26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Homa ya ini tishio

  • Watu 13,613  wabainika kuugua, hadi sasa hakuna dawa

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WACHANGIAJI damu 13,613 kati ya 307,835 waliojitolea damu mwaka 2018 wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini B.

Ugonjwa wa homa ya ini husababishwa na virusi aina ya hepatitis ambavyo hushambulia ini na vipo katika makundi ya A, B, C, D na E.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Catherine Sungura, maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini B ni asilimia 4 miongoni mwa Watanzania.

“Utafiti ujulikanao kama Tanzania HIV Indications Survey (THIS) ulioratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2016/17, ulionesha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini B ni asilimia 4 miongoni mwa Watanzania wenye umri kati ya miaka 15-49.

“Hivyo kutokana na takwimu hizi mbalimbali hali ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya Ini aina ya B nchini inakadiriwa kuwa kama asilimia nne,” alisema Sungura katika taarifa hiyo.

Alisema vipimo vilivyofanyika kwa watoaji damu 307,835 mwaka 2018, vilibaini uwapo wa maambukizi ya virusi vya hepatitis B kwa watu 13,613 sawa na asilimia 4.4 na uwapo wa maambukizi ya hepatitis C kwa watu 1,092 sawa na asilimia 0.35.

Alisema utafiti uliofanyika mwaka 2017, iligundulika kuwa kati ya wachagiaji damu 233,953 asilimia 4.9 sawa na watu 11,417 walikuwa na maambukizi ya homa ya ini aina ya B.

DALILI

Sungura alisema mtu anaweza kupata maambukizi ya homa ya ini na asioneshe dalili yoyote na watu wengi hawaoneshi haraka dalili za maambukizi kwa kipindi cha awali cha ugonjwa huo.

Alizitaja dalili za ugonjwa wa homa ya ini zinaonekana pale ambapo ugonjwa unakuwa umekolea mwilini, ambapo ni pamoja na ngozi na macho kuwa na ragi ya njano, wakati mwingine hata mkojo huwa wa njano, kukosa nguvu, kichefuchefu na kutapika.

Alisema dalili nyingine ni homa, tumbo kuuma upande wa juu kulia, na kuumwa kichwa. Kwa baadhi ya watu wachache wenye ugonjwa huu ini hushindwa kufanya kazi na kuleta madhara makubwa zaidi na hata kusababisha kifo.

TIBA

Sungura alisema kuwa hadi sasa hakuna tiba mahususi kwa kwa watu waliogundulika kuwa na Hepatitis B na kwamba matibabu anayopewa mgonjwa ni ya kumwezesha kupata nafuu  na kumpa lishe inayostahili na kumwongezea maji anayopoteza mwilini kwa kutapika na kuharisha.

“Zipo dawa za kupunguza makali ya virusi vya Hepatitis B ambazo mgonjwa anatakiwa kutumia kwa kipindi chote cha uhai wake.

“Virusi vya homa ya ini aina ya C, tiba ipo ingawa gharama yake ni kubwa na inachukua muda wa miezi mitati hadi sita kukamilisha matibabu,” alisema

TAARIFA POTOFU

Alisema hivi karibuni kumeibuka taarifa potofu kuwa ugonjwa huo huenezwa kwa njia ya hewa na kusababisha kuongezeka kwa vifo, hali inayosababisha watumishi wa afya kupatiwa chanjo kwa lazima.

“Serikali iliwataka wananchi kuzipuuza na badala yake kupata taarifa sahihi kutoka wizara ya afya au kwa wataalamu wa fani hiyo.

“Virusi vya kundi A na E huenezwa kwa njia ya kunywa au kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi, virusi hivi hushambulia ini na huweza kusababisha homa kali inayoambatana na dalili nyinginezo. Kirusi cha E kinaweza kusababisha mlipuko wa ugonjwa,” alisema Sungura katika taarifa yake

Alisema kuwa wagonjwa wanaopatwa na virusi hivyo hupona baada ya miezi miwili ama mitatu na kwamba njia ya kujikinga ni kuzingatia kanuni za afya, unywji maji safi na salama, ulaji chakula salama na usafi wa mazingira na matumizi bora ya choo. Aidha, virusi vya A na E si tishio kubwa sana kwa afya ya jamii.

“Virusi vya kundi la B, C na D huambukizwa kwa kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiana na mwenye maambukizi, kujidunga sindano wenye virusi vya ugonjwa huo na kupitia uambukizo kwa njia ya majamaji yenye uambukizi (kama damu, matapishi) kutoka kwa mgonjwa mwenye virusi hivi na kuingia kwa mtu mwingine iwapo mtu huyo ana kidonda/mchubuko wa ngozi.

“Moja ya njia kubwa kwa aina ya B pia ni pale mama anapoweza kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua. Hivyo kwa ufupi njia hizo hizo zinazoeneza virusi vya Ukimwi.

“Virusi vya kundi B na C vinapoingia kwenye mwili wa binadamu hushambulia ini ambapo baadhi hawaoneshi dalili, baadhi hupata athari kwenye ini na wengine hupata uambukizi sugu na wa muda mrefu,”alisema

Alisema baadhi ya uambukizo husababisha ini lisinyae na pengine huweza kusabisha saratani ya ini

Kuhusu uambukizo wa kirusi cha kundi D, Sungura alisema kuwa huwapata baadhi ya watu walioambukizwa kirusi cha kundi B ambao kitaalamu hufahamika kama ‘co infection’.

CHANJO

Akizungumzia kuhusu chanjo ya homa ya ini B hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya ili kutoa kinga ya muda mrefu na kwa kipindi chote cha maisha yake.

Alisema pia chanjo hutolewa kwa watoto na watu wazima walio katika makundi hatarishi ya kupata maambukizi.

“Serikali kwa kuzingatia miongozo ya wizara ya afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo dozi tatu kwa watoto walio na umri chini ya mwaka mmoja.

“Chanjo hiyo yenye mchanganyiko wa chanjo tano ilianza kutolewa kwa watoto wote waliozaliwa kuanzia mwaka 2002 na hadi sasa zaidi ya Watanzania milioni 20 wamepatiwa chanjo wakati wa utoto,” alisema

Sungura alisena pia Serikali hutoa chanjo kwa watu walio katika hatari zaidi ya maambukizi ambao ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya, watumiaji dawa za kulevya kwa kujidunga, wanaoishi karibu na ugonjwa wa homa ya ini, watu wenye wapenzi wengi na wengine ambao mara kwa mara wanakuwa karibu na damu kutokana na shughuli zao.

“Idadi ya dozi tatu hutolewa kwa mtu ili kupata kinga kamili ya ugonjwa huu. Katika vituo vya umma tumeanza kutoa chanjo kuzuia ugonjwa wa homa ya ini inayosababishwa na virusi vya kundi B.

“Tumepeleka chanjo hizi kwenye hospitali zetu za mikoa na vituo vyetu vya mipakani na katika hospitali zingine kama vile Ocean Road ambapo utaratibu wa kuchangia gharama unafanyika.

“Utaratibu unaotumika ni kupima kwa Sh 10,000 na kila dozi inagharinu Sh 10,000, hivyo dozi tatu ni Sh 30,000,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles