25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu yatanda virusi vipya vikizidi kusambaa kwa kasi nchini China

Wuhan, China

IDADI ya watu walioathirika na virusi vipya nchini imeongezeka mata tatu zaidi, huku ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo  ukielezwa kuenea katika majiji mengine makubwa.

Jiji la Wuhan ulikoanzia ugonjwa huo limeripotiwa kuwa na kesi mpya 136 za  ugonjwa huo ambao husababisha mgonjwa kushindwa kupumua vizuri.

Tayari Jiji la Beijing zimekwisharipotiwa kesi mbili, wakati Shenzhen ikithibitisha moja.

Idadi ya watu walioathirika na ugonjwa huo inaelezwa kuzidi 200, na watatu tayari wamekwishafariki dunia.

Taarifa hizi za kushtua zimekuja wakati mamilioni ya Wachina wakijiandaa kusafiri kwa ajili ya mapumziko wa mwaka mpya wa China ‘The Lunar New Year’.

Kutokana na hilo mamalaka  za nchini humo zimesema zitachunguza kila mtu anayesafiri.

Tayari maofisa wa afya wameubaini ugonjwa huo ambao ulianzia Wuhan mwezi Desemba mwaka 2019 kuwa ni aina ya

virusi vya ‘corona’ lakini mengi kuhusu ugonjwa huo bado hayajajulikana.

‘Corona virus’  ni ugonjwa ambao huathiri  mfumo mzima wa pua, macho, koo na karibu na paji la uso na hivyo kumfanya mgonjwa apate homa kali na zaidi kushindwa kupumua.

Pamoja na kwamba ugonjwa huo unasadikika kuanzia katika soko la vyakula vya baharini, Serikali na wataalamu wa afya bado hawajabaini ni kwa namna gani ulisambaa.

Taarifa hizi mpya zimekuja ikiwa ni mwishoni mwa wiki iliyopita wanasayansi wa Uingereza walilidokeza Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kwamba ugonjwa huo mpya ulioibuka nchini China umeathiri mamia tofauti na idadi inayotolewa na maofisa wa serikali nchini humo.

Wataalamu hao wa Uingereza wanasema wanakadiria kuwa idadi ya walioathirika inaweza kukaribia 1,700.

Mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko, Profesa Neil Ferguson, amesema ana wasiwasi idadi ikawa ni kubwa zaidi.

Singapore na Hong Kong  wamekuwa wakiwachunguza abiria wanaotoka Wuhan na Marekani pia imetangaza kuchukua hatua kama hizo katika viwanja vya San Francisco, Los Angeles na New York.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati mlipuko wa ugonjwa huo ukitajwa kuanzia Wuhan, kesi mbili zinazohusu ugonjwa huo zimeripotiwa katika nchi za Thailand  na moja nchini Japan

“Hii inasababisha wasiwasi,” alisema Prof. Ferguson.

Aliongeza kuwa: “Wuhan kupeleka kesi tatu katika nchi nyingine inamaanisha kwamba huenda kuna kesi zaidi ambazo hazijaripotiwa.”

Alisema japo inaweza kuwa ni vigumu kupata idadi kamili lakini kutokana na ugonjwa huo kuenea kwa virusi na mazingira ya nchi yenyewe yenye idadi kubwa ya wananchi na idadi ya wasafiri wa ndege hilo linaweza kutoa taswira nini kinaendelea.

Pamoja na hayo Prof. Ferguson alisema ni mapema mno kutangaza hali ya hatari.

Mamlaka za nchini China zimesema hakuna kesi yeyote ya virusi hivyo kusambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Badala yake wamesema kuwa virusi hivyo vimetoka kwa wanyama walioathirika kutoka katika soko la vyakula vya baharini na wanyama la Wuhan.

Taarifa hizi mpya zimekuja ikiwa ni takribani wiki mbili zimepita tangu mamlaka ya China ianzishe utafiti kuchunguza virusi vinavyosababisha ugonjwa huo wa ajabu ambao umewaambukiza watu kadhaa katika mji wa Wuhan.

Ugonjwa huo ulizua hofu mtandaoni na kuhusisha virusi hivyo kuwa unaweza kusababisha kuwa na mtindio wa ubongo na madhara mengine yanayoweza sababisha vifo.

Awali ilidaiwa kuwa kuna uwezekano wa ugonjwa huo kufanana na ugonjwa wa ‘sars’ ambao uliua watu zaidi ya 700 ulimwenguni kote mwaka 2002-03, baada ya kutokea nchini China.

Shirika la Afya duniani la WHO lilisema linaangalia kwa karibu mlipuko huo na itaweza kutoa taarifa zaidi watakapozipata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles