31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Hatima ya Aussems kujulikana leo

Theresia Gasper -Dar es salaam

NAFASI ya Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, kuendelea kukinoa kikosi hicho inatarajia kujulikana leo baada ya maelezo yake kufikishwa ngazi za juu.

Juzi Aussems aliwekwa kitimoto na Kamati ya Maadili ya Simba kutokana na kudaiwa kuondoka nchini bila ya kutoa taarifa.

Kocha huyo aliondoka nchini kwa muda wa siku tatu, na kudai kuwa anakwenda kwao kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia huku akiujulisha uongozi kwa barua pepe kwamba atarejea kuendelea na programu mara baada ya kurejea, kitendo kilichochukuliwa kama ni utovu wa nidhamu.

Mara baada ya kurejea Aussems aliendelea na majukumu yake na kuisimamia timu hiyo katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ambao walipata ushindi wa mabao 3-0, katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo Uongozi wa Simba ulimsimamisha Aussems kuendelea kukinoa kikosi hicho na majukumu hayo kupewa kocha msaidizi Denis Kitambi.

Akizungumza na MTANZANI jana, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alisema, wao hawana taarifa zozote kuhusiana na maamuzi ya kikao hicho hadi hapo Bodi ya Wakurugenzi itakapotoa tamko.

“Baada ya juzi kukaa kikao na Kamati ya Maadili, maelezo hayo yalipelekwa uongozi wa juu, ambako kesho (leo), Bodi inaweza kutoa taarifa kuhusiana na kikao hicho walichokaa,” alisema.

Katika hatua nyingine kikosi hicho jana kiliendelea na mazoezi chini ya kocha Kitambi, ikiwa ni moja ya kujiweka fiti na leo wataendelea na mazoezi ya Gym.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles