Ramadhan Hassan -Dodoma
IKIWA zimebaki siku chache kabla ya Bunge kuvunjwa Juni 16, na mchakato wa uchaguzi mkuu kuanza, hatma ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ipo mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Hali hiyo inatokana na uchunguzi uliotangazwa jana na taasisi hiyo kuhusu fedha ambazo wabunge wa chama hicho wamekuwa wakikatwa na kupelekwa kwenye chama.
Wakati ikielezwa kuwa baadhi ya viongozi wamehojiwa, sasa kwa mara nyingine Takukuru imetangaza kuhoji wabunge 69 wakiwamo waliopo Chadema na waliowahi kuhudumu kupitia chama hicho.
Mwishoni mwa Mei, Takukuru ilisema imeanza kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha Chadema.
Hatua hiyo imetokana na madai yanayotolewa na baadhi ya wabunge kuhusu matumizi mabaya ya fedha walizochanga kila mwezi kwa mujibu wa katiba yao.
Kwa siku za karibuni, shutuma hizo zilitolewa na wabunge wa viti maalumu, Susan Maselle, Joyce Sokombi na Peter Lijualikali wa Kilombero ambao wote wametangaza kukihama chama hicho.
Pia Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alinukuliwa akisema hatua zimechukuliwa dhidi ya tuhuma hizo, ikiwamo kuwahoji wanachama waandamizi na viongozi wa Chadema, wabunge waliotoa tuhuma hizo na maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema taasisi hiyo imeshaanza kukusanya nyaraka mbalimbali zinazohusiana na tuhuma hizo.
WABUNGE 69 KUHOJIWA
Jana Takukuru ilisema leo inatarajia kuanza kuwahoji watu 69 ambao ni wabunge ama wamewahi kuwa wabunge wa Chadema, kuhusiana na ubadhirifu na ufujaji wa fedha na matumizi mabaya ya mamlaka yanayodaiwa kufanywa na chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana, wabunge hao walitarajiwa kuanza kuhojiwa jana, lakini suala hilo liliahirishwa.
MTANZANIA ilikuwepo eneo la Ofisi za Makao Makuu ya Takukuru jirani na Uwanja wa Jamhuri jijini hapa kushuhudia jinsi ambavyo wabunge hao wangetinga katika ofisi hizo, lakini majira ya mchana ofisa mmoja wa taasisi hiyo alisema wangehojiwa leo.
Taarifa ambayo ilikuwa imetolewa awali na Takukuru na kusainiwa na Ofisa Uhusiano wake, Doreen Kapwani, ilieleza mahojiano hayo yatakayofanyika ofisi za Takukuru makao makuu jijini hapa yanatarajia kukamilika wiki ijayo.
“Kwa taarifa hii, tunapenda kuuthibitishia umma kwamba ni kweli kuwa Takukuru makao makuu imewaita waheshimiwa wabunge wa Chadema na waliowahi kuwa wabunge wa chama hicho kwa mahojiano,” ilisema taarifa hiyo.
Ilifafanua kuwa hatua hiyo inafanyika ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi unaoendeshwa na Takukuru makao makuu, wa malalamiko dhidi ya matumizi ya fedha za chama hicho na kwamba hatua iliyopo sasa ni ya kuwahoji wabunge 69, wanachama na waliowahi kuwa wanachama wa chama hicho.
Pia taarifa hiyo ilisema fedha hizo ni zile ambazo zililalamikiwa na wabunge wa chama hicho waliotangaza kukihama, ambao katika malalamiko yao walidai kwamba walikuwa wakikatwa fedha katika mishahara yao kila mwezi kuanzia Juni 2016.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, kila mwezi wabunge wa viti maalumu walikuwa wakikatwa kiasi cha Sh 1,560,000 na wabunge wa kuchaguliwa kwenye majimbo Sh 520,000 na kwamba hawakuwa wakifahamu namna ambavyo fedha hizo zimekuwa zikitumika.
“Kwa hiyo, tunapenda kujulisha umma kwamba kama ambavyo Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Bregedia Jenerali Mbungo alivyoviambia vyombo vya habari Mei 27, 2020 ni kwamba uchunguzi dhidi ya tuhuma hii tayari ulishaanzishwa na baadhi ya wahusika walishaanza kuhojiwa,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema kuwa wanafanya hivyo kwa kuwa yawezekana katika tuhuma hii kukapatikana makosa, ikiwemo ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama na matumizi mabaya ya mamlaka.
“Makosa haya yote yanaangukia katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007 ambayo ndiyo inayoongoza chombo chetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilisema hadi sasa tayari Takukuru wamefanya mahojiano na viongozi wa Chadema, viongozi waliowahi kuwa Chadema, wabunge waliotoa taarifa na maofisa wa NEC.
Wengine ni viongozi wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema na sasa wanawahoji wabunge wanachama wa chama hicho pamoja na wabunge waliowahi kuwa wanachama.
Kutokana na tuhuma hizo, Mei 23, 2020, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, alisema hakuna uthibitisho unaoonyesha chama hicho kina matumizi mabaya ya fedha.
Alisema fedha za michango ya wabunge na zinazotoka kwa wadau wengine wa Chadema, matumizi yake hupangwa na vikao vyake vya chama, wakati bajeti ya matumizi hayo ikipitishwa na Baraza Kuu, kisha taarifa zake hutolewa na Kamati Kuu.
Kigaila alisema ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inakagua taarifa za matumizi ya Chadema na kwamba kwa mujibu wa ukaguzi huo, hakuna ushahidi kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.