa rai ya dhati  kuwa yuko tayari kushirikiana wa wananchi wote wakiwemo wapinzani ili mradi kuiletea nchi maendeleo.

Aidha, kwa sasa kauli na maelekezo  ya msisitizo ya rais baada ya kuapishwa ni kuwa “uchaguzi sasa umekwisha na jukumu kubwa lililo mbele ni kujenga taifa letu” MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA.

Donald Ndagula ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma – MSTAAFU na Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi Mtiifu, anapatikana kwa namba: 0754 290 084

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles