26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HATARI UNAYOWEZA KUIPATA UNAPOTUMIA BIDHAA ZA PLASTIKI

 

 

Na MWANDISHI WETU,

MAISHA ya mwanadamu kwa  sasa yanategemea mno  bidhaa za plastiki katika kuhifadhia  mizigo mbalimbali ikiwamo vyakula, maji na mafuta ya kula.

Licha ya kutumika katika matumizi mbalimbali katika kuhifadhia vitu, imebainika kuwa plastiki ina madhara makubwa katika matumizi ya binadamu.

Utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Madaktari wa Marekani ulitoa tahadhari kuhusu matumizi ya vyombo vya plastiki vinavyotumika kufungashia na kubebea vyakula.

Wanasayansi hao wanasema plastiki ina madhara makubwa endapo ikikutana na joto kali na kutoa kemikali iitwayo BPA(bisphenol A).

Mwaka jana, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na  Mazingira, January Makamba alipiga marufuku moja kwa moja, utengenezaji, usambazaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia mwaka huu.

Makamba alisema mifuko ya plastiki imekuwa na changamoto kubwa ya mazingira kwa kuwa sehemu kubwa ya mifuko hiyo hutolewa bure na kusambaa ambapo husababisha  mafuriko na athari nyingine kubwa za kimazingira.

Anasema ofisi yake inakamilisha majadiliano ndani ya serikali na baadae kuwahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku moja kwa moja matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.

Anasema serikali itatoa muda kwa waliojiajiri na kuajiriwa kwenye biashara ya mifuko ya plastiki kujiandaa kuacha shughuli hizo na itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.

 “Tumetuma wataalamu wa serikali katika nchi zilizofanikiwa kwenye jambo hili ili kujifunza namna bora ya kulitekeleza jambo hili,” anasema Makamba.

Nchi ya Rwanda na  Zanzibar zimefanikiwa katika upigaji marufuku wa mifuko ya rambo baada ya kuonekana ni chanzo cha uchafuzi wa mazingira na mafuriko kutokana na mifuko hiyo kuziba katika mitaro.

Licha ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko plastiki, vyombo vya plastiki aina ya sahani, bakuli, vikombe vimeendelea kutumika huku viwanda vikizidi kuvizalisha kwa wingi hivyo kufanya afya ya mwanadamu kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya saratani.

Walter Miya ni Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania, anasema plastiki imetengenezwa kwa kemikali zaidi ya 200 ambazo  zinaweza kusababisha aina 100 za saratani.

Anasema toka matumizi ya plastiki yazidi kuongezeka nchini, ugonjwa wa saratani nao umeongezeka  hasa kwa upande wa akina mama  ambapo ugonjwa huu huharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususani kwa watoto ambao bado hawajazaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kushindwa kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa wa tabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanyakazi vizuri.

Anasema kutokana na utafiti mdogo walioufanya inaonesha kuwa asilimia 60 ya saratani zimesababishwa na matumizi ya vifaa vya plastiki.

“Watu wengi wanatumia vifaa vya plastiki bila kujua madhara yake, ukienda majumbani utakuta wanawake wengi wanachemsha maji na kuyahifadhi katika ndoo za plastiki yakiwa bado ya moto.

“Baada ya muda ukija kuchunguza ile ndoo utakuta ina mabaka mabaka maana yake imeshatoa kemikali nyingi na athari hutoiona kwa muda huu, mpaka ifike miaka 10 au 15 na ndio maana huwezi kugundua saratani yako imesababishwa na nini,” anasema Miya.

Anasema pia kuna kinamama ambao hutumia mifuko ya rambo kufunikia wali wakati wa kupika ili uweze kuiva haraka bila kujua kuwa mifuko  hiyo ina athari kubwa kutokana na kemikali zilizopo kuingia katika chakula hicho.

Miya anasema jamii inapaswa kupunguza matumizi ya plastiki au kutumia zilizo na viwango ambavyo hazitoleta madhara na kwa upande wa wachemshao maji wanapaswa kusubiri hadi yapoe ndipo wamimine katika ndoo.

“Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na watu mbalimbali, bado jamii haina uelewa kuhusiana na vifaa hivyo vya plastiki.

“Hivi karibuni kuna taarifa ilisambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa watu wasitumie vikombe vya plastiki, sahani, bakuli na hata mifuko ya rambo katika matumizi ya vyakula, lakini ukipita mitaani utakuta bado wanaendelea navyo,” anasema Miya.

Anasema kuna vitu vingi ukiviangalia unaweza ukaogopa ila huwezi kuvikimbia ni kuangalia ni namna gani tunaweza kuvipunguza ili athari ya saratani isizidi kuongezeka.

“Binafsi natembea na kontena langu la aina ya glass ili kuweza kuhifadhia chakula pindi ninapoenda kununua , nimeamua kutembea nalo kutokana na mama lishe wengi kutumia vyombo vya plastiki katika kuwekea chakula,” anasema.

 “Kutokana na kukithiri kwa matumizi ya  plastiki wakati serikali ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, tunahitaji sera na sheria dhidi ya matumizi ya vifaa hivi.

“Inatakiwa iwepo sera ya kutoruhusu kusafirisha maji bila kuwa na vifaa vinavyodhibiti joto kama wafanyavyo wanaposafirisha maziwa,” anasema Miya.

Anashauri iwepo sheria ya kuwadhibiti wauzaji wa  maji juani kuanzia asubuhi hadi jioni kutokana na kupata kemikali nyingi inayotoka kwenye chupa za plastiki kwa sababu ya kuwapo juani kwa muda mrefu. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles