23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hekaheka ya corona

Waandishi Wetu – Dar/Mikoani

HALI ya taharuki na hekaheka imetanda maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na kuwapo kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitangaza kugundulika kwa mgonjwa mmoja ambaye aliwasili nchini Jumapili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), akitokea Ubelgiji.

Mgonjwa huyo Isabela Mwampamba (36), ambaye ni mmiliki wa shule binafsi ya Upendo Friends iliyopo jijini Arusha, anaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru.

Tangazo la kuwapo kwa mgonjwa huyo limeongeza mwamko wa watu kujikinga ambapo katika maeneo mbalimbali ya nchi kumeshuhudiwa matukio yaliyoashiria tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Wananchi wengi wameonekana kuvaa vifaa vya kujikinga sehemu za puani na mdomoni, mipira ya mkononi (gloves) na wengine walikuwa wakitembea au kuingia katika vyombo vya usafiri kwa tahadhari kubwa kuepuka kugusana.

Pia katika ofisi mbalimbali za umma na binafsi kulikuwa na vitakasa mikono na sabuni (sanitizer dispenser) na kila mtu aliyeingia alisisitizwa kuvipaka.

Wakati hali ikiwa tete kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, shughuli nyingi ikiwamo mikutano ambayo ilitarajiwa kufanyika kwa kuhusisha mikusanyiko ya watu wengi imesitishwa.

MAAGIZO YA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alitangaza hatua za dharura kukabiliana na corona ikiwemo kufunga shule kwa siku 30 na kuzuia mikusanyiko yote.

Alisema Serikali imeamua kufunga shule zote kuanzia za chekechea hadi kidato cha sita na kusitisha mikusanyiko yote mikubwa ya nje na ya ndani.

Majaliwa alisema mikusanyiko hiyo inahusisha ile ya warsha, semina, mikutano ya siasa na michezo ikiwemo ya soka kama Ligi Daraja la Kwanza, la Pili na mingine.

Katika kutekeleza hilo, Majaliwa aliiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuyaandikia mashirikisho yote ya michezo kuwaeleza kuhusu hatua hiyo.

Alisema pamoja na uamuzi huo, Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu maeneo yote ambayo yanatumiwa kupitisha wageni, ikiwemo kwenye viwanja vya ndege, bandari na mipakani kwa kuweka vipimo maalumu vya kubaini watu walioathiriwa na ugonjwa huo.

“Hatua hizi zinalenga kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini na pamoja na tahadhari hiyo, Watanzania waliopo maofisini, mashambani na maeneo ya uzalishaji mali waendelee kuchapa kazi kwa nguvu zote na huu ni wakati mzuri wa kufanya kazi ili kuzalisha mali kwa wingi,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali imechukua hatua za kumuhifadhi mgonjwa husika kwenye karantini kwa uangalizi na tayari imeshafuatilia watu wote waliokutana naye ambao nao wamewekwa kwenye karantini kwa siku 14, huku wakiendelea kupimwa sampuli ili kujua iwapo wameambukizwa.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuimarisha udhibiti wa wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia nchi kavu na kwenye viwanda vya ndege na kuimarisha uwezo wa kupima kupitia maabara za Serikali na kwamba Maabara ya Mkemia Mkuu tayari ina uwezo wa kupima sampuli ili kubaini maambukizi ya virusi hivyo.

Majaliwa alisema Serikali pia imeamua kuweka maeneo maalumu ya karantini katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba na kwamba inaendelea kuweka maeneo zaidi ya dharura.

“Lakini pia, Rais John Magufuli jana (juzi) alitangazia umma kuwa amechukua hatua kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru na fedha zaidi ya Sh bilioni moja zimepewa maelekezo ziende Wizara ya Afya kwa ajili ya vifaa na tiba ya ugonjwa wa corona, tayari Sh milioni 500 zimeshapelekwa Wizara ya Afya,” alisema Majaliwa.

Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo na kuvitaka viendelee kuelimisha umma.

Aliwaomba wananchi waendelee kutoa taarifa kupitia namba maalumu zilizotolewa na Wizara ya Afya ambazo ni 0800110124 au 0800110125 au 0800110037 ambazo zitakuwa tayari kupokea taarifa pale ambapo wanapata wasiwasi wa kuona watu wenye dalili za ugonjwa huo.

CCM YASITISHA MIKUTANO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha mikutano yote ya ndani na ya hadhara kukabiliana na tishio la corona.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema jana kuwa kulikuwa na ziara za viongozi wa chama akiwemo makamu mwenyekiti bara, katibu mkuu, manaibu katibu wakuu bara na Zanzibar na wakuu wa idara, lakini zimesitishwa hadi watakapotoa maelekezo mengine.

“Tuna matukio makubwa ya ujenzi wa chama ndani na nje ya chama, lakini kuanzia leo (jana) shughuli zote zenye asili ya mikusanyiko mikubwa iwe ya ndani au ya hadhara zisitishwe mara moja kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na ugonjwa huu,” alisema Polepole.

Alisema vikao vya chama vilivyo kwenye kalenda ambavyo si vya mikusanyiko mikubwa, kama kamati za siasa na halmashauri kuu, watatoa maelekezo namna ya kuvifanya.

Pia aliagiza katika ofisi zote za chama hicho kuwekwa dawa maalumu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Pia alipendekeza kwa viongozi na wana–CCM wengine kusalimiana kwa kunyoosha alama ya dole gumba badala ya kushikana mikono au kukumbatiana kama njia ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Tusishikane mikono, si kwa maana mbaya, bali kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa huu mpaka pale tutakapojiridhisha hakuna hatari,” alisema Polepole.

HOTELI YAFUNGWA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema wameifunga Hoteli ya Themi Valley iliyobainika kuwa na mgonjwa na kwamba watu waliokuwepo wakiwemo wageni na wahudumu hawataruhusiwa kutoka eneo hilo.

“Hoteli tumeifunga na hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kutoka au kuingia wakiwemo wafanyakazi na wageni.

“Tumechukua sampuli za watu wote waliokuwa wanaishi katika hoteli hiyo, zitasafirishwa kwenda maabara iliyopo Dar es Salaam, kama kuna wengine ambao wameambukizwa tumetenga eneo maalumu, akipatikana mgonjwa anawekwa hapo,” alisema Gambo.

Aliwataka maofisa wa Serikali waliopo kwenye mipaka ikiwemo ya Namanga, Ngorongoro, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA na uwanja mdogo wa Arusha kuongeza umakini.

MTANDAO WA MGONJWA

Gambo alisema wanaendelea kufuatiliamtandao mzima wa mgonjwa, alioshirikiana nao kwa namna moja ama nyingine.

Alisema tayari dereva aliyempakia mgonjwa huyo amechukuliwa vipimo vya sampuli ambavyo vimetumwa Dar es Salaam kwenye maabara kwa uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa Gambo, dereva huyo baada ya kumshusha mgonjwa, alikwenda nyumbani ambako ana mke na watoto wanne na alikutana nao kwa maana ya kushikana mikono kama sehemu ya familia.

“Wale watoto walivyoamka asubuhi (Jumatatu) wakaenda shuleni (Shule ya Msingi Engusingiu), kule wamekutana na watoto wengine ambao tunadhani inaweza kuwa sehemu ya changamoto,” alisema Gambo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema dereva huyo aliwaeleza kuwa juzi alipata abiria wengine wawili ambao aliwapeleka Karatu kwenye kituo kinachoitwa Mwema Children Center ambako walikaa kwa muda na watoto kisha kurejea jijini Arusha.

“Baada ya kupata taarifa hiyo jana (juzi) hiyo hiyo usiku nilimjulisha Mkuu wa Wilaya ya Karatu aende kwenye kituo hicho akiwa na wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua watu waliopo pale, wawape elimu, kuchukua sampuli na kuelekezwa wasiende popote mpaka baada ya siku 14,” alisema Gambo.

VITAKASA MIKONO BEI JUU

Vifaa vya kujikinga vikiwemo vitakasa mikono (sanitizer) na vile vya kuziba pua na mdomo vimeanza kuadimika baada ya kutangazwa kuwapo kwa mgonjwa wa corona.

Sabuni hizo zilizoelekezwa na Wizara ya Afya zitumike kunawia mikono kujikinga na ugonjwa huo, zimeadimika ambapo inadaiwa baada ya mgonjwa huyo kubainika zilisafirishwa kupelekwa nchini Kenya.

Pia katika baadhi ya maduka ya dawa na maduka makubwa zilipanda bei maradufu kutoka Sh 3,000 hadi 6,000 huku wengine wakiuza hadi Sh 20,000.

Mmoja wa wauzaji wa bidhaa hizo jijini Arusha, alisema maduka yanayouza bidhaa za jumla, supermarket na maduka ya dawa wananchi walimiminika kununua bidhaa hizo kujikinga na janga hilo.

“Wateja ni wengi wanafatufa vifaa hivyo, tumeuza ‘stock’ imeisha na wasambazaji wetu wakuu nao hawana zimeisha kote mji mzima, na nyingi tulikuwa tunategemea zinazotoka nchini China,” alisema mfanyabiashara huyo.

Mmoja wa wakazi wa Arusha, Anna Steven, alisema amezunguka kuanzia juzi jioni hadi jana na kila anapokwenda aliambiwa vifaa hivyo vimeisha.

Naye Joachim Solomon alisema tangu jana asubuhi alizunguka kuulizia vifaa hivyo ila kila anapokwenda aliambiwa vimeisha.

Mkoani Kagera MTANZANIA lilitembelea katika maduka ya dawa muhimu pamoja na maduka makubwa ya bidhaa tofauti na kubaini kuwa vitakasa mikono vimeadimika.

Muuzaji wa dawa muhimu katika duka lililopo Hamgembe Manispaa ya Bukoba, Geofrey Rutahiwa, alisema sabuni hizo zimenunuliwa kwa wingi kuanzia Jumatano wiki iliyopita.

“Sabuni yenye ujazo wa milimita sita tunauza Sh 35,000 lakini bei hii inaweza kuongezeka kwa sababu bidhaa zimeadimika,” alisema Rutahiwa.

Naye Joyce Rweyemamu ambaye ni muuzaji katika moja ya maduka makubwa yaliyopo Manispaa ya Bukoba, alisema soko la sabuni hizo limeongezeka katika siku tatu zilizopita.

“Tunauza sana sabuni zilizoelekezwa kwa ajili ya kunawa mikono ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa corona, wateja wengi tunawauzia mils 6 kwa Sh 35,000 na vifaa vya kuziba pua na mdomo (mask) na gloves kwa Sh 1,000.

“Lakini bidhaa ambazo tumebaki nazo hazinunuliwi sana ni mask na gloves, sabuni tumeishiwa na bado tunapata wateja wengi ambao wanadai wamezunguka katika maduka tofauti bila mafanikio,” alisema Joyce.

WAFANYABIASHARA WALIA

Wafanyabiashara wa Soko la Vinyago Jijini Arusha maarufu kama Maasai Market, walisema tangu kutangazwa kwa ugonjwa huo wateja wamepungua.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Ally Kingwe, alisema mapato mengi wanategemea kutoka kwa watalii, lakini tangu kutokea kwa ugonjwa huo idadi ya wanaofika kununua bidhaa mbalimbali za asili imepungua.

“Soko letu tunategemea watalii wa kigeni ila tangu ugonjwa umeingia nchini hakuna mgeni wa kitalii aliyefika hapa.

“Tumechukua tahadhari, kwenye geti la kuingilia tumeweka ndoo ya maji na sabuni kwa ajili ya kila mtu anayeingia, na kila mtu aliye nje ya duka ana maji na sabuni ya kunawa mikono,” alisema Kingwe.

Naye Emanuel Gasper alisema ugonjwa huo umeathiri biashara ya vinyago na vitu vingine vya asili na kushindwa kujua watakidhi vipi mahitaji ya familia zinazowategemea.

“Kipindi cha nyuma kuanzia asubuhi tulikuwa tunapata wateja ila kwa sasa hakuna kabisa, tunaomba Serikali ichukue hatua zaidi ikiwemo kufunga mipaka ili tuweze kudhibiti maambukizi mapya na kulinda afya zetu,” alisema Gasper.

WATALII WAANZA KUSITISHA SAFARI

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya utalii jijini Arusha ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema mwajiri wao amepunguza wafanyakazi kutokana na wageni wengi kusitisha safari zao kwa hofu ya corona.

“Ofisini kwetu watu wamepunguzwa kazi kwa sababu wageni wengi wamesitisha safari, mfano mwezi huu kuna wageni 23 wamesitisha safari kutokana na nchi zao kuwa na maambukizi ya corona.

“Mwajiri ameamua kila idara abaki mtumishi mmoja, tena mwenye usafiri (gari), wanaopanda daladala amewaomba wabaki nyumbani kwanza wakati juhudi za kupambana na ugonjwa huo zikiendelea… tunafanya kazi kwa shida sana,” alisema mfanyakazi huyo.

KAMBI ZA KITAALUMA ‘STOP’

Mkoa wa Simiyu umesitisha kwa muda usiojulikana kambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha sita.

Kambi hiyo ilikuwa ikijumuisha shule 10 zilizoko mkoani humo na wanafunzi 953 ambao walianza masomo tangu Machi Mosi katika Shule ya Sekondari Maswa (Maswa Girls) iliyoko wilayani Maswa mkoani Simiyu.

Akitangaza uamuzi huo jana, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, alisema mbali na kambi hiyo, kambi nyingine ndogo ambazo zinakusanya wanafunzi kutoka shule zisizozidi tatu hazitakuwepo tena.

“Kambi za shule kwa maana ya wanafunzi wa shule moja zitaendelea, lakini kambi ndogo na kubwa hazitakuwepo mpaka ugonjwa huu utakapoisha. Hata zile za darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha pili, nazo hazitakuwepo,” alisema Sagini.

Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Erenest Hinju, alisema wanafunzi hao waliweka kambi ya wiki mbili kati ya sita ambazo walipanga kukaa kwa maandalizi ya mtihani wa taifa.

Baadhi ya wanafunzi walisema kufungwa kwa kambi za kitaaluma kutawaathiri kwani walikuwa wakifundishwa mbinu za kujibu maswali kwa ufasaha.

“Tulikuwa tunafundishwa mada ngumu kwenye masomo ambazo zingetusaidia kujibu maswali kwa ufasaha, ila kwa sasa tunahisi tutakosa maarifa zaidi na mbinu za kufanya mtihani,” alisema William Nyalabwa.

Izack Ndasa alisema kupitia kambi walikuwa wanapata nafasi kujifunza mada ngumu kutoka kwa walimu mahiri.

KKKT IRINGA KUKUTANA

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kanisa Kuu umeitisha kikao cha dharura cha wachungaji wote katika sharika za Iringa Mjini ili kuweka tahadhari kujikinga na corona.

Mchungaji Kiongozi Usharika wa Kanisa Kuu, Bryson Mbogo, alisema wanatarajia kukutana na wachungaji wote Jumamosi kujadili na kuweka mipango ya pamoja kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya imekwisha tangaza kuwepo kwa ugonjwa wa corona nchini na sisi mkuu wa kanisa amekwisha agiza kusitishwa kwa salamu za  kushikana mikono na nyingine ambazo zinaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya corona,” alisema Mchungaji Mbogo.

Alisema wameweka maji ya kunawa mikono na sabuni katika maeneo yote ya ofisi ili watu wanaofika kupata huduma waweze kunawa kabla ya kuingia ndani.

Mchungaji Mbogo alisema wajibu wa kanisa ni kuendelea kuelimisha waumini kuhusu mambo mbalimbali yanayotangazwa na Serikali likiwemo jambo hilo ili kuhakikisha hakuna muumini anayepata maambukizi.

Kwa upande wake, Askofu mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela, alisema uchafu ni dalili ya shetani na kwamba suala la usafi ni hekima ya roho mtakatifu.

“Kwenye hili la ugonjwa wa corona watu wanaelimishwa juu ya kunawa mikono kwa sabuni ila  wapo ambao watapuuza, ni vizuri kila mmoja kuzingatia ushauri unaotolewa,” alisema Askofu Mdegela.

WAFANYABIASHARA WAAHIRISHA SAFARI

Ziara ya wafanyabiashara kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya Aprili 6 na 9 imehairishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Ziara hiyo ililenga kutafuta soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, alisema ziara hiyo imesitishwa kufuatia kuwepo kwa wagonjwa wa corona katika nchi hizo mbili.

“Ziara yetu itafanyika mara baada ya mamlaka husika kutangaza hali ya usalama juu ya ugonjwa wa corona katika nchi zetu,” alisema.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha na kutafuta  masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini hivyo kuhairishwa kwake kunatoa nafasi kwa wafanyabishara na wajasiriamali wengine kujiandaa.

“TPSF ndiyo kiungo cha wafanyabiashara nchini hivyo ziara hii imelenga kutengeneza soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo na wakubwa ili kukuza biashara zao na kufikia maendeleo yaliyokusudiwa,” alisema Ngalula

Alisema Tanzania ndiyo lango kuu la biashara kwa nchi ya Kongo hivyo ni lazima kuchangamkia fursa hiyo na kuongeza masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza azma ya ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Kongo, Luteni Jenerali Mstaafu Paul Mella, aliwatoa hofu wafanyabiashara kuwa hali ya usalama nchini humo ni nzuri wakati wote hivyo wajitokeze kuchangamkia fursa hiyo kujenga na kuimarisha biashara zao.

“Suala la muhimu ni kufuata taratibu zote zinazotakiwa katika kufanya biashara na kwa wale wanaohitaji msaada ili waweze kufanya biashara

nchini Kongo watembelee ofisi za ubalozi watapata mwongozo utakaowawezesha kufanya biashara halali,” alisema Balozi Mella.

Mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya Demokrania ya Kongo (DRC), Moma Kampinga, alisema ziara ya wafanyabiashara wa Tanzania kwenda Kongo ilikuwa na maana kubwa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara ili kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

“Fursa ya biashara hasa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, bidhaa za vyakula ni kubwa hivyo tuna imani ziara itakapokuja kufanyika bidhaa za Tanzania zitapata soko kubwa nchini kwetu,” alisema Kampinga

KITUO CHA MABASI UBUGO

MTANZANIA lilipopita katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, abiria waliokuwa wakisafiri walionekana kunawishwa mikono kwa kutumia vitakasa mikono.

Kampuni mbalimbali zinazosafirisha abiria ndani na nje ya nchi zimechukua hatua ili kuwakinga wafanyakazi wake na abiria.

Meneja wa mabasi ya Simba Mtoto, Mohamed Said, alisema wamenunua vifaa mbalimbali ili wafanyakazi wake wajikinge na virusi vya corona.

“Tumechukua hatua ya kununua ‘mask na hand sanitizer’ ili wafanyakazi wangu pamoja na abiria wajikinge na maabukizi ya virusi vya corona,” alisema Said. 

Hata hivyo MTANZANIA lilipopita katika vituo mbalimbali vya mwendokasi bado zoezi la kunawa mikono kwa abiria lilikuwa halijaanza.

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian, Andrew Msechu na Aveline Kitomary (Dar), Janeth Mushi (Arusha), Derick Milton (Simiyu), Nyemo Malecela (Kagera) Na Francis Godwin (Iringa).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles