HONGERA NASH MC KWA KUSIMAMIA UKUAJI WA KISWAHILI

0
1149

NA CHRISTOPHER MSEKENA

WIKI hii imekuwa njema kwa msanii mwenye misimamo mikali juu ya utamaduni wa hip hop nchini, Mutalemwa Jason ‘Nash Mc’, ambapo amepata shavu la kuhudhuria kongamano la 30 la lugha ya Kiswahili nchini Ujerumani, katika mji wa Beyreuth.

Kongamano hilo linayakutanisha mataifa zaidi ya 24 na watu wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku likijumuisha wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali za lugha ya Kiswahili.

Nash Mc anakuwa msanii wa kwanza wa hip hop kutoka Afrika Mashariki kupata nafasi ya kuhudhuria kongamono hilo, huku akipata shavu la kutumbuiza hip hop mubashara, hivyo kuzidi kutengeneza nguvu ya ushawishi kwa vijana wa sasa na baadaye.

Mwasisi huyo wa taasisi ya Kiswahili na Sanaa (KINASA), mbali na kutumbuiza kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya kongamano hilo la Kiswahili, amepata wasaa wa kushiriki mjadala wa uhusiano wa lugha na maarifa.

Na katika mjadala huo, Nash Mc atachambua kuhusu utamaduni wa hip hop na ushirikiano wake na lugha ya Kiswahili katika kuwapa watu maarifa, hivyo kupata jukwaa pana la kusimamia ukuaji wa lugha hii adhimu.

Kongamano hilo limemkutanisha Nash Mc na wazungu wanaoongea lugha ya Kiswahili kama wamezaliwa Tandale na maeneo mengine kama hayo yanayoitumia lugha hii kwa asilimia kubwa, hivyo kuonyesha namna Kiswahili kinavyokubalika.

Ikumbukwe Ujerumani ni moja ya nchi zinazopenda na kuthamini utamaduni wa Afrika, lakini pia ni nchi ambayo ipo juu katika masuala yanayohusu hip hop.

Hii ni hatua nyingine muhimu katika lugha ya Kiswahili na tamaduni za hip hop nchini. Naamini Nash Mc amekwenda kuliwakilisha Taifa na madini atakayoyapata huko atajaribu kugawana na vijana wa Tanzania.

Nafahamu Taasisi ya KINASA ilivyo mstari wa mbele katika kuikuza lugha ya Kiswahili. Baada ya safari hiyo itakayochukua siku saba, Nash Mc ataunganisha nguvu na wachanaji wenzake kupitia jukwaa la KINASA ili waweze kufikisha kile kinachostahili kwa jamii.

Hongera nyingi ziende kwa msanii huyu kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia misingi ya hip hop na kuitumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zake za sanaa na huu unaweza kuwa mfano bora kwa wasanii wengine wanaodharau Kiswahili katika kazi zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here