WASHINGTON, MAREKANI
UONGOZI wa aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hilary Clinton dhidi ya Donald Trump wa Republican katika kura za kawaida, umeongezeka kufikia milioni mbili.
Rais mteule Trump alishinda uchaguzi huo wa urais uliofanyika Novemba 8 kwa wingi wa kura za wajumbe na anatarajia kuapishwa Januari 20.
Lakini kura za kawaida zinaendelea kuhesabiwa, ikiwa ni wiki mbili tangu ufanyike Hillary akiwa na kura milioni 64.2 na Trump milioni 62.2.
Hii ni mara ya tano kwa mgombea urais kuongoza kwa kura za kawaida, lakini akashindwa uchaguzi kwa kura za wajumbe, ambazo ndizo zinazoamua mshindi.
Mwaka 2000, mgombea wa Democratic, Al Gore, aliongoza dhidi ya George W Bush kwa karibu kura 544,000.
Lakini baada ya mvutano wa muda mrefu mahakamani, Mahakama ya Juu iliamua mshindi wa urais baada ya kumkabidhi Bush ushindi katika Jimbo la Florida.
Mwaka huu, Hillary alipata kura nyingi katika majimbo kama vile California, lakini Trump alishinda majimbo muhimu yaliyompa kura nyingi za wajumbe wa Baraza la Uamuzi.
Kundi la wasomi, mawakili na wataalamu wa data, wanajaribu kumshawishi Hillary na watu wake wajiunge na juhudi za kuchunguza matokeo katika majimbo matatu, kubaini iwapo kulikuwa na uingiliaji wa mitambo ya kompyuta.
Kundi hilo linashangaa ni kwa nini Hillary alionekana kutofanya vyema katika wilaya zilizotumia kompyuta kupiga na kuhesabu kura, ikilinganishwa na maeneo ambayo watu walipiga kura halisi za karatasi na mitambo ya skana ya kuhesabu kura.
Lakini maofisa wa kampeni wa Hillary hawajaonyesha nia yoyote ya kutaka kura zihesabiwe tena.
Mgombea wa chama cha Green Party, Jill Stein, anachangisha fedha za kupigania kura zihesabiwe upya katika majimbo hayo ya Michigan, Wisconsin na Pennsylvania ambayo Trump alishinda.
Wakati hayo yakijiri, Trump kwenye hotuba yake siku ya kutoa shukrani, aliwahimiza raia wa Marekani kuunga mkono juhudi zake za ‘kujenga upya nchi’ na kuponya makovu baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.