LRAMADHAN HASSAN, DODOMA
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, imeyataja magonjwa 10 yaliyochangia vifo vya watu 20,087 mwaka 2018 huku homa ya mapafu ikiwa kinara na shinikizo la damu likiingia kwa mara ya kwanza katika orodha hiyo.
Orodha hiyo ilitajwa jijini hapa jana na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alipozungumzia hali ya huduma ya afya nchini katika kipindi cha mwaka jana.
Alisema takwimu zilizokusanywa kupitia mfumo wa DHIS2, zimeainisha kuwa mwaka jana kumetokea jumla ya vifo 20,087 ikilinganishwa na vifo 19,693 vilivyotokea mwaka juzi vilivyosababishwa na magonjwa hayo.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili (2017 na 2018), homa ya mapafu imeongoza kwa kusababisha vifo ambapo mwaka jana ilichangia asilimia 18.2 ya vifo vyote.
Alisema mwaka jana ugonjwa huo ulisababisha vifo kwa watu 2,590 na ulichangia kwa asilimia 12.9 ya vifo vyote.
Pia alisema mwaka jana, ugonjwa wa shinikizo la damu umejitokeza katika magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo baada ya kuchangia kwa asilimia 1.9 ya vifo vyote.
Aliyataja magonjwa mengine na idadi ya watu iliyoua katika mabano kuwa ni ugonjwa wa moyo (1,253), kifo cha mtoto tumboni (ngozi imechubuka) (766) sawa na asilimia 3.8.
Mengine ni malaria (693) sawa na asilimia 3.4, Ukimwi (605) sawa na asilimia tatu, kifo cha mtoto tumboni (540) sawa na asilimia 2.7, magonjwa mengine (538) sawa na asilimia 2.7.
Alisema maambukizi katika damu (496) sawa na asilimia 2.5 na shinikizo la damu (382) sawa na asilimia 1.9.
Pia alisema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto na kwa mwaka jana jumla ya wajawazito zaidi ya milioni mbili walihudhuria kliniki.
Aliitaja mikoa ambayo mahudhurio ya kliniki kwa wajawazito yapo chini na asilimia katika mabano kuwa ni Mara (40), Njombe (40), Simiyu (41), Iringa (45), Tanga (46), Dodoma (47) na Ruvuma (49).
Pia alisema huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto iliendelea kutolewa ambapo na kwa mwaka jana asilimia 97 ya wajawazito walipima ikilinganishwa na asilimia 95 ya mwaka juzi.
“Katika wajawazito waliopima VVU ni asilimia 3.9 waligundulika kuwa na VVU na kati ya hao waliogundulika asilimia 99 walianzishiwa dawa za ARV’s,” alisema.
Pia alisema watoto chini ya mwaka mmoja walipatiwa huduma za chanjo ili kuzuia magonjwa yanayowaathiri ikiwamo ugonjwa wa kupooza, kuharisha, pepopunda, preumonia, homa ya ini na surua.
Alisema katika kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka jana hospitali za rufaa za mikoa zilihudumia jumla ya wagonjwa 3,526,503, kati yao wa nje walikuwa 3,054,318 na wa ndani 472,185.
Kuhusu malaria, alisema idadi ya watu 5,769,837 waligundulika kuwa na ugonjwa huo mwaka 2018 ukilinganisha na 5,595,916 kwa mwaka juzi.
MWISHO
Kigwangalla aivunja Bodi ya TTB
Na Loveness Bernard, Dar es Salaam
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kutokana na kushindwa kutekeleza maagizo ya wizara kwa wakati.
Akizungumza Dar es Salaam jana alipotembelea bodi hiyo, Kigwangalla, alisema amefanya uamuzi huo kutokana na kutokutekelezwa maagizo yake aliyotoa kwa TTB mwaka mmoja uliopita.
“Kuanzia leo (jana) naivunja bodi ya wakurugenzi isipokuwa mwenyekiti wake tu, nawapa muda watendaji kutekeleza maagizo yangu,” alisema Kigwangalla.
Pia alihoji suala la kuwekwa mabango yanayotangaza utalii katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam ikiwamo katika eneo la ofisi za bodi hiyo na kuweka majarida ya utalii katika ndege za Tanzania.
“Niliwaagiza muweke majarida katika ndege zetu na mabango sehemu mbalimbali yanayotangaza utalii, juzi nikitoka jimboni nilipanda ndege na baadhi ya abiria walinifuata na kuniuliza kwanini hatuna majarida yanayotangaza vivutio vyetu,” alisema Kigwangalla.
Katika hatua nyingine, aliitaka TTB kutumia watu maarufu kama vile Judith Wambura maarufu kama Lady Jay Dee, Ali Kiba, Barnaba, MwanaFa, Millard Ayo, Mbwana Samatta, Diamond Platinumz na wengine wenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii kutangaza utalii kwa kuwapa safari katika vivutio mbalimbali.
Pia aliitaka bodi hiyo kuwatumia wapiga picha waliopo nchini kwa kuwapa safari za mbugani ili wapate picha za matukio mbalimbali kwa ajili ya chaneli ya utalii.
“Chaneli yetu tangu imeanza kuruka ina wiki chache tu lakini tunarudia mikanda ile ile kwa maana hatuna footage za kutosha imefikia kipindi mtumie hawa wapiga picha kwa kuwapa ziara na footage mzipate kwa ajili ya chaneli yetu,” alisema.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa TTB, Godfrey Meena, alisema majarida yanayotangaza utalii yameshachapishwa pamoja na flashi na yote bado yako bandarini yanasubiri kulipiwa ushuru.
“Majarida tumeyachukua jana na tunatarajia kuyasambaza haraka na kuna flashi zipo bandarini zinasubiri kulipiwa ushuru kwa sababu zilitengenezwa nje kutokana na oda ilikuwa kubwa, hakuna kampuni nchini iliyoweza kukidhi mahitaji yetu ikatulazimu kuagiza nje,” alisema.
Pia alisema baadhi ya taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili ikiwamo Ngorongoro, Tanapa, Tawa na TFS hazijawasilisha michango yao kwa ajili ya uanzishwaji chaneli hiyo.
“Ni TTB tu tumetoa mchango wetu kwa ajili ya uanzishwaji wa studio, tumenunua samani na kompyuta yenye server kubwa, changamoto ni kwamba wenzetu bado hawajawasilisha michango yao,” alisema.