26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

HAWA HAPA WAZUNGU WANAOTAMANI KUWA WAFRIKA

NA JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA,

KWA miaka mingi wanawake wa Kiafrika au weusi barani humu na kwingineko duniani wamekuwa na utamaduni wa kutumia ‘cream’ kujichubua ili waonekane weupe.

Ni kasumba ya kujihisi kwamba kuwa na ngozi nyeupe unakuwa kiumbe bora zaidi, unapendwa na au kuthaminika zaidi.

Wana kasumba potofu kuwa bila kuwa weupe hawawezi kuonekana kuwa ni wanawake warembo.

Mitazamo hiyo ndiyo inayowafanya wengi kutumia vipodozi vikali kujichubua ili waonekane wazuri na wapendwe au wafanane na uzungu huku wengine wakifanyiwa upasuaji  ili kutimiza ndoto zao hizo za uzungu huo feki.

Wanawake hawaishii tu kujichubua ngozi ya sura bali pia kutumia vipodozi vikali kutengeneza nywele ili ziwe za mlalo.

Wengi wao utawaona wakizungumza kwa pozi la kutingisha kichwa mara kwa mara wakati nywele hizo zinapowalalia usoni, hali ambayo imezoeleka kwa Wazungu kutokana na aina ya nywele zao.

Japo hakuna takwimu halisi kuonyesha idadi ya wanawake wanaotumia vipodozi hivi hatari barani Afrika, mabango ya kutangaza bidhaa hizo  yamezagaa katika miji yote barani humu na kwingineko duniani.

Mbali ya wanawake, idadi ya wanaume wanaousaka uzungu nao imekuwa ikiongezeka kila uchwao na kujiweka katika hatari ya kupata maradhi mbalimbali ya ngozi pamoja na saratani, kisukari na mengineyo.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa dada zetu weusi, kuna wazungu pia wanaochizika na weusi.

Hapa tunawataja kwa ufupi wanawake wawili waliogonga vichwa vya habari kwa kuukana uzungu, 

RACHEL DOLEZAL

Miaka miwili iliyopita maisha yalikuwa yakimwendea vyema Rachel Dolezal (40). Alikuwa Rais wa Tawi la Chama cha Taifa cha Watu wa Rangi Mchanganyiko (NAACP), mwalimu wa chuo kikuu na mwenyekiti wa Tume ya Polisi ya Usuluhishi ya mji wa Spokane.

Hakika alikuwa mwanaharakati ‘mweusi’ maarufu mno wa haki za kiraia mjini Washington na kwingineko.

Tangu akiwa Rais wa NAACP na mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Howard alikuwa akidai kuwa baba yake ni mweusi.

Wanafunzi wake wa Chuo Kikuu cha Eastern Washington walimhusudu mno; mwanawe mwenye umri wa miaka 21 alikaribia kujiunga na kundi la ushawishi la watu wa rangi tofauti la mjini Washington DC; mwanawe mdogo alikuwa akifanya vyema shule ya juu wote wakiwa wa mseto wa rangi kutokana na kuzaa na mwanamume mweusi.

Lakini kulikuwa na kundi kubwa lililoifahamu fika asili yake wakiwamo wazazi wake wazungu waliokuwa hawafurahishwi na kitendo chake cha kuficha asili yake.

Jioni moja ya mwaka juzi, chombo cha habari kiliwasili kwa ajili ya kufanya naye mahojiano, Dolezal hakuwa na tatizo kwa vile kwa hadhi yake yu mtu wa mahojiano mara kwa mara.

Kwa akili yake alidhani kutakuwa na mazungumzo kuhusu uhalifu wa chuki dhidi ya watu wa rangi tofauti.

Aliulizwa; “Je, wewe ni Mmarekani mweusi?” Akiwa kama kikatuni vile, sura yake ilibadilika na kunywea. Akajibu; “sielewi swali hilo.”

Lakini mwandishi wa habari hakumkawiza, “Je, wazazi wako ni weusi?” Dolezal aligeuka kuipa mgongo kamera na kutimka kutoka mahojiano hayo.

Picha ya mkwaruzano huo ukasambaa duniani na wazazi wake Wazungu wa wakajitokeza na picha ya binti yao akiwa mdogo inayoonesha yu mzungu safi bila chembe yoyote ya weusi.

Walimlaani binti yao huyo katika vyombo vya habari kwa kuidanganya dunia kuhusu rangi yake halisi, wakisisitiza wao kwa upande wao si wabaguzi kwa vile katika familia yao wameasili watoto weusi.

“Ameishi kwa kujifanya mweusi, ilihali akijua hakuwa Mmarekani mweusi,” walisema.

Dolezal akajiuzulu wadhifa wake kutoka NAACP, akatimuliwa kutoka chuo kikuu na kupoteza kazi yake ya uandishi wa koramu gazetini na kuondoshwa kutoka tume ya polisi ya usuluhishi.

Tangu hapo akaja julikana kama mzungu mwenye uso mweusi.

Alilaaniwa si tu kwa kuficha asili yake bali pia kupora ajira isiyomstahili ya urais NAACP lakini pia akitetewa na kundi kubwa hasa la weusi lililosema anapaswa kuachwa kwa uhuru rangi aipendayo sawa na watu wanaochagua kujibadili jinsia.

Mwanaharakati huyu anayehusudu weusi na kuchukia uzungu ikiwamo dhana ya ubora wa wazungu hadi sasa hana ajira kwa kile baadhi ya waajiri wanachokiona si mkweli.

Kwa sasa amekiri kuwa alizaliwa akiwa Mzungu kwa wazazi wa Kizungu, lakini anasisitiza kwamba anajitambua kuwa ni mweusi.

Baada ya Dolezal, amejitokeza mwanamke mwingine Martina Adam, raia wa Ujerumani, ambaye anauhusudu mno weusi.

Tofauti na Dolezal ambaye alichagua kuonekana kama shombe shombe, Martina amechagua weusi tii.

Modo huyu Mjerumani kwa sasa ndiyo ‘habari ya mjini’ kwa kusaka uso mweusi katika historia ya kisasa.

Adam, akijulikana kama Martina Big kutokana na kuwa na matiti makubwa ya zaidi ya kupandikiza barani Ulaya, anadai yupo katika mwelekeo wa kuwa msichana mweusi na sasa anapitia mlolongo wa sindano za kufifisha ngozi zake kuwa nyeusi.

Na karibuni amekutana na mtaalamu za nywele za weusi ili kuzitengeneza ziwe za Kiafrika.

Martina Big amelenga mbali ya weusi kuwa na midomo mikubwa, matiti makubwa, makalio makubwa na vikorombwezo vinginevyo vya usoni kama wanawake weusi.

Martina Big tayari ametumia maelfu ya dola kwa upasuaji katika jaribio lake la kuwa mwanamke mweusi.

Mwanamitindo huyo, ameendelea kusisitiza mabadiliko ya rangi yake katika mitandao ya kijamii.

“Nina habari kubwa. Nimepiga hatua katika mageuzi yangu ya kuelekea kuwa mwanamke mweusi. Jana nilikuwa na mtaalamu wa nywele za Kiafrika na kuzitengeneza kuwa za Kiafrika.

Kuwa zaidi na zaidi mwanamke mweusi, hiyo ni hisia ya ajabu ya aina yake. Nina furaha mno. Kitakachofuata ni majadiliano ya kuongeza makalio na kuwa na uso wa Kiafrika,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles