Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
ZIKIWA zimebaki wiki mbili kabla ya pambano la ngumi za kulipwa la lililopewa jina la Safari ya Beach, mabondia watakaopanda ulingoni siku hiyo wameendelea kupigana mkwara kila mmoja akitambia kambi yake.
Pambano hilo linalowakutanisha wakali wa wilaya zote za Dar es Salaam, litafanyika Oktoba 22, 2023 kwenye fukwe za Rongoni, Kigamboni.
Miongoni mwa mabondia hao ni mkongwe Jackson Malinyingi kutoka City Center Gym atakayezichapa Bahari Juma Kijo wa Mabibo, ametamba kuwa yeye ni daraja la kuvusha damu changa hivyo mpinzani wake ajiandae kwa kipigo kizito.
“Mimi niko fiti namuomba Mungu anaifikishe hiyo siku ya tarehe 22, nitamfunza sana na atajua kwamba utu uzima ni dawa na jungu kuu halikosi ukoko. Nimwambie kabisa Chui wa Mabwepande atakuja kunguruma pande za beach,” ametamba Malinyingi.
Naye bondia Bakari Mangosongo, amesema amejiandaa kuipa heshima wilaya yake ya Kigamboni dhidi ya Yake Ya Kigamboni Kwa Kumtwanga Felix Malume kwa kumaliza pambano mapema.
Mwingine ni Sebastian Deo wa Chamazi, amemtangazia vita kali Yohana Daud wa Tegeta Nyuki, huku akiungwa mkono na mashabiki wake ambao wameahidi kutoa sapoti kwa bondia wao kuhakikisha anamtwanga mpinzani kwa K.O.
Kwa upande Francis Nampumula wa Kijichi, amesema amesikia maneno ya mpinzani wake Sultani Kiyoko wa Mbagala Rangi Tatu na kumfanya azidi kupata hasira za kuongeza dozi ya mazoezi ili ampe kipigo cha ufundi.
Zaidi ya mabondia 30 wanarajiwa kupanda ulingoni siku hiyo, huku wanawake wakiwa ni Zawadi Kutaka dhidi ya Flora Machela.