HIFADHI YA TAIFA ZIWA MANYARA NA VIVUTIO VYA AINA YAKE

0
1001
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Noelia Myonga (kushoto), akifafanua jambo kwa mwandishi wa makala hii, baada ya kutembelea kivutio cha fuvu la kiboko.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Noelia Myonga (kushoto), akifafanua jambo kwa mwandishi wa makala hii, baada ya kutembelea kivutio cha fuvu la kiboko.

Na Kulwa Karedia,

“HII ndiyo Hifadhi ya Taifa yenye vivutio pekee vya ajabu, kama vile simba wanaopanda miti na chemuchemu ya maji moto”

“Lakini pia kuna kivutio kingine ambacho nadhani hakipatikani maeneo mengine ambacho ni daraja lililotengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu linapita juu ya miti ndani ya hifadhi hii.”

Hayo ni maneno mazuri ya utangulizi ya Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Noelia Myonga, wakati wa mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika wiki iliyopita ofisini kwake katika Mji mdogo wa Mto wa Mbu mkoani Arusha.

Anasema hifadhi hiyo ambayo ni ya pili kuanzishwa mwaka 1960, wakati inaanzishwa Desemba 16, 1960, ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 330 kwa eneo lote kuonekana lina mvuto wa aina yake.

Anasema ni ya pili kuanzishwa baada  ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ilikuwa na mahitaji makubwa ya wanyama aina ya tembo ambao walikuwa na mapito katika maeneo hayo.

“Ilionekana wanyama wengi wakati walikuwa kusini mwa hifadhi, ukafanyika utaratibu wa kuongeza maeneo kwa ajili ya mgawanyiko na shoroba kuungana na tembo waliopo maeneo ya Ngorongoro, hapo katikati kuna mapori kuelekea milima mitatu, Simanjiro mpaka Makuyuni hadi maeneo  ya Selela.

Anasema wanyama wanatambua kuwa na vizazi endelevu, kama ilivyo kwa binadamu ambao hawaoleani, nao wanyama wanahitaji kuchanganya vizazi, ikaonekana hatua za haraka zinahitajika.

“Kuanzia wakati huo, uongozi uliokuwapo ulianza mchakato wa kupata eneo zaidi na kulikuwa na msitu wa Marang’ ambao ulikuwa msitu wa hifadhi chini ya Idara ya Misitu na Nyuki, walifanya mawasiliano mbalimbali ili tembo wasiharibiwe maeneo yao.

Anasema kutokana na hali hiyo, uongozi wa wakati huo ulianza kufanya mawasiliano ya kupata shamba la maji moto namba moja, namba mbili na namba tatu yanafuatana.

“Mashamba haya yalikuwa ya wawekezaji wenye hatimiliki (wawekezaji wakubwa), taratibu mbalimbali zilifanyika hiyo ilikuwa mwaka 1974, aliyekuwa mkurugenzi wa hifadhi za Taifa, aliwasilisha mada katika kikao kilichofanyika Hanang’ na wakamwelewa vizuri na umuhimu wa hifadhi ukaonekana Tanapa wakapewa shamba namba moja kwa sababu mwekezaji aliondoka miaka mingi ya 50 huko na shamba likarudishwa serikalini.

Anasema baadaye Serikali kupitia Wilaya ya Hanang’, walikubaliana eneo hilo ni muhimu kwa uhifadhi eneo endeleo hasa kwa ajili ya tembo.

Anasema ilipofika 1990, mashamba hayo yalinunuliwa na Tanapa na umiliki ukahamishiwa kwenye mamlaka hiyo rasmi, baadaye zilifuata taratibu za kujumuishwa kwenye maeneo hayo, ambapo taratibu zilifuatwa kuanzia ngazi ya kijiji, kamati ya ushauri ya wilaya, mikoa na ngazi zote hadi bungeni na hatimaye Bunge likapitisha azimio maeneo hayo yawe ndani ya hifadhi mwaka 2008.

“Mwaka 2009 lilitoka tangazo jingine  la Serikali la kujumuisha maeneo hayo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara na sehemu ya Ziwa Manyara kuelekea usawa wa kusini. Kwa ujumla hifadhi ikapata kilomita za mraba 648,” anasema Myonga.

Anasema wanafanya kazi kwa mgawanyiko ili kusimamia vizuri utajiri ambao Mungu ametupatia, kila miaka mitano tuna kitabu kinachotuongoza kusimamia mpango wa uhifadhi.

“Haya mapito ya wanyama yanaunganisha eneo la hifadhi ya Ngorongoro, imekuwa na vivutio vingi ambavyo kwa kweli ni hazina kubwa kwa Watanzania na wageni wanaotoka nje ya nchi.

Asema lengo la kuanzishwa hifadhi lilikuwa ni kuhakikisha Ziwa Manyara ambalo limezunguka maeneo kadhaa mpaka ya wilaya za jirani, linaendelea kutunzwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo kutokana na kuwapo hatari ya kutoweka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu.

Anasema ndani ya hifadhi hiyo, kuna vivutio vingi ambavyo wakati inaanzishwa ilikuwa na wanyama wakubwa watano (big five) kama tembo, simba, faru, nyati na chui.

“Utaona aina hii ya wanyama hawa ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii tangu miaka hiyo wapo hapa, jambo ambalo limesaidia mno kupata watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Hii ndiyo hifadhi pekee ambayo unaweza kuja na kuona simba wanapanda miti…hili ni jambo  ambalo linaonekana kuwa la ajabu, lakini ndiyo aina ya vivutio kwa wageni. Ninaamini hii ni kutokana na kuwapo na misitu minene ambayo wanyama wa aina hii huipendelea mno.

Anasema mwaka 1982, eneo hilo liliongezwa kwenye uhidhafi wa kimataifa (Biosphere Reserves) ambako kwa Tanzania  kuna maeneo matatu tu.

VIVUTIO

Anasema wamefanikiwa kubuni vivutio vingi ndani ya hifadhi hiyo, ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa daraja la kisasa ambalo kwa Afrika Mashariki linapatikana Tanzania pekee.

“Daraja hili limejengwa juu ya miti ndani ya hifadhi, lina urefu wa mita 18 juu mpaka chini na kwa wakati mmoja, lina uwezo wa kubeba watu wanne na urefu wake miaka 400.

“Ukiwa juu ya daraja hili, una uwezo mzuri wa kuangalia wanyama, mandhari nzuri ya hifadhi…hiki ni moja ya kivutio ambacho kwa kushirikiana na mwekezaji tumefanikiwa kuwa nacho…tena jambo la kuvutia eneo hili ni kwamba mwaka mzima ni kwenye msitu wa kijani tupu kama vile mtu anamwagilia…watalii wengi wanavutiwa, kuna maji yanapita eneo hili,” anasema Noelia.

Anasema hata kama nchi kama Rwanda au Kenya watakuwa na daraja za aina hiyo, zitakuwa ni ndogo mno kwa utafiti wao walioufanya.

MAJI MOTO

Anasema miaka miwili au mitatu iliyopita, waliweza kuongeza  kivutio kingine cha kipekee ndani ya hifadhi hiyo kwa kujenga daraja kubwa na lenye kuvutia zaidi watalii.

Anasema wageni wanavutia kuona maji moto ndani ya hifadhi, hata ukiwa yai linaiva ndani ya dakika sita.

“Eneo hili tumejenga daraja la kisasa, watalii wanapita moja kwa moja hadi ndani ya ziwa. Pia kuna ndege wengi  aina ya flamingo ambao wanapita eneo hili kwa sababu ya kuwapo na chakula cha kutosha…ni uoto wao wa asili ambao wanaupenda… watalii wengi wanapenda mno kufika eneo hili kujionea.

“Bado tupo kwenye mpango wa kuongeza vivutio zaidi vya aina fulani za masaji ili watalii wakifika hapa wanaburudika kwa kupata joto la maji, kwa sababu wanasema yana tiba.

“Tunategemea kujenga kitu kama bwawa hivi, mtalii akifika hapa amechoka anaweza kufanyiwa ‘massage’, tunaamini ni kivutio kizuri zaidi,” anasema.

NDEGE

Anasema kuna aina nyingine ya kivutio cha ndege  wanaohama kutoka Bara la Afrika kwenda Ulaya.

“Tumebahatika kuwa na ndege wanaohama, wanatoka Afrika wanakwenda Ulaya na mabara mengine…hawa huwa na vitu fulani kwenye vichwa vyao (homing).

“Mara nyingi wanakuwa hapo Machi, hadi Juni, ukija Julai unaweza usiwakute…hawa wanaitwa Korongo Domo njano (yellow billed stoke), ni kivutio kikubwa, watalii wengi wanapenda kuja msimu kama huu kuwaona… kamwe hawana athari yoyote kwa binadamu.

“Wanapenda kurudi Ziwa Manyara, kwa sababu wanafuata chakula cha kutosha ambacho ni samaki kutoka Ziwa Manyara, viluwiluwi na vyura ambao wanapatikana kwa wingi…chakula kikiwa kingi na kukuta mazingira mazuri wanakaa muda mrefu.

“Wanatumia muda wao mwingi kula na kushiba ili kutaga mayai, wakishaangua huwalisha kwa bidii vifaranga ili kuanza safari kurudi Ulaya. Kwa Afrika wanapenda kutua nchini Madagascar kisha kuendelea na safari.

“Hawa ndege wengine huwa wanafungwa vifuatiliaji, iliwahi kutokea wageni walikuja hapa mpaka wakalia, wakisema waliwahi kuwaona nyumbani kwao (Ulaya)… inawezekana waliwapiga picha huko huko kwao…ni jambo la kufurahisha katika hili,” anasema.

SHUGHULI ZA KIBINADAMU

Anasema kadiri siku zinavyodi kwenda, kumekuwapo na shughuli nyingi za kibinadamu ambazo kwa namna moja au nyingine, zinahatarisha uhai wa Ziwa Manyara.

“Kumekuwapo na shughuli za kinabadamu ambazo si rafiki katika masuala ya uhifadhi, zinakwenda kwa kuathiri Ziwa Manyara hasa kilimo, ziwa hili lipo bondeni… kilimo kinachofanyika maeneo ya miinuko si rafiki, udongo mwingi unasombwa na kuja kujaza kwenye ziwa… kina chake kinazidi kupungua.

“Kwa takwimu za miaka ya nyuma ziwa lilikuwa na kina cha mita nne na nusu, lakini hivi sasa kimepungua hadi maeneo mengi ni mita moja na nusu… ni changamoto wadau mbalimbali, maofisa ugani kupitia ofisi husika na wakurugenzi wa halmashauri kufanya uamuzi wa kutoa elimu kwa vitendo na kuelekeza wananchi namna ya kulima ili udongo usije kwa kasi kubwa ziwani.

“Kama tukipoteza ziwa ina maana uwezekano wa kupoteza wanyama au ndege hawa hawataweza kurudi hapa, watahamia maeneo mengine, hata wale flamingo watakosa chakula,” anasema Noelia.

Anasema Ziwa hilo ambalo limezungukwa na wilaya za Monduli, Babati, Karatu na Mbuli, linapaswa kulindwa kama mboni ya jicho.

“Kama hali hii haitadhibitiwa, ikolojia inayotengenezwa na samaki na ndege hawa yote itapotea kabisa…hii ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi kwelikweli,” anasema Noelia.

Anasema kupungua kwa kina cha ziwa, kumesababisha utalii wa mitumbwi kukosekana katika miaka ya karibuni.

“Sisi kama shirika tunaendelea kutoa elimu, lakini tunaamini kabisa maofisa ugani wanayo nafasi ya kushughulikia jambo hili…tumefanya vikao vingi na wadau wanaozunguka ziwa hili ili kunusuru janga hili,” anasema Noelia.

UTALII WA USIKU

Anasema utalii wa usiku ambao unapendwa kutumiwa na watalii wengi, kwa sababu ndiyo muda wao mzuri wa kuwaona wanyama ambao wanapenda kutembea usiku tu.

“Wengi wao wanafurahi kuona kuna wanyama wanaopenda kuwinda usiku, wanyama wengi usiku huwa hawaoni vizuri…pia kuna wanyama wa kuwindwa wanaotembea usiku, kama vile kiboko,” anasema.

WATANZANIA

Kuhusu mwitikio wa Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa, Noelia anasema umekuwa si wa kuridhisha kwa kuwa kasi ni ndogo.

“Watanzania wanatutembelea, tunawashawishi waje kwa wingi tumejitahidi kutangaza, mwitikio bado.

“Si kwamba hawana uwezo, utamaduni au mwamko wa kuwekeza fedha kwa ajili ya kutembelea kama wageni wa nje…bado hawaoni thamani ya kufanya hivi, tukiamua tunaweza.

“Huwa nafanya matembeezi kwenye minada naona Watanzania wanaagiza nyama mguu mzima wa mbuzi, ni kuamua na kuwa na mpangilio… ukija hapa unalipa Sh 11,800 za kiingilio pamoja na VAT), gharama za usafiri ni kidogo kwa Mtanzania…tunawakaribisha kwa wingi,” anasema.

Anasema hata wakati wa maadhimisho wa Siku ya Mazingira Duniani, Serikali ilitoa ofa kwa Watanzania kuingia katika hifadhi zote ambapo kwake watu 1,582 walikwenda kutembela hifadhi.

“Si kila mwaka tunatoa ofa kama hii, maana idadi ilipanda mno…tukifanya tunaweza kushindwa kujiendesha…lazima Watanzania si wote, wajenge utamaduni wa kulipa hata kidogo,” anasema.

UJAMBAZI

Anasema moja ya jambo ambalo liliwahi kumnyima usingizi, ni matukio ya ujangili ambao kwa kweli yalisababisha wanyama kama vile tembo kuuawa kwa wingi.

Anasema kazi ya kupambana na ujangili ni ngumu, lakini wao kama shirika wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa mno ndiyo maana mpaka sasa hali imetulia.

“Jambo hili huwa linatukosesha usingizi timu nzima, wale watu wanakuwa na mbinu nyingi kila kukicha, nasi tumejizitati kwelikweli, tumeimarisha doria zetu, tunashirikiana na wananchi ambao wanazunguka hifadhi hii na vyombo vingine vya dola kupambana na tatizo hili.

“Kwa kweli wizara yetu imefanya kazi kubwa, hatulali tunafanya kazi usiku na mchana kupambana na tatizo hili…nakumbuka ilifikia hatua majangili yalianza kutumia sumu kuua wanyama kwa wanyama ambao wanakula maboga kama tembo, wengi walikufa,” anasema.

MIGOGORO

Anasema hifadhi hiyo inazungukwa na vijiji 46, jambo ambalo wakati mwingine husababisha migogoro hasa ya mipaka.

“Sheria zetu zinasema wananchi wanapaswa kuishi umbali wa mita 500 kutoka eneo la mbuga, lakini cha ajabu wapo wanaingia ndani na mwisho wa siku hujikuta wanashambuliwa na wanyama wanaokwenda kuvamia mashamba.

“Lakini pia wananchi hawa huingiza mifugo mingi ndani ya hifadhi, jambo ambalo husababisha magonjwa na uharibifu mkubwa wa ardhi. Na mwananchi wa kawaida akiona mnyama amevamia shamba anasema ni kazi yetu kumtoa, ukweli jambo hili lipo chini ya ofisa wa idara ya wanyamapori ambao anakuwa chini ya ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri husika,” anasema.

Itaendelea wiki ijayo kwa kuangalia masuala ya ujirani mwema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here