33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hekaheka za kampeni zilivyofanya Mkapa anusurike kupata ajali ya ndege

Andrew Msechu-Dar es Salaam

RAIS Mstaafu Benjamini Mkapa, ameeleza jinsi alivyomlazimisha rubani kutua kwenye mazingira magumu wakati wa kampeni, hali iliyofanya ndege yao ikaribia kuanguka.

Ameeleza hayo kwenye kitabu chake cha “My Life, My Purpose” (Maisha Yangu, Kusudio Langu), kilichozinduliwa na Rais MJohn Magufuli Novemba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mkapa anasema hekaheka za kampeni hazikuwa kitu rahisi na kwamba akiwa mgombea aliyepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), asingeweza kuacha kufika katika kila wilaya nchini.

Anasema anakumbuka namna ambavyo alikuwa akipokelewa na umati wa watu, ngoma, mashairi na kila aina ya mapokezi ikiwemo kuombwa kupiga picha za kumbukumbu na wananchi katika kila eneo alilopita.

Anasema anakumbuka alipolazimika kuahirisha safari yake kwenda kwenye kampeni Ifakara ambapo viongozi wa CCM walimweleza kuwa amewaudhi wananchi kwa kuahirisha safari hiyo imeonesha haoni umuhimu wa watu wa huko na kwa mtanzamo wao yeye (Mkapa) alitembelea maeneo ambayo si ya muhimu kama ilivyo Ifakara.

Anasema kutokana na hali hiyo, alilazimika kwenda Ifakara akitumia ndege ili kuokoa muda, ambapo alisafiri kwa ndege ndogo aina ya Cessna.

Anasema anakumbuka, siku hiyo mvua ilikuwa imenyesha sana na rubani hakuwa na uhakika kama wangeweza kutua salama kwenye uwanja wa nyasi uliotarajiwa na walipofika, rubani alipotaka kutua, alighairi akiwa umbali wa meta moja kutoka ardhini .

“Tuliendelea kuzunguka angani mara kadhaa huku tukijadiliana iwapo tutue au tuahirishe na kurudi zetu Dar es Salaam, tuliona mamia ya watu wakiwa wamekusanyika na miavuli yao wakitusubiri kwenye mvua. Nilifikiria ni kwa kiasi gani tutawaudhi watu wale iwapo tutaamua kuondoka, nilimuamuru rubani atue.

“Tulipokuwa tukizidi kukaribia kwenye uwanja, ndivyo ndege iiliyoonyesha kupoteza ushirikiano, ilikuwa ni hali ya kutisha kwetu, hakukua na afadhali hata baada ya ndege kugusa ardhi, ardhi ilikuwa na utelezi na zaidi ilianza kupoteza mwelekeo tukiwa ardhini lakini hatimaye rubani alifanikiwa kuidhibiti,” anasema.

Anasema umati uliokusanyika hapo uliwapokea kwa shangwe na baada ya kumaliza, walipokuwa wakiondoka, rubani aliwaamuru wajiandae vizuri kwa kuwa wakati wa kuondoka unaweza kuwa mgumu kuliko wakati wa kutua.

“Rubani wetu ambaye alionyesha kuwa mzoefu, alituambia alibaini kulikuwa na kichuguu mita chache toka ndege iliposimama, hivyo alilazimika kurudisha nyuma na kuigeuza, ni kwa bahati tu kwamba tulinusurika,” anasema.

Utoaji wa maamuzi

Katika kitabu chake hicho, Mkapa anasema wakati wa utawala wake, alijitahidi kuwa wazi na kushirikiana na mawaziri wake kwa karibu kabisa.

Anasema alipoingia madarakani, kwa mtu ambaye hakumjua vyema awali alitambua kuwa hakuwa mtu mwoga, hakufanya lolote kwa woga na kwamba kiongozi lazima awe mtu wa kuwapa watu moyo wakati mwingine.

Anasema ilipotokea tatizo katika wizara, aliwasiliana na Waziri Mkuu, kisha waziri husika na mara nyingi alipenda kumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikaki ambaye alikuwa akitoa mtizamo wa kisheria kuhusu suala husika.

Anasema wakati wote aliwasisitiza mawaziri kujua mipaka yao kimamlaka na ni wakati gani wanatakiwa kutumia mamlaka yao na wakati gani hawahitaji kuyatumia.

“Ninapokaa na kuangalia nyuma sasa, ninabaini kuwa niliwahi kufanya makosa kwa baadhi ya watu waliokuwa wateule wangu, katika mihula yangu miwili ofisini,” anasema.

Anasema alikuwa wazi sana kwa mawaziri wake na alijifunza kutoka kwa Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtulivu, msikivu na kutafuta suluhu kwa kadiri ilivyowezekana, lakini zaidi kuweka mazingira bora na shirikishi ya utendaji kazi.

Anasema kwa baadhi yao ambao waliwahi kufanya kazi na Mwalimu, waliwahi kushuhudia akitoa ufumbuzi wa matatizo lakini akiendelea kutoa nafasi ya majadiliano ili kuwapa wengine wasaa wa kuelewa kwa undani kuhusu maamuzi aliyoyatoa.

“Nilijaribu kufuata utaratibu huo wa kushauriana na baraza langu la mawaziri. Niliona ilikuwa vyema kwangu katika utendaji, kwa sababu kwanza wengi tulikuwa katika umri unaokaribiana, kwa hiyo majadiliano yetu yalikuwa wazi sana.

“Hata hivyo kulikuwa na changamoto hasa katika kufikia makubaliano na baadhi ya mawaziri wangu na nilikuwa makini sana katika mambo yanayohusu masuala ya kisera, nilikuwa nikifanya juhudi zaidi kujua kwa undani kwa hiyo haikuwa rahisi kwangu kufanya maamuzi yasiyo sahihi,” anasema.

Anasema mara nyingine baraza lilikuwa likikosoa maamuzi yake na walikuwa na utamaduni wa kulifanya baraza kuwa mshauri wa Rais, walimshauri na hatimaye Rais alitoa maamuzi.

“Rais anaweza kupuuza ushauri wowote anaopewa na matokeo yake ni kwamba iwapo kuna waziri aliyeona hakutendewa haki katika hilo alikuwa huru kujiuzulu, ninashukuru haikutokea waziri yeyote kujiuzulu kwa sababu hiyo katika utawala wangu,” anasema.

Anasema alitambua kuwa yeye ndiye anayebeba majukumu yote na kuna wakati alilazimika kuwaambia mawaziri wanne wajiuzulu, watatu katika kipindi chake cha kwanza ambao ni Juma Ngasongwa, Simon Mbilinyi na Kilontsi Mporogonyi, japokuwa badaye alimrejesha Ngasongwa baada ya uchunguzi kumsafisha.

Anasema katika kipindi chake cha pili, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba alijiuzulu baada ya kuonekana alikuwa akitumia mamlaka yake kuhusisha shughuli za Serikali na maslahi yake binafsi.

Anasema mwingine alikuwa Waziri wa Nchi, Hassy Kitine ambaye alilazimika kujiuzulu baada ya kubainika mkewe alitoa taarifa za uongo kuhusu gharama za matibabu aliyofanyiwa huko Marekani.

Mkapa anasisitiza kuwa ni muhimu kiongozi kuwa karibu na watu japokuwa inahitaji ujanja ili kuwajua wakweli na wasio wema, hasa katika nchi zinazoendelea ambapo ukiwa karibu sana na watu fulani hutumia nafasi hiyo kama njia ya kujinufaisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles