26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hii ndio gharama ya mpenzi wa kweli

RAFIKI yangu mmoja aliniuliza swali, kwanini mahusiano mengi ya siku hizi hayadumu? Nikamjibu kifupi sana, kwamba watu wengi hawataki kulipa gharama halisi ya kumpata mpenzi sahihi.

 Hakunielewa. Akaniuliza tena kwamba hata wenye kipato cha juu pia na wao hawadumu katika mahusiano yao. Ikabidi nimpe ufafanuzi juu ya gharama niliyoikusudia.

 Gharama ambayo wengi wanashindwa kuilipa ili kupata mpenzi sahihi siyo ya fedha au mali. Ila ni gharama ya mchakato kamili wa kumpata mpenzi sahihi.

Vijana wengi wa kiume siku hizi akipata kazi na kujiona anaweza kumudu gharama za maisha , anadhani anafaa kuwa na mke ama mpenzi. Kwa akili ya namna hii ndipo unakuta kijana yuko bize kusaka mpenzi atakayemkubali na kumvutia bila kuangalia mambo mengine ya msingi.

 Vijana wengi siku hizi wako bize kuangalia sura, maumbile na vipato bila kuangalia ubora wa tabia za wahusika. Msisimko halisi wa ndani ya ndoa unachangiwa zaidi na tabia kuliko sura na umbile. Hivyo mtu anayekimbilia sura na umbile na kuacha kuangalia tabia ni dhahiri hajui mahitaji halisi ya ndoa.

Sisemi mtu aoe ama aolewe na mtu asiyemvutia. Sisemi hivyo hata kidogo. Kila mmoja anatakiwa kuwa na mtu anayemvutia ila tamaa juu ya sura ama umbile la mtu lisikufanye ukasahau thamani na ubora wa tabia ya muhusika. Tabia ndiyo injini ya ndoa. Tabia ndiyo inafanya ndoa itoe tafsiri nzuri ama mbaya na wala siyo sura ama umbile lake.

 Mwanamke ana fahari gani kuwa na mwanaume mrefu, mwenye ‘six packs’ na mwenye kipato cha juu kama mwanaume huyo anamdharau, anampiga na haoni umuhimu wa kumuheshimu? Mwanaume ana fahari gani kuwa na mwanamke mwenye umbile namba nane na mwenye kubabaisha wengi ila ni malaya na hamuheshimu mumewe?

 Ili ndoa ilete thamani na ubora kila mamaoja anatakiwa kuwa tayari kulipa gharama na thamani yake. Kama umemwona mwanamke au binti na akakuvutia acha papara ya kumchombeza na kutaka kuingia naye katika mahusiano. Kuwa rafiki yake kwanza, kuwa makini mno na tabia na mienendo yake.

Chunguza aina ya marafiki zake, familia yake na kama ukiweza fahamu kwa uhalisia kama aliwahi kuwa katika mahusiano, chunguza mahusiano hayo yalivunjika kwanini? Nani alikuwa sababu? Nani alikuwa akiyapa mahusiano hayo hadhi na heshima?

 Mahusiano mengi yanavunjika kwa sababu wahusika wanaingia katika mahusiano kwa mizuka na bila kujuana vizuri. Kwa kuwa kina fulani ni mtanashari na anasifiwa na wengi, unakuta binti akitongozwa na kijana huyo hata hajiulizi mara mbili, haraka tu anaingia katika mahusiano. Baada ya miezi kadhaa anaanza kulalamika kwamba wanaume wabaya kwa sababu ameteswa na kuumizwa sana kihisia.

Swali la kujiuliza, wakati unakuwa ana muhusika ulijipa muda na tafakuri ya kina juu ya tabia na mienendo yake?

 Heshimu hisia zako na yathamini maisha yako. Acha kuwa mtu wa hovyo unayeweza kutongozwa katika mitandao ya kijamii na haraka ukakubali na kujiona unafanya jambo sahihi. Mahusiano bora ni yale ambayo wahusika wanajuana na kuamua kuwa pamoja kutokana na nguvu ya hisia zao za upenado na siyo nguvu ya tamaa ya kutaka kuonekana unatoka na fulani.

 Kubali kulipa gharama za mahusiano ili upate mahusiano bora naya uhakika. Acha kubabaika na mtu. Acha kudhani kwamba kumkubalia haraka ndiyo njia ya kuiwahi bahati yako. Haraka haraka isiyo na mipango siyo njia ya kuiwahi bahati bali ni njia ya uhakika ya kukimbilia mikosi na majuto makuu katika maisha yako.

Instagram: g.masenga

Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia ( Psychoanalyst)

  [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles