Mwandishi Wetu
HATUA ya Shirika la Reli nchini (TRC) kurejesha safari za treni katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini baada ya kusitisha miaka 26 iliyopita, ni ya kuungwa mkono na kuiwekea mikakati.
Treni ya kwanza kufika Arusha ni ile ya mizigo iliyowasili juzi Jijini Arusha ikitokea Dar es Salaam.
Kwa sisi ambao tunatambua manufaa ya reli kwenye uchumi, tunasema hiyo ni hatua kubwa ambayo haipaswi kuishia tena njiani bali kuendelea mbele.
Tunasema hivyo tukitambua kwamba usafiri wa reli umezitoa kiuchumi nchi nyingi zilizoendelea.
Mathalani Marekani ripoti zinaonyesha; viwanda vya vyake vinategemea reli ya mizigo kwa asilimia nyingi kupata bidhaa, ikiwamo zile ghafi lakini pia kuwezesha biashara zenye nguvu kama uuzaji wa magari, wazalishaji kupata wateja wapya nakadhalika.
Ripoti ya mwaka 2018 ya nchini humo inaonyesha; katika biashara za kimataifa, usafiri wa reli umewezesha biashara nchini humo kufanyika kwa asilimia 35, na hivyo kusaidia viwanda vya Marekani kushindana kwenye uchumi duniani kote.
Zaidi usafiri wa treni umetoa ajira kwa watu wanaokadiriwa kufikia 150,000.
Mwaka 2018 nchini Marekani, reli ilitoa fidia kwa wafanyakazi, pamoja na malipo mbalimbali kwa wastani wa karibu dola 130,200 kwa mwaka, sawa na asilimia 61% zaidi ya mfanyakazi wa Marekani.
Kwenye miundombinu reli pia imeonekana mkombozi kwani treni moja inaweza kubeba mizigo ya malori mia kadhaa ya mizigo ambapo ripoti inaonyesha yanaongeza mzigo kwa taifa ikiwa ni pamoja na magari kujaa barabarani.
Moja ya ripoti za Benki ya Dunia (WB) zinaonyesha katika tasnia ya usafirishaji reli inabeba sura pana na muhimu katika uchumi.
Kwamba njia nyingine zote za usafiri zibeba sura ya kutoa huduma ingawa usafiri wa reli ni tofauti na kipekee kwani hutoa huduma zote za reli na miundombinu ya mtandao.
Zaidi huduma zinazotolewa na reli ni za juu au kubwa kwa kiwango ukilinganisha na usafiri mwingine kama wa magari.
Pamoja na hatua nyingine zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na hii ya sasa ya kufufua usafiri huo katika baadhi ya maeneo kama Kaskazini, ni wakati wa TRC na Serikali kwa pamoja kuangalia nini kilichosababisha reli kushindwa kujiendesha na baadae kushuhudia kifo cha taratibu.
Pamoja na hilo, huko mbele pengine Serikali na TRC ifikirie kuwa na sera safi itakayoruhusu uwekezaji kwenye mtandao wa reli ili kukidhi mahitaji ya soko linalobadilika.
Baadhi ya nchi zimetumia utaratibu huo kwenye reli zao na faida imepatikana pasipo serikali kutumbukiza fedha yake.
Ushauri huu inawezekana ukawa ni mgumu sasa, lakini ni vyema utafiti ukafanywa kwanza katika nchi zenye utaratibu huo ili kuona faida na hasara zake.
Tunaamini majibu sahihi ya utafiti yatawezesha uchumi wa reli katika Taifa letu kusimama tena imara na zaidi kuwa na mtandao mpana wa reli ambao utakuwa na manufaa makubwa kwenye uchumi wa nchi.