MALEZI  ni matendo muhimu yanayofanywa na wazazi, walezi na jamii kwa lengo la kumlea, kumkuza, kumlinda, kumuendeleza mtoto kimwili, kiakili, kijamii, kihisia na kimaadili ili aweze kuishi, vizuri na kukubalika miongoni mwa jamii husika.
Malezi hayo humsaidia mtoto kukua katika misingi muhimu ambayo imeambatana na mambo yafutayo:
Afya
Ili mtoto awe na afya bora, anahitaji kupatiwa kinga zote dhidi ya maradhi ya kuambukiza kwa njia ya chanjo na kupatiwa tiba mara anapougua, pia mazingira yanayomzunguka mtoto hayana budi kuwa katika hali ya usafi na usalama wakati wote. Mazingira hayo ni pamoja na mahali anapolala, sehemu anazocheza, mavazi na vyombo anavyotumia.
Lishe
Ili mtoto aweze kukua vizuri kimwili na kiakili anahitaji chakula bora au mlo kamili unaojumuisha vyakula vyenye virutubisho kama protini, wanga, mafuta, vitamini na madini. Chakula bora ni lazima mtoto akipate toka akiwa tumboni mwa mama yake mara baada ya kuzaliwa apatiwe maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza, baada ya miezi hiyo apatiwe vyakula vya kuridhika.
Furaha ya mtoto au uchangamfu
Uchangamfu ni matendo au mwelekeo anaoonyesha mzazi au mlezi kwa mtoto kwa lengo la kuchochea ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili, kimaono, kihisia na kimaadili, ambao huanza tangu akiwa tumboni kwa mama na kuendelezwa baada ya kuzaliwa.
Uchangamfu katika kipindi hiki huchangiwa kwa kiwango kikubwa na hali ya afya ya mama. Mjamzito anahitaji matunzo kimwili, kijamii na kisaikolojia ili mtoto aliyeko tumboni aweze kukua katika mazingira salama. Inashauriwa mjamzito kutojihusisha na ulevi wa pombe, dawa za kulevya, uvutaji wa sigara na vile vile kujiepusha na magonjwa ya kuambukiza. Mtoto anapokosa uchangamfu huishia kuwa katili badaye.
Ulinzi
Ulinzi unajumuisha vitendo vitakavyowezesha kuhakikisha kuwa mtoto yuko katika hali ya usalama ili kulinda uhai na maendeleo yake. Vitendo hivyo vinajumuisha kumpatia mahitaji muhimu kama vile chanjo dhidi ya magonjwa, chakula chenye virutubisho vyote na tiba mara anapougua, ulinzi na usalama, kumpakata, kuzungumza naye na kucheza naye.
Hivyo, inashauriwa kuwa ni vyema mtoto apewe uangalizi wa kutosha ili kumwepusha na ajali na mazingira hatarishi yatakayoathiri afya yake, kupata ajali au kufanyiwa vitendo viovu kama kubakwa.
Pamoja na hayo, ni muhimu wazazi au walezi na jamii kuelewa kuwa kuna hatua muhimu za ukuaji ambazo kila mtoto hupitia na katika kila hatua kuna tabia ambazo mtoto huonyesha na ni muhimu wazazi au walezi na jamiii kujua na kuzizingatia.
Hata hivyo, walezi na wazazi ni muhimu kujua kuwa miaka mitano ya kwanza ya maisha ya mtoto ni muhimu kwa malezi ya utu uzima wa baadae, hivyo ni lazima kudhibitiwa ili kukidhi mahitaji ya kijamii, migogoro na kanuni za kijamii.
Hatua tano muhimu ambazo mtoto lazima apitie na iwapo hayatafanyika, hali hizo huhifadhiwa katika mawazo yake ya kina na hivyo kumsababishia matatizo makubwa ukubwani.
Hatua ya kwanza – oral stage (0-2 miaka)
Hatua hii huwahusu watoto kuanzia siku moja mpaka miaka miwili. Katika hatua hii ya kwanza, furaha na raha ya mtoto huwa imejificha mdomoni. Utakuta mtoto kila wakati anafurahia kunyonya maziwa ya mama yake, vidole au midoli. Mtoto anatakiwa atumie mdomo wake mpaka ile hamu yake yote iishe. Kama ni kunyonya basi aendelee kufanya hivyo mpaka pale utakapofika wakati mzuri wa kumwachisha ziwa. Kumnyanyasa mtoto wakati ananyonya au kumfanyia vitendo ambavyo si vya kiungwana ikiwa ni pamoja na kumwachisha ziwa mapema, husababisha hamu yake ya kuutumia mdomo ibaki na hivyo kuhifadhiwa kwenye mawazo yake ya kina. Anapokua hulipa kisasi bila kujua kwa kuutumia mdomo kwa kadri anavyoweza. Hivyo, anapokuwa mtu mzima anaweza akawa muongo, mlevi kupindukia, mvuta sigara, muongeaji au mmbeya. Kama kuna watu unawafahamu wenye tabia hizi, jaribu kupeleleza kama walinyonyeshwa bila kunyanyaswa au kama hamu yao ya kunyonya iliisha, hii ni muhimu wazazi na walezi kujua umuhimu wa hatua hii kwa mtoto yeyote.
Hatua ya pili – Anal Stage(miaka 2-3):
Hatua hii humhusu mtoto wa miaka miwili au mitatu. Matumizi ya mdomo huwa yamekwisha na raha huhamia sehemu za haja. Katika hatua hii, mtoto hupendelea zaidi kutumia sehemu zake za haja kwa kukojoa au kwenda haja kubwa mara kwa mara. Katika kipindi hiki wazazi wengi hufanya makosa. Mzazi anashauriwa kuwa makini kwa kutoa mafunzo mazuri kwa mtoto wake, kumfundisha jinsi ya kujisaidia au kutumia potti na si kumvalisha pampasi muda wote kwa kuwa hatojifunza matumizi ya choo. Mlezi anaposhindwa kumfundisha mtoto matumizi ya kijisaidia, humfanya mtoto awe na tabia ya kujifanyisha na hivyo kuwa na hali mbaya ukubwani. Mtoto aliyenyimwa huduma hii akiwa katika hatua hiyo hubakiwa na deni, anapokuwa mkubwa anaweza kupata matatizo, wengine huwa wazembe na huwa na tabia fulani fulani ambazo zinahitaji msaada mkubwa wa wengine. Kuna haja kubwa ya walezi na wazazi kuzielewa hatua hizi muhimu za makuzi kwa mtoto.