Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Michuano ya Tigopesa Mbungi ya Boda Boda Cup hatua ya 16 bora, inatarajia kuanza kutimua vumbi kesho kwenye viwanja vya Bandari, Tandika, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa vifaa, leo Desemba 7, 2023, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha na Wamiliki wa Boda Boda Mkoa wa Dar es Salaam(CMPD), Michael Masawe, amesema bingwa wa mashindano hayo atapata zawadi ya bajaji, kombe na jezi seti moja.

Amesema mshindi wa pili atachukua pikipiki aina 125 TVS ,huku wa tatu akipata pikipiki ya ya 100 TVS pamoja seti ya jezi kila mmoja
” Leo tumetangaza zawadi na tumegawa jezi kwa timu zetu 16 bora kuelekea hatua ya 16 bora inayotarajia kuanza kesho, baada ya fainali kila mmoja atachukua kile anachostahili,” amesema Masawe.
Ameeleza kuwa lengo la mashindano ni kuwakutanisha waendesha bodaboda na kutoa elimu ya masuala mbalimbali ikiwamo ya usalama barabarani na matumizi ya mfumo wa kifedha.

Naye Ofisa Maendeleo ya Biashara Lipa kwa simu kutoka Tigo, Nelson Rwehumbiza amesema wametumia nafasi ya michaano hiyo kuwaendeleza kiuchumi wafanyabiashara wa usafirishaji ili kuweza kutumia Tigopesa kutunza fedha zao.
“Nia ya Tigopesa ni kuwaendeleza kiuchumi madereva wote waliopo kwenye sekta ya usafirishaji. Tunajua malipo ya fedha tasilimu si salama,pia hatutawapa huduma ya Lipa kwa Simu tu bali tutawapa na huduma za mikopo na bima,” amesema Rwehumbiza.
Kwa upande wa Nahodha wa timu ya CCM Kigamboni, Musellem Omary ‘Dunga’ ametamba kuwa wataondoka na ubingwa huo kwa sababu ya ubora waliokuwa nao, kwani tangu mwanzo mashindano hawajapoteza mechi.