28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Heko JPM kwa kurudisha utaratibu wa zamani mafao ya wafanyakazi

RAIS Dk. John Magufuli, jana aliagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani wa ulipaji wa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu uliokuwa ukitumika kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Ametaka utaratibu huo utumike hadi mwaka 2023 wakati wadau wakijadiliana juu ya kikokotoo kitakachotumika kulipa mafao hayo bila kuathiri mfuko na wastaafu kulipwa vizuri.

Magufuli alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), vyama shiriki, viongozi wa mifuko ya hifadhi ya jamii (PSSSFna NSSF), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Katika mkutano huo, alisikiliza maoni ya viongozi hao kuhusiana na utekelezaji wa Sheria ya Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2018 na kanuni zake ambapo viongozi hao wameelezea changamoto zilizojitokeza kwa wastaafu kulipwa kiasi kidogo cha fedha za mafao ya mkupuo (asilimia 25 badalaya asilimia 50 ya zamani) na taharuki iliyowakumba wafanyakazi ambao ni wastaafu wa baadaye.

Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Magufuli alisema uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya PSPF, LAPF, GEPF na PPF na kuunda mfuko mmoja wa wafanyakazi wa Serikali uitwao PSSSF pia kuwa na mfuko mmoja wa wafanyakazi wa sekta binafsi uitwao NSSF, ulitokana na mapendekezo ya wadau yaliyolenga kuondoa mkanganyiko wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu na pia kuokoa baadhi ya mifuko iliyokuwa mbioni kufa kutokana na kuelemewa na madeni ya wastaafu.

Sisi MTANZANIA Jumamosi tunaunga mkono uamuzi huo wa Magufuli kwa sababu umeangalia masilahi mapana ya haki za wafanyakazi.

Tunatambua kwamba katika kipindi cha mpito ambacho Rais amekitoa, kitatoa mwelekeo mpya wa kikokotoo  kisichokuwa na uminyaji wa haki ya mfanyakazi.

Tayari Serikali imeonyesha nia yake njema ya kuhakikisha imedhamiria kunusuru hali hiyo kwa kulipa deni la makato ya wafanyakazi kwa mifuko ya hifadhi ya jamii la Sh trilioni 1.23 ambalo lililimbikizwa.

Pia imewalipa wastaafu waliokwama kulipwa mafao yao kiasi cha Sh bilioni 550 kati ya Sh bilioni 774 walizokuwa wakidai huku waliobaki wakiendelea kulipwa kadiri uhakiki unavyofanyika.

Pia tunaiunga mkono Serikali juu ya msimamo wake wa kwamba haiko tayari kuona wafanyakazi wanakatishwa tamaa na haiko tayari kuona wastaafu wanapata shida baada ya kuitumikia nchi yao.

Hivyo tunaamini kurejeshwa utaratibu uliokuwa ukitumika kabla ya mabadiliko kumewapa matumaini mapya wafanyakazi kwa kuamini hata mazungumzo yanayoendelea kufikia mabadiliko ya mwaka 2023 yatakuwa yenye tija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles