30.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Hii hapa ndoa iliyodumu miaka 82

HASSAN DAUDI

BILA shaka umewahi kukutana na swali juu ya chanzo cha ndoa nyingi za siku hizi kuvunjika miezi au miaka michache tu baada ya sherehe kubwa iliyogharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Huenda kuna sababu nyingi, lakini wanandoa hawa walioishi pamoja miaka 82 wanaweza kuwa na jibu sahihi katika hilo.

Inaweza kukushangaza kidogo, lakini ukweli ni kwamba wanandoa hawa wameweza kuishi pamoja kwa miaka 82 sasa tangu walipoidhinishwa kuwa mke na mume.

Raia hao wa Japan, ambao pia wote wanatokea jijini Oita, ndiyo wanaoshikilia rekodi ya dunia, wakiwa na ndoa iliyodumu muda mrefu zaidi duniani. 

Ifahamike kuwa Japan ni moja kati ya nchi ambazo wananchi wake wana wastani mkubwa wa umri wa kuishi, ikitajwa kuwa ni miaka 84.

Masao Matsumoto (109), alimuoa Miyako Sonoda (101) mwishoni mwa mwaka 1937 na wamebahatika kupata watoto watano, wote wa kike, tena wakiwa na wastani wa umri wa miaka 66 hadi 77.

“Wameingia ukurasa wa mwisho wa maisha yao. Ni jambo la heshima kwao kupewa tuzo. Ningependa kuona wakiendelea kuishi maisha ya amani,” anasema binti yao, Hiromi.

Pia, wahenga hao wamefanikiwa kupata wajukuu 13, huku idadi ya vitukuu ikitajwa kufikia 25.

Hata hivyo, Masao na Miyoba, wanakiri kuwa haikuwa rahisi kwa ndoa yao kudumu muda mrefu kiasi hicho kwani kama si uvumilivu, basi ingefungwa au ingekuwa imeshavunjika muda mrefu.

Moja kati ya majaribu yaliyohitaji uvumilivu wa kiwango cha juu ni kitendo cha Masao kutakiwa kujiunga na jeshi mara kwa mara kabla ya kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia, ambapo alilazimika kumwacha Miyako. 

Ifahamike kuwa wakati huo walikuwa hawajafunga pingu za maisha hivyo kama si uvumilivu huenda ndoa yenyewe isingekuwapo. 

“Wazazi wa Miyako walikuwa wakija kwetu mara kwa mara kuuliza lakini waliambiwa sijarudi,” anakumbuka Masao.

Kutokana na hilo, ndoa yao ililazimika kupigwa kalenda mara kadhaa kutokana na Masao kupelekwa katika operesheni mbalimbali za kijeshi.

Anaongeza kuwa hata ilipofanikiwa kufungwa mwishoni mwa mwaka 1937, ndoa yao haikuwa na sherehe kwani haikuchukua muda mrefu kabla ya mumewe huyo kurejea kambini.

Miyako anasema: “Kuna kipindi nilikuwa nahisi  hatarudi lakini mwaka 1946 akawa anapatikana nyumbani rasmi,” anasema Masao.

Kumalizika kwa vita hakukuwa mwisho wa changamoto za wawili hao kwani kutokana na uharibifu uliotokana na vita, walikabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi.

“Tulikuwa na uhaba wa chakula na nguo. Hata mume wangu alipopata kazi bandarini, ndoa ikawa na changamoto kama ya mwanzo, alitakiwa kusafiri mara kwa mara.

“Shukrani pekee ni kwa uvumilivu wangu, kabisa,” anasema Miyako, kauli inayosindikizwa na tabasamu lake la kichovu kutokana na umri wake.

Katika kuadhimisha miaka 80 ya ndoa yao mwaka juzi; ndugu, jamaa na marafiki waliwaandalia sherehe, ambayo wazee hao walisema hawakubahatika kuipata wakati wakivishana pete wala kufunga pingu za maisha.

Wengi kati ya waliohudhuria sherehe hiyo walionekana kuvutiwa na picha za wawili hao walioonekana wenye furaha iliyopitiliza.

Akivizungumzia vikongwe hivyo, mmoja kati ya mabinti zao, Etsuko Kawamura, anasema: “Si tu bado wazazi wetu wana nguvu, pia mama aliweza kupika vizuri tu hata alipokuwa na umri wa miaka 98.

Wakati binti yao huyo mkubwa akiwa na hamu ya kuishi kwenye ndoa kwa muda mrefu kama ilivyo kwa wazazi wake hao, iko hivyo pia kwa mwanawe aitwaye Aya Ozawa.

Hapa Ozawa anamzungumzia babu yake, Masao, anasema alipokuwa mdogo alikuwa akimwogopa kutokana na mwonekano wake wa kizee.

“Nilipokuwa mdogo, nilikuwa namuogopa babu kidogo lakini nilipokuwa mkubwa, tulitazama soka na kucheza pamoja.

“Pia alikuwa akinisimulia mengi kuhusu vita. Tulifanya hivyo mara nyingi tu na alikuwa akinishangaza kwa wepesi aliokuwa nao licha ya umri wake. 

“Najivunia kuona babu na bibi yangu wakipewa tuzo ya Guinness World Records,” anasema Ozawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles