27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Hii ndiyo athari ya mitandao ya kijamii

KAHINDE KAMUGISHA

MITANDAO ya kijamii imekuwa ikitajwa kama moja ya mifumo inayoharibu maadili kwa vijana.

Kutokana na hali hiyo, sasa ipo haja kwa wazazi na walezi kushirikiana pamoja na Serikali ili kulinda maadili mema ya jamii ikiwamo kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi elimu ya juu.

Changamoto kubwa inayotajwa kwenye mitandao ya jamii ni kusababisha watoto kupoteza maadili na kuwa sehemu ya vishawishi kwa watoto wa kike kupata ujauzito huku wale wa kiume wakitajwa kuangukia kwenye kundi baya likiwamo la uhalifu.

Wakizungumzia hali hiyo kwa nyakati tofauti akiwamo Mdhibiti Ubora wa Elimu Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Cecilia Mduma, ambaye aliweka wazi hayo kwenye semina ya elimu ya ushauri nasaha na unasihi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari walioko halmashauri za Misenyi, Kyerwa na  Ngara.

Mduma anasema wanafunzi wamekosa malezi katika familia na kupata nafasi ya kujitawala katika mazingira ya kutafuta elimu hatimaye kuporomoka kimaadili kwa kutazama picha na sinema za matukio yanayowazidi uwezo wao kiakili na kushawishika kufanya majaribio.

“Majaribio ya kufanya ngono katika umri mdogo wanapata mimba za utotoni na kupoteza ndoto za maisha yao, wavulana wanakimbia masomo wakiogopa kukamatwa na vyombo vya dola lakini baadhi yao wanapata magonjwa ya ngono zembe ukiwemo Ukimwi,” anasema Mduma.

Pia anasema watoto wengine wanakosa malezi katika familia kutokana na migogoro ya wazazi na kujikuta wakikumbana na msongo wa mawazo wakiathirika kisaikolojia hali ambayo imesababisha baadhi kujinyonga wakikaribia mitihani wakifikiria changamoto zinazowakabili.

Baadhi ya wazazi na vijana waliotoa maoni yao kuhusiana na changamoto zinazowakabili wameeleza kuwa ukosefu wa mabweni au hosteli unasababisha wajitawale na wengine hushawishika kutokana na umasikini uliopo kwenye familia wanapokosa mahitaji kutoka kwa wazazi wao.

Vijana wanaoishi katika Mji wa Rulenge wilayani Ngara, Meshack Athumani na Editha Simon, wanasema walimu na mamlaka za nidhamu katika utoaji taaluma pia ni vema wasimamie sheria za shule au vyuo kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao kulinda maadili ya kiroho na kimwili.

Hata hivyo, Mzee Pius Ngeze na  Evangelina Kalugendo, ambao ni wazazi walisema shughuli za kimaisha zimetawala na kukosekana nafasi ya kukaa na watoto wao kuwapatia maadili, mila na tamaduni za Kiafrika baada  ya  watoto wengi kusomea mbali na wazazi au walezi.

Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Katoke mkoani Kagera, Ezekiel Mugishagwe, anawataka walimu na wazazi au walezi kuepuka utumiaji wa adhabu kupita kiasi na kusababisha wanafunzi kukata tamaa za kuhudhuria masomo au kukimbia familia na wengine wakipata ajira zisizo rasmi.

Anasema suluhu la kuwaondolea watoto msongo wa mawazo na kuhudhuria masomo kisha kufaulu vizuri ni kuepuka kutoa adhabu za viboko au nyinginezo zinazoweza kuwaumiza mwili au kuwaathiri kiakili, lakini kuonesha upendo na huruma kwa kufanyia tafiti changamoto zao.

“Adhabu za kukurupuka zilisababisha kifo cha mwanafunzi Shule ya Msingi Mafumbo Manispaa ya Bukoba,  wazazi walipoteza mtoto, Serikali kupoteza nguvu kazi ya taifa, lakini wahusika wanazidi kuhoji na kutofanya kazi pia gharama zisizokusudiwa,” anasema Mugishagwe.

Madhara mengine alisema vijana wanaathirika kisaikolojia kutokana na adhabu zinazotolewa na walimu bila kufanya utafiti  wa kosa linalojitokeza,  kusababisha madhara kwa mtoto kimwili na kiakili, lakini mzazi naye kujenga mahusiano mabaya na walimu huku wenye kutoa adhabu kushikiliwa na vyombo vya dola  hatimaye kupoteza kazi zao.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,451FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles