24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

HONGERA FATMA KARUME, RAIS MPYA TLS

Na, HUSSEIN JUMA, SHINYANGA


MBIU ya ushindi wako ilipopigwa, hakika Watanzania wa aina yangu tuliinuka kuimba sifa zako. Si tu kwamba una haiba ya ucheshi, ukarimu na kuheshimu mkubwa na mdogo, lakini pia kwa utashi wako wa kumsaidia kila Mtanzania mwenye uhitaji wa msaada wa kisheria; si kwa maneno, bali kwa maneno na vitendo halisi.

Fatma Karume, hongera sana kwa kuchaguliwa kwako kuwa mrithi wa mikoba ya Tundu Lissu ambaye licha ya muda mchache  alioutumia kukitumikia chama cha wanasheria, lakini amekuwa ni zaidi ya kioo, kwani kupitia yeye, Watanzania wa hali ya chini kabisa wamepata kuelewa mambo kadha wa kadha hata yahusuyo sheria, ambayo kimsingi ni vigumu kuyatenganisha na siasa.

Fatma Karume, Rais mpya wa TLS. Yapo mambo mengi ambayo Watanzania tunayatarajia kutoka kwako. Watanzania sasa tunakutegemea kwenye masuala ambayo aidha kwa weledi wako wa kazi au ujuzi wako wa sheria, yatapata suluhu. Hapa ninayo masuala machache, kati ya mengi, ambayo naamini ni tatizo kwa Tanzania na Watanzania.

Utawala wa sheria. Demokrasia, haki za msingi za Watanzania ndani na nje ya Tanzania. Msaada wa kisheria kwa watu wa chini; haya ni mambo manne ambayo hakika Watanzania tunahitaji utatuzi wa haraka sana.

Utawala wa Sheria.

Utawala wa sheria nchini una historia yake. Mengi yamezungumzwa sana hapa, lakini nataka kutolea mfano mmoja peke yake. Nimemsikiliza vizuri sana Zitto Kabwe akichambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kati ya mambo manane aliyoyasema, lipo suala la kukosekana kwa tija ya Bajeti zinazopangwa kwa sasa. Zitto, kutokana na taarifa hiyo ya CAG, alisema, kwa sasa Bajeti za Tanzania si ‘credible’ tena. Maana yake ni kwamba, Bajeti zinapangwa, lakini kuna Bajeti nje ya Bajeti inaundwa. Na hii Bajeti nje ya Bajeti, kimsingi haipo kisheria, ndiyo inayotekelezwa zaidi kuliko Bajeti iliyopitishwa na chombo chenye dhamana hiyo.

Kama Bunge lilitoa ukomo wa kukopa, Bajeti nje ya Bajeti ikakopa bilioni 500 zaidi ya ukomo huo, bado pia hili ni suala ambalo linahitaji mwarubaini ili tuweze kupata Tanzania ya kuigwa. Kwangu mimi kama Mtanzania wa chini, kwanza umoja wetu kama Tanzania ndiyo mwarubaini, lakini umoja huu ni lazima uende sambamba na ujuvi wa masuala yahusuyo sheria ili kila mwananchi aweze kuelewa nini hasa kinaendelea, vinginevyo mwananchi huyu ataendelea kusema tu ‘Maisha magumu’, kumbe kuna visababishi vya ugumu na moja likiwa ni kukosekana kwa utawala wa sheria.

Tuna vyombo mbalimbali ambavyo mimi nimekuwa nikivisifu kwa utendaji kazi kwa uhodari. Kwa mfano, mimi ni ‘ferminist’, ukiachilia mbali jinsi yangu. Ustawi wa Jamii, Mahakama na Dawati la Wanawake Jeshi la Polisi, ni baadhi ya vyombo ambavyo sikuwahi kusikia vimeshindwa kusikiliza kinamama waliotelekezwa. Cha ajabu, leo Mkuu wa Mkoa ndiye amechukua jukumu la kusikiliza kinamama hao, tena hadharani kabisa. Mimi nafikiri si sawa. Kwa kuwa umepata dhamana hii, Fatma Karume, tunaomba sana, tena sana, kwa ujuzi wako wa sheria na ujasiri wako, urudishe hadhi ya vyombo hivi ili viendelee kufanya kazi kadri sheria inavyoelekeza, ili tuwe na Taifa linalothamini utu kulingana na sheria ilivyo. Vyombo hivi havikuwekwa kwa bahati mbaya. Na kinachoendelea kwa sasa, vyombo hivi vinakosa maana ya kuwapo kwake na badala yake kesi zihusuzo masuala ya kinamama zinageuka kuwa fimbo kwa ‘critics’; fimbo ambayo kimsingi inaondoa kabisa utawala wa sheria.

Fatma Karume. Mimi kama Mtanzania nimepata matumaini kedekede kusikia kwa maneno yako mwenyewe ukionesha kulijua suala hili kuwa, kwa sasa Taifa linaongozwa kwa ‘decree’; kitu ambacho tunarudi kwenye Uingereza ya zamani kwamba, Mwili wa Mfalme ndiyo Katiba na maneno yake ndiyo sheria.

Demokrasia. Mtanzania ambaye amefuatilia vizuri chaguzi ndogo za marudio kuanzia kata 43 na majimbo mawili, basi atakubaliana na mimi kuwa, kwa sasa demokrasia Tanzania ni mahututi. Watu wamepigwa, wameumizwa, wameuawa na wapo pia ambao wametishiwa maisha kiasi kwamba demokrasia kwao imekuwa ghasia.

Katiba yetu pia, ibara ya 18 (1) na (2), inaeleza Uhuru wa kutoa maoni. Kifungu kwanza inampa Uhuru kila aliye Mtanzania kuwa na haki ya kujieleza, kutoa maoni, kutafuta taarifa na kuzijadili bila kuingiliwa kwenye mawasiliano yake. Lakini kifungu cha pili kinampa mwananchi haki ya kujulishwa matukio yote yahusuyo jamii yake na yaliyo muhimu kwa jamii yake.

Ibara ya 23, hasa kifungu cha pili, kinasema kuwa, kila mtu anayefanya kazi anastahili ujira sawasawa na kazi yake. Waraka wa Utumishi wa Umma wa Machi 28 ambao ulielekeza kuanza kutumika Aprili Mosi, mwaka huu, umemdhulumu mtumishi haki yake ya msingi kabisa. Waraka ule umefuta madaraja ambayo, kwa mfano Mwalimu, alipanda kisheria mwaka wa fedha 2015/2016 na siku chache baadaye kunyang’anywa madaraja yale kutokana na kile kilichoitwa ‘ukaguzi wa vyeti feki’.

‘Annual Increments’, ambazo zipo kisheria, kwa sasa ni kama hisani ya mfumo. Yaani, walimu wanapata kana kwamba mtu mmoja ndiye mwenye kuwafanyia hisani, asipotaka, basi hawapati.

Msaada wa kisheria kwa watu wa chini pia ni tatizo. Wapo watu, kwa mujibu wa viongozi wachache ambao wamewahi kuwekwa jela, wamefungwa kwa kesi zisizo na msingi na hawana watetezi. Hili linawanyima haki zao za msingi kama Watanzania.

Nimalize kwa kusema kwamba,  Fatma Karume, Watanzania tunakupenda na tunakuombea Qudra za Allah ziwe pamoja na wewe. Nchi hii ni nchi yetu sote na sisi kama Watanzania, kwa umoja wetu, tunalo jukumu la msingi la kuhakikisha tunakuwa na nchi imara inayowapenda wananchi wake.

Nchi ambayo ipo kuwatetea wananchi wake na si kuwanyanyasa wananchi wake. Nchi ambayo raia atajivunia kuwa raia na si kuvumilia kuwa raia. Nchi ambayo itaheshimu haki za raia na si kuzifanya haki za raia kama hisani ya mtu mmoja. Nchi ambayo itafikia malengo yake kwa uamuzi wa wengi na si uamuzi wa mtu mmoja. Nchi ambayo itaheshimu wataalamu wa kada mbalimbali na si wataalamu kutumika kama miavuli ya chama fulani pekee. Nchi ambayo itakuwa ni suluhisho kwa Watanzania maskini bila kujali wanatoka wapi, na si nchi ambayo inajali Watanzania Maskini wa eneo moja. Mimi sina mengi, ila naamini Fatma Karume utakuwa upande wa Watanzania. Utalia na Watanzania. Utasaidia Watanzania.

Nakutakiwa kazi njema na Allah akupe wepesi katika utekelezaji wa majukumu yako.

Tel: 0739 947 397

Email: [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,268FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles