Ramadhani Hassan – Dodoma
BUNGE limesema litaielekeza Serikali ije na taarifa rasmi kuhusu maafa yaliyotokea nchini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa (CCM).
Mbunge huyo katika hoja yake alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kuwasaidia wananchi wa Rufiji, ambao wamekumbwa na maafa na kusababisha wakose makazi ya kuishi na kubaki wakihangaika.
“Mheshimiwa Spika, Rufiji kumekuwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na mvua kuliko maeneo mengine yote nchini, mpaka sasa wananchi takribani 20,000 hadi 50,000 hawana makazi ya kuishi.
“Hawana chakula na wanahangaika sana kuokoa maisha yao, je kama Bunge tunachukua hatua gani ili kuwaangalia hata hawa wananchi wanyonge ambao wako kwenye maafa ya mafuriko,” alihoji Mchengerwa.
Spika Ndugai alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa mbunge huyo wa Rufiji na wa Kibiti kwa niaba ya Bunge akiwataka kufikisha pole hizo kwa wananchi.
Alisema mafuriko ya aina hiyo yaliyotokea katika eneo hilo hayajapata kutokea na ni makubwa sana na kwamba anaamini Serikali imesikia ujumbe wa mbunge huyo.
“Tunapokea ushauri wake mheshimiwa mbunge, Mheshimiwa Jenister (Mhagama) ambaye ndiye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, masuala ya maafa yako chini yake, wakati utakapofika atatupa taarifa kama Bunge,” alisema Ndugai.
Mafuriko hayo yanaelezwa kukata mawasiliano ya ndani ya Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani na kuziacha zaidi ya kaya 350 bila makazi.
Mafuriko hayo yameharibu barabara mbalimbali za wilaya hiyo, ikiwamo inayotoka Kibiti kwenda katika eneo la mradi wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji ambako magari yenye vifaa yalikwama ndani ya maji.
Pia, baadhi ya barabara zinazounganisha kata 13 za Rufiji hazipitiki kutokana na makaravati kusombwa na maji na Daraja la Ikwiriri limeonyesha dalili za kubomoka, hali inayotishia kukatika kwa mawasiliano na mikoa ya kusini.