MADRID, HISPANIA
NYOTA wa Chelsea, Eden Hazard, anataka kuandika historia katika timu ya Real Madrid ya kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha kuliko mchezaji mwingine katika historia ya timu hiyo.
Wababe hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanadaiwa kutenga kiasi cha pauni milioni 130, zaidi ya bilioni 378 za Kitanzania kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji raia wa nchini Ubelgiji.
Hata hivyo, wamedai endapo watafanikiwa kumsajili mchezaji huyo, basi wataanza kumpa kiasi cha pauni milioni 88 zaidi ya bilioni 256 za Kitanzania, huku fedha zingine zikitarajiwa kutolewa kwa nyakati tofauti ikiwa pamoja na sehemu ya bonasi yake.
Tayari uongozi wa timu hizo mbili umekutana kwa ajili ya kufikia makubaliano ya mwisho, hivyo siku za hivi karibuni Madrid watamtangaza mchezaji huyo ambaye ameonesha kiwango cha hali ya juu ndani ya Chelsea kwa kipindi cha miaka 7.
Madrid haijawahi kufanya usajili wa bei kubwa kufikia hiyo ambayo wanataka kuifanya, kiasi kikubwa ambacho walikitumia kwa ajili ya kumsajili mchezaji na kuandika historia ni uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham na kujiunga na Real Madrid, Septemba 2013 kwa uhamisho wa pauni milioni 86, zaidi ya bilioni 250. Akifuatiwa na Cristiano Ronaldo ambaye alijiunga na Madrid akitokea Man United kwa uhamisho wa pauni milioni 80.
Real Madrid wamekuwa wakiifuatilia saini ya Hazard tangu miaka miwili iliopita, hivyo kwa sasa dili hilo linaelekea ukingoni huku ikiwa tayari mchezaji huyo amewaaga wachezaji wenzake wa Chelsea pamoja na mashabiki baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Europa dhidi ya Chelsea ambapo aliwasaidia kulitwaa taji hilo.
Uhuamisho wa Hazard utakuwa mkubwa kwa wachezaji wa Ligi Kuu England, mchezaji ambaye anashikilia rekodi kwa sasa ni Philippe Coutinho, aliyejiunga na Barcelona miezi 18 iliopita akitokea Liverpool kwa uhamisho wa pauni milioni 145.