HATIMA YA WABUNGE WALIOVULIWA UANACHAMA CUF MIKONONI MWA NDUGAI

0
462

WABUNGE nane wa Chama cha Wananchi (CUF), hatarini kupoteza ubunge endapo Spika Job Ndugai ataridhia ombi la barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba baada ya kuwafuta uanachama wabunge hao.

Spika Ndugai amekiri kupokea barua hiyo ambayo pamoja na mambo mengine imeainisha makosa sita yakiwamo wabunge hao kukihujumu chama hicho katika uchaguzi wa marudio wa madiwani Januari 22, mwaka huu na kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa chama hicho na Katibu Mkuu wake ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya.

Makosa mengine ni kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupanga operesheni waliyoiita ‘Ondoa Msaliti Buguruni’ wakiwa na lengo la kumuondoa Mwenyekiti wa chama hicho kinyume na Katiba ya CUF na Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 na kulipia pango na kufunga Ofisi ya Magomeni bila kufuata za kukatiba.

“Napenda kuuarifu umma kuwa suala la kuwaondoa uanachama ni utashi wa vyama vyenyewe, na kila chama kina utaratibu wake, hivyo bado naendelea kuitafakari barua hiyo na taarifa rasmi kuhusu maamuzi ya Spika kwa wabunge waliofukuzwa nitaitoa baadaye,” amesema Spika katika taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Bunge.

Wabunge hao Riziki Shahali Ngwali, Saverina Mwijage, Salma Mwassa, Saumu Sakala, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari, Halima Ali Mohammed, Khadija El Kassim ambao wote ni wabunge wa viti maalumu pamoja na madiwani wawili wa Viti Maalumu, Elizabeth Magwaja na Leila Hussein, walitangazwa kuvuliwa uanachama juzi na Profesa Lipumba kwa makosa yanayodaiwa ya kinidhamu kwa uamuzi wa Baraza Kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here