27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja 11 kupinga hukumu iliyokataza wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Kulwa Mzee -Dae es salaam

MAHAKAMA ya Rufani imesikiliza rufaa iliyokatwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake wawili, wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotengua wakurugenzi wa halmashauri za miji, wilaya na manispaa kusimamia uchaguzi kwa madai kwamba ilikosea.

Rufaa hiyo ilisikilizwa jana, huku upande wa warufani wakiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Clement Mashaba, aliyeongoza jopo la mawakili 10 wa Serikali wakipinga uamuzi huo wakiwa na jumla ya hoja 11.

Serikali inapinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha kifungu namba 7 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachowapa mamlaka wakurugenzi hao kuwa wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanaharakati Bob Chacha Wangwe, akipinga wakurugenzi hao kuwa wasimamizi wa uchaguzi, ilitolewa Mei 10, mwaka huu na jopo la majaji watatu; Dk. Atuganile Ngwala (kiongozi wa jopo), Dk. Benhajj Masoud na Firmni Matogolo.

Wakiwasilisha hoja hizo mbele ya jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa na  Jaji Agustine Mwarija, mawakili hao wa Serikali walidai pamoja na hoja nyingine, Mahakama Kuu ilikosea kutamka kwamba vifungu hivyo vinakinzana na katiba kwa kuzingatia ibara ya 74 (14), kwa kuwa haihusiani na nafuu ambazo mdai alikuwa akiziomba.

“Mahakama Kuu ilikosea kwa kushindwa kutathmini makatazo chini ya ibara ya 74(14) ya katiba na ulinzi unaotolewa na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kanuni zake, Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake na sheria nyinginezo zinazohusiana na uendeshaji wa uchaguzi.

“Mahakama ilikosea kwa kushindwa kutambua matokeo (legal effect) ya kiapo cha siri na tamko la kujiondoa katika uanachama wa chama cha siasa au kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa, vinavyoapwa na wasimamizi wa uchaguzi kabla ya kuingia katika ofisi hizo kuchukua majukumu yao.

“Sisi tunaamini sheria ya uchaguzi imezuia mianya ya upendeleo na yapo maeneo mengi ambayo wasimamizi hao husimamiwa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi na pili husimamiwa na NEC,” alidai Mashaba.

Warufani katika kesi hiyo namba namba 17 ya mwaka 2018, walikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), NEC na Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Katika hukumu yake, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za Wangwe kupitia kwa wakili wake, Fatma Karume, ikisema kuwa kifungu hicho ni kinyume cha katiba ya nchi, kwani kinakinzana na matakwa ya katiba inayotaka Tume ya Uchaguzi iwe huru.

Pia mahakama hiyo ilibatilisha kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya Uchaguzi, kinachoipa NEC mamlaka ya kumteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma, kuwa msimamizi wa uchaguzi kwa niaba yake.

Wakili Karume pamoja na hoja za kupinga rufani hiyo, anadai sheria ya uchaguzi haisemi ni kwa jinsi gani hao wakurugenzi wanakuwa wamejitoa katika chama pindi wanapoapa au kula kiapo wakati wa kusimamia uchaguzi.

Uamuzi wa kesi hiyo utatolewa baadae kwa tarehe itakayotangazwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles