28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

‘Headphone zinazoingizwa nchini zichunguzwe’

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SERIKALI imeombwa kuchunguza ubora wa spika za masikio ‘headphones’ zinazoingizwa nchini ili kuhakiki iwapo zimekidhi viwango.

Ombi hilo limekuja wakati mabingwa wa masikio, pua na koo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila) walipokuwa wakieleza namna vifaa hivyo vinavyotajwa kuwa ni miongoni mwa visababishi vinavyoweza kuathiri usikivu wa masikio.

Wataalamu hao walielezea kwamba, ‘headphones’ ambazo watumiaji huzipachika ndani ya sikio ndizo zenye hatari zaidi kuliko zile zinazovaliwa nje (sehemu ya juu) ya sikio.

Akiwasilisha ombi hilo jana mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwenye Maadhimisho ya Siku ya  Afya ya Masikio na Usikivu Duniani yaliyopewa kaulimbiu isemayo ‘Chunguza Usikivu wako (check your hearing)’.

Mkazi wa Tegeta, Gabriel Mageda, alisema ana hofu kwamba ikiwa ubora wa vifaa hivyo hautafuatiliwa, siku zijazo Watanzania wengi watakuwa viziwi hususan kundi la vijana.

“Nilipofika hapa (Mloganzila) na kupewa elimu na wataalamu, nikawatafakari mno vijana kwa sababu wao ndio hasa ukipita hata barabarani utaona wana ‘headphones’ masikioni mwao.

“Waziri Ummy naomba kuwasilisha ombi langu kwako mkalitazame huko kwenye vikao vyenu, wataalamu wenu wahakiki hizi bidhaa maana kama ubora wake utakuwa haukidhi vigezo, kuna hatari ya wengi kupata matatizo ya usikivu siku zijazo,” alisema.

Akizungumza Waziri Ummy, alisema amepokea wazo hilo na kwamba atakwenda kulifanyia kazi kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora.

“Tunajitahidi kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana, sasa hivi tunaandaa sera mpya ya afya ambapo tunataka kuimarisha huduma za usikivu katika hospitali za rufaa za mikoa, kuwe na wataalamu wa kutosha, lakini kinga ni muhimu, kweli vijana wamekuwa kama ‘matahira’ wanavaa asubuhi, mchana, jioni na usiku, ni hatari.

“Sambamba na hili, zipo kumbi za starehe ambazo hawajafunga vifaa vya kuzuia kelele, lakini ipo sheria ya mazingira ambayo inaeleza kelele ni uchafuzi wa mazingira, ni muhimu kila mmoja akasimama katika nafasi yake hasa watendaji wa mitaa kuhakikisha kumbi zinafungwa vifaa,” alisema.

Alisema Shirika la Afya Duniani (WHO)  linakadiriwa zaidi ya asilimia tano ya watu duniani ambayo ni sawa na watu milioni 446, wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa usikivu. 

Alisema miongoni mwa hao, milioni 432 ni watu wazima na milioni 34 ni watoto na kwamba inatarajiwa ifikapo mwaka 2050, zaidi ya watu milioni 900 watakuwa na tatizo hilo.

Alisema katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo, inakadiriwa kuwa na watu milioni 518.

“Hii ni takriban asilimia 10 ya watu wote duniani, ambapo kati yao watoto wenye umri chini ya miaka 15 ni asilimia 46, inakadiriwa watoto milioni 1.2 kati yao wenye umri kati ya miaka 5 hadi 14 wana ukosefu wa usikivu,” alisema.

Alisema kwa sasa hapa nchini bado hawajakusanya takwimu kupata idadi ya watu wanaokabiliwa na tatizo hilo, hivyo kuwaagiza wataalamu wa Wizara kufuatilia jambo hilo.

Awali akizungumza, Kaimu Mkurugenzi wa Muhimbili-Mloganzila, Dk. Makwaia Makani, alisema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wagonjwa waliohudumiwa katika idara ya masikio, pua na koo kati ya Novemba 2018 na Januari mwaka huu ni 5,959.

Alisema kati ya hao, wagonjwa 454 sawa na asilimia nane, walikuwa na tatizo la ukosefu wa usikivu.

Alisema kwa kipindi cha 2018, takriban wagonjwa 117 walipatiwa vifaa vya kukuza mawimbi ya sauti (Hearing aids) na 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio. 

Alisema kuanzia Juni 2018 mpaka Desemba 2018, jumla ya watoto 21 wameweza kupandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlear implants).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles