Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imekataa maombi ya Jamhuri ya kutaka kuwasilisha majibu ya kiapo katika maombi ya dhamana ya mwandishi wa habari za uchunguzi Erick Kabendera Agosti 7, mwaka huu.
Jamhuri wamekutana na kikwazo hicho leo Alhamisi saa tatu asubuhi mbele ya
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile anayesikiliza maombi hayo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai maombi hayo yaliwafikia jana na leo shauri linakuja kwa mara ya kwanza hivyo anaomba apewe muda wa kuwasilisha kiapo cha majibu kinzani Agosti 7 mwaka huu kwa sababu kesho atakuwa Mahakama Kuu katika kesi nyingine.
Wakili wa mwombaji, Shilinde Swedy alidai mteja wake yuko chini ya ulinzi kwa
zaidi ya saa 24, hajapata uwakilishi wa aina yoyote hivyo aliomba kesi ije
Jumatatu.
Hakimu Rwizile alisema kwa kuwa maombi yamekuja chini ya hati ya dharura, muda
ulioombwa na Jamhuri ni mrefu, hivyo maombi hayo yatasikilizwa Agosti 5, mwaka
huu.
“Maombi yatasikilizwa Agosti 5, mwaka huu siku ya Jumatatu saa saba mchana,
wajibu maombi watajibu wakati wowote kabla ya muda huo,” amesema Hakimu
Rwizile.
Mwisho