24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

HONGERA AY, WASANII WENGINE MNASUBIRI NINI?

NA MWANDISHI WETU

HABARI kubwa kwenye tasnia ya burudani wiki hii ni tukio la staa wa Bongo Fleva, Ambwene Yessaya ‘AY’  kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake wa siku nyingi mwenye asili ya Rwanda, anayefahamika kwa jina la Remy.

Ni tukio lililotokea ghafla, amewashangaza mashabiki zake, hasa ukizingatia AY ni miongoni mwa wasanii wachache ambao wamejitahidi kutochanganya maisha ya kawaida na yale ya ustaa uliotokana na sanaa.

Unaweza kuona ni namna gani ambavyo AY anaendelea kuwa mfano bora na wa kuigwa kwa wasanii wenzake, ambao wengi wao huishi zaidi maisha ya kistaa, hata kwenye maisha halisi, kitendo kinachofanya wawe na taswira mbaya kwa jamii.

Staa huyo wa singo ya Zigo amefanya tukio la kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake raia wa Rwanda ikiwa ni siku chache baada ya kaka yake kimuziki na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, kufunga ndoa iliyowavutia vijana wengi, hasa wasanii.

Profesa Jay alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, Grace Mgonjo, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, siku ya Jumamosi iliyopita na kufuatiwa na sherehe kubwa na ya kifahari iliyowakutanisha watu maarufu kutoka kwenye sekta mbalimbali.

Sherehe hiyo iliwakusanya wasanii wa muziki na filamu, wanasiasa na wabunge kutoka kwenye vyama mbalimbali, tukio lililovuta hisia za watu wengi ambao wamekuwa wakifuatilia harakati za mkongwe huyo wa muziki wa hip hop nchini.

Tunaweza kusema AY alivutiwa na tukio lile, akaona naye afanye kweli kwa kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake huyo aliyemtambulisha Desemba, mwaka jana, wakati wa sherehe ya kumbukumbu siku yake ya kuzaliwa.

Ikumbukwe kuwa, moja ya vitu ambavyo vinatia doa sekta ya sanaa ni pale ambapo wasanii wake wamekuwa wakitoka kimapenzi na watu tofauti tofauti, jambo ambalo limepelekea muziki, hata filamu kuonekana ni ulingo wa watu kufanya uhuni.

Jambo ambalo Profesa Jay, AY na hata wengine ambao  wameoa na kuolewa wameendelea kuthibitisha ni kuwa sanaa si uhuni, bali ni kazi, kwani ina watu wenye heshima zao kama sekta nyingine.

Nadhani baada ya AY kumvika pete ya uchumba mpenzi wake, vijana wengine wa Bongo Fleva nao watafuata mfano huu muhimu na kuacha kuishi maisha yanayowapunguzia heshima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles