32.3 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Hisa za UDA-RT kuanza kuuzwa Machi

SIMONMAULI MUYENJWA NA JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, amesema UDA-RT imewekeza zaidi ya Sh bilioni 90 na kuanzia Machi mwaka huu kuna mpango wa kuanza kuuza hisa kwenye Soko la Hisa.

Pamoja na hali hiyo kampuni hiyo imeweka wazi wamiliki halali wa UDA wanaotambulika kwa mujibu wa sheria.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari   katika Ukumbi wa Karimjee   Dar es Salaam jana kuhusu tuhuma kwamba Kampuni ya Simon Group ilipata upendeleo kununua Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), pamoja na kutoa ufafanuzi wa wanahisa halali kwa mujibu wa sheria.

Alisema   hivi sasa kampuni hiyo imejikita katika kuhakikisha  Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, unaanza kwa wakati sambamba na uuzaji wa hisa.

Kisena alisema kuna mpango wa kuuza asilimia 70 ya hisa zake kwenye soko la hisa.

“ Tunatarajia kupata Sh bilioni 600 ambazo zitatumika kujenga maegesho ya magari ambayo yatakuwa na huduma nyingine kama maduka na kadhalika,” alisema Kisena.

Alisema  wamiliki wa mabasi   138 ya dalaala wameshalipwa fidia ya   Sh bilioni mbili ambako kila basi   limelipiwa  Sh milioni nne na katika fedha hizo   Sh milioni moja zitabaki kama hisa.

Akizungumzia suala la umiliki wahisa wa familia ya Rais Kikwete katika UDA, alisema ni vema washindani wake wa  biashara wamwache Rais mstaafu Jakaya Kikwete  apumzike kwa kuwa hahusiki katika biashara zake.

Kisena alisema kuna watu wanataka kumchafua yeye katika biashara huku akiwataka wasimhusishe Rais Kikwete,   badala yake wamshambulie yeye bila kuhusisha wala kuumiza watu wengine  ambao hawana uhusiano na biashara zake.

“Kama kuna watu wana ugomvi wa siasa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, washambuliane wao kwa wao huko huko, wasitumie kampuni yangu kama jukwaa la mashambulio hayo.

“Mimi niliacha siasa tangu mwaka 2010… nilipongombea nikashindwa nimebaki kuwa mwanachama hai na mwaminifu kwa CCM,” alisema na kuongeza:

“Kampuni hii tumeipa jina la marehemu baba yangu, Mzee Simo.

Tangu imeanzishwa imekuwa kampuni ya familia, wamiliki wake ni mimi, mdogo wangu William Simon, mpwa wangu Kulwa Simon, ndugu yangu Ngalula Saguda, mke wangu na watoto wangu, imekuwa hivyo tangu ianzishwe na haijabadilishwa”.

Akizungumzia   ununuzi wa hisa katika za UDA, alisema  alinunua hisa zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuuzwa (allotted shares) kwa Sh bilioni saba mwaka 2011.

Alisema  baadaye mwaka 2013 alinunua hisa za Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam ambazo zilikuwa ni   asilimia 24 ya hisa zote za UDA, kwa Sh bilioni 5.8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles