25.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

Hoja ya Katiba mpya bado ni hai

image29
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete

 

Na BALINAGWE MWAMBUNGU,

RAIS Jakaya Kikwete alipotangaza kwamba Tanzania itapata Katiba Mpya kabla hajaondoka madarakani mwishoni mwa 2015, tulidhani alikuwa na nia njema kwamba alitaka kujiwekea uhalali wa kudumu kwamba historia ingemuenzi kuwa alikuwa na visheni ya namna ya kuendesha utawala bora wenye kufuata misingi ya kidemokrasia.

Kikwete angekumbukwa kwamba ndiye aliyefanya mageuzi ya kuitoa nchi katika utawala msonge wa chama kimoja na kuweka mizizi ya utawala wa watu kwa niaba ya watu na kwa ajili ya watu.

Haya yote yangepatikana tu kama Katiba Mpya yenye maridhiano ya wananchi ingepatikana. Maana Katiba ndiyo inayoweka msingi wa kuendesha mambo yote ya nchi.  Kikwete akakatishwa tamaa na vigogo wenzake ndani ya chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao waliiona Katiba Mpya kama fagio la chuma ambalo lingewaondoa kwenye mtandao ‘haramu wa ufisadi’ na ubadhirifu wa rasilimali za nchi.

Ndio maana Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa pamoja walimchagua Samuel John Sitta kuwa Spika wa Bunge hilo, wakiamini kwa dhati kwamba alikuwa na nia na uwezo na kwamba angeliendesha Bunge kwa utulivu hadi mwisho. Sitta naye angeingia kwenye kumbukumbu za historia ya Taifa kama kiongozi aliyeitumikia nchi vyema na angekumbukwa kwa utumishi uliotukuka.

Kupatikana kwa Katiba yenye maridhiano ya wananchi kungekuwa heshima kubwa kwake. Lakini naye kama Rais Kikwete, akaingiwa na woga kwa kuwa alikuwa ana mambo yake binafsi ya kutaka kugombea urais na hapana shaka alipenda Katiba ya sasa ambayo inampa madaraka makubwa Rais na si Katiba ambayo ilikuwa na mapendekezo ya kupunguza madaraka ya Rais.

Wahafidhina ndani ya CCM, walitumia nguvu ya wingi wao na kuwatisha wajumbe waliokuwa wanataka mabadiliko. Karibu viongozi wote 42 walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya rais kupitia CCM, walikuwa Wajumbe la Bunge Maalumu la Katiba. Hawakupaza sauti ili ipatikane Katiba nzuri kutokana na ubinafsi wao kujifikiria wao endapo watabahatika kupenya kwenye kinyang’anyiro cha urais wangependa Katiba ya sasa itumike.

Spika Sitta hakutenda haki kwa wajumbe wa upinzani ambao kwa maoni yao, waliona kama analiendesha Bunge la Katiba kwa maelekezo ya chama tawala. Wakasusia vikao vya Bunge huku wakishinikiza kwamba wanataka Katiba mpya, kwa sehemu kubwa, ibebe maudhui ya Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba ambayo iliainisha matakwa ya wananchi na kuweka utaratibu wa namna wanavyotaka watawaliwe.

Lakini Sitta, tofauti na matarajio ya Watanzania, akalivuruga Bunge Maalumu la Katiba na kujigeuza Tume, akawa anakusanya maoni kutoka vikundi maalumu kazi ambayo tayari ilikwisha fanywa na Tume ya Warioba. Wakati wa kulihitimisha Bunge hilo, ili akidi ikidhi matakwa ya Kanuni ambayo ilitaja idadi ya wabunge kutoka Tanzania Bara na Zanzibar itimie.

Akafanya ‘udanganyifu’ na kuwaorodhesha wabunge ambao walikuwa wamekwenda Hijja na kuonesha kwamba walipiga kura. Mbunge mmoja, Zakia Megji, ambaye maisha yake yote ameishi Bara, akaorodheshwa kuwa anatoka Zanzibar!

Pamoja na kuandaa sherehe kubwa yenye mbwembwe nyingi pale Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kukabidhi mapendekezo ya Bunge Maalumu la Katiba kwa Rais Kikwete, mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi hadi sasa.

Bunge Maalumu la Katiba, badala ya kuwaunganisha wajumbe, likavurugika na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umoja ambao sasa umekuwa mwiba kwa Serikali ya sasa na zoezi la kuipigia kura Katiba pendekezwa halijafanyika na huenda lisifanyike kwa sababu si suala la kipaumbele kwa sasa.

Rais John Magufuli ametamka wazi kwamba Serikali yake itashughulika na mambo yanayowagusa wananchi moja kwa moja ndio maana katika mikutano yake yote ya hadhara ambayo amekwishafanya hadi sasa, hajatamka kwamba ataendesha na  kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya, zoezi la kupiga kura ya maoni.

Lakini masuala haya yanazikumba nchi nyingi za Kiafrika ambazo viongozi wake hawafuati misingi ya kidemokrasia. Nchi ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na kujiita ya kidemokrasia, haijawahi kufanya uchaguzi wa kidemokrasia tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Wabelgiji mwaka 1960.

Kutokana na nchi kutokuwa na miundombinu mizuri, ni vigumu hata kuendesha chaguzi, halafu zikawa za kidemokrasia. Nchi ni kubwa sana, ina eneo la kilomita mraba 2,345,408 sawa na maili mraba 905,567.

DRC imegawanywa katika majimbo 26 ambayo yanaongozwa na magavana na kila jimbo linajiendesha lenyewe. Ni kazi ngumu sana kuendesha chaguzi kutoka Mji Mkuu Kinshasa. Sehemu kubwa ya DRC ni misitu na ardhi oevu, hata viwanja vyake vya ndege si vizuri sana.

Zipo pia nchi za Kiafrika ambazo zinazingatia katiba zao na zinaendesha chaguzi vizuri; Afrika Kusini, Namibia, Ghana, Senegal na jambo la kustaajabisha kabisa Nigeria pia inapigiwa debe kwamba Uchaguzi Mkuu uliomwingiza madarakani rais wa sasa, Mohammed Buhari, ulikuwa huru na wa haki.

Nchi nyingine kama Tanzania, Uganda, Zimbabwe na Angola, zinatajwa kwamba zinaendesha chaguzi ili kuhalalisha vyama tawala viendelee kushika madaraka ndio maana viongozi wao hawapendi mabadiliko. Tanzania kwa mfano, inaendeshwa kwa Katiba iliyotungwa mwaka 1977 wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho kidogo, ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini haikubadili mfumo wa utawala umebaki vile vile. Chama tawala kinabebwa na vyombo vya usalama na Jeshi la Polisi. Katiba ya sasa inampa mtu mmoja madaraka makubwa sana na Mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema angetaka kuwa dikteta, angeweza kwa kuwa Katiba inampa Rais madaraka makubwa sana.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema katiba kama hizo ndio chanzo cha utawala mbaya, kukosekana kwa uwazi (transparence) kunachangia na kuendeleza rushwa ambayo ni adui mkubwa wa maendeleo.

Kama alivyosema Rais wa Marekani, Barack Obama, Afrika haihitaji watawala wababe ili iweze kuendelea, bali inahitaji taasisi imara zenye uwezo wa kusimamia mambo ya nchi. Afrika inahitaji viongozi ambao uongozi wao hautegemei matumizi ya vyombo vya dola au majeshi.

Rais Robert Mugabe, amekuwa akitegemea zaidi jeshi ili aendelee kuwapo madarakani kwa kuwa jeshi limetokana na jeshi la wapigania uhuru, Zimbabwe National Liberation Army na yeye akiwa kiongozi wake wa kisiasa.

Aidha, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, nguvu ya chama chake cha NRM (National Resistance Movement) kimetokana na jeshi lake la msituni, National Resistance Army (NRA), jeshi ambalo baadaye aliligeuza kuwa vuguvugu la kisiasa, hawa hawawezi kuachia nchi kirahisi.

Tanzania haijawahi kutawaliwa kijeshi kwa vile ilitokana na mfumo wa Utawala wa Kibunge (Parliamentary System), mfumo ambao kiongozi wake anakuwa Waziri Mkuu wa Serikali inayowajibika bungeni.

Nchi zote za Kiafrika ambazo zilitawaliwa na Waingereza, zikachagua mfumo wa Kijamhuri (Republican System). Mfumo ambao unatakiwa uangaliwe upya kila baada ya miaka fulani kupita. Hii ni kwa sababu mfumo huu unatoa uhuru mkubwa sana kwa rais kufanya anavyotaka na haulizwi na chombo chochote, kwa sababu yeye ni kila kitu ndiye mamlaka teuzi.

Kwa hiyo Rais Kikwete alipotangaza kwamba Tanzania itapata Katiba Mpya kabla hajaondoka madarakani, tulimwona katika muktadha huo kwamba kwa kuwa Tanzania ilikuwa haijawahi kuwa na Katiba iliyoshirikisha wananchi wake kutoa maoni yao jinsi wanavyopenda watawaliwe, ule ulikuwa muda mwafaka.

Lakini Kikwete, kwa kuwaogopa mahafidhina ndani ya chama chake, akawa mzito kuamua. Lakini hoja ya Katiba Mpya bado ni hoja hai na inawezekana imeahirishwa kwa muda tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles