LONDON, ENGLAND
NYOTA wa zamani wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, amedai kuwa anatamani kuja kuwa kocha wa klabu hiyo ambayo inafundishwa na aliyekuwa kocha wake, Arsene Wenger.
Wenger alimteua Henry kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18, lakini aliamua kuachana na timu hiyo ya vijana mara baada ya Wenger kumtaka achague jambo moja kuwa kocha wa timu hiyo au kuwa mchambuzi wa habari za michezo.
Henry mbali na kuwa kocha wa vijana, pia alikuwa na mkataba katika kituo cha utangazaji cha Sky Sports kwa ajili ya masuala ya uchambuzi, hivyo alikuwa anafanya kazi sehemu zote mbili kwa wakati tofauti.
Kauli ya Wenger ilionekana kumgusa sana Henry, hivyo aliamua kuachana na ukocha katika klabu hiyo ya vijana na kuendelea na majukumu yake ya uchambuzi.
Hata hivyo, mchambuzi huyo ameweka wazi kuwa ana ndoto za kuja kuwa kocha wa klabu hiyo kutokana na kuwa na mapenzi ya dhati.
“Nitakuwa muongo nikisema kuwa sitaki kuja kuwa kocha wa Arsenal, siku zote nimekuwa nikiipenda klabu hiyo kwa kuwa nimekuwa hapo kwa miaka mingi, hivyo Arsenal bado ni timu ninayoipenda.
“Ninaamini ipo siku nitakuja kuwa kocha wa Arsenal, si mbali sana kutoka sasa kwa kuwa ni kazi yangu.
“Kwa sasa naweza kuwa kocha wa klabu yoyote kutokana na leseni yangu, hivyo ninachokiangalia ni kuja kuwa kocha wa Arsenal, naendelea kujifunza mambo mbalimbali katika soka ili kuja kuwa bora zaidi.
“Ninachokijua ni kwamba kabla ya kuja kuwa kocha mkuu, lazima uwe na uzoefu, ninachojaribu kukifanya ni kuyafanya yale yote ambayo kocha anatakiwa kuyafanya.
“Ninaitakia kila la heri Arsenal kwa sasa na katika msimu mpya wa Ligi Kuu, ninaamini itafanya vizuri,” alisema Henry.