25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

HILI LA KUPIMA ARDHI SERIKALI IACHE MANENO, ICHUKUE HATUA

JUZI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake bungeni na miongoni mwa mambo makubwa aliyoyagusia ni kusudio la serikali kuhakikisha kila ardhi inapimwa na kutumika kwa usawa na haki.

Si hilo tu, serikali pia imeeleza mipango yake kuhusu utoaji wa miliki za ardhi, kuhakiki viwanja na mashamba, lakini pia sheria za kimila kuhusu umiliki wa ardhi, hasa zile zinazokandamiza wanawake.

Ni ukweli usiopingika kwamba ukiondoa kero kama maji, inayofuata kwa kulalamikiwa na wananchi wengi ni migogoro ya ardhi.

Zipo sababu kadha wa kadha za kuwapo kwa migogoro hii, kubwa inachangiwa na kasi ndogo ya serikali katika kupima viwanja ili viweze kutumika si tu kwa usawa na haki, bali kwa mipango bora ya ardhi.

Leo hii ukifuatilia migogoro mingi ya ardhi utagundua ni ile inayotokana na ama watu kutapeliana au mtu mmoja kujimilikisha ardhi kubwa.

Kwa mantiki hiyo, ile dhana au ndoto ya serikali kutaka watu wamiliki ardhi kwa usawa, haki na kwa mipango bora ni kama haipo, na kila siku ni kama tunaanza mwanzo kwa sababu tu ya kasi ndogo ya serikali katika kuhakikisha ardhi yote iliyopo nchini inapimwa.

Ni ukweli mchungu kwamba, katika kila bajeti serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imekuwa ikilisema jambo hilo, huku kasi ya kulitekeleza ikionekana kuwa ni ndogo na haifanani na kile ambacho Bunge linaelezwa katika mipango ya wizara.

Kama si sasa, katika mipango yake ya baadaye ni vyema serikali ikafikia hatua ya kufanya maamuzi magumu kwa kutenga fedha za kutosha katika suala hili la kupima ardhi, kama ilivyofanya katika ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli ya kisasa.

Kwa sababu ya kuchelewa kuchukua maamuzi magumu ya kupima, tumefanya matumizi yetu ya ardhi kutokuwa bora, leo hii kila kona ya nchi tunashuhudia migogoro isiyokwisha.

Matokeo yake, baadhi ya viongozi wametumia udhaifu huo kujimilikisha ardhi kubwa, huku baadhi ya wananchi wa kawaida wakiwa hawana hata mita moja ya ardhi.

Hatua hiyo pia imesababisha migogoro ya kutapeliana kati ya jirani na jirani, mwekezaji na wananchi, mwekezaji na serikali na migogoro mingine chungu nzima yenye sura hiyo.

Kwa sababu kama hizo, tunadhani ni vyema sasa serikali ikachukua hatua kwa vitendo kwa kupima ardhi na tunadhani si tu utakuwa mwanzo wa kupunguza migogoro, bali pia ardhi yetu kuwa na thamani na kufanya matumizi bora na yenye tija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles